Ikulu ya Misri tarehe 2 huko Cairo ilitoa taarifa ikisema kuwa, rais Hosni Mubarak ametoa mwaliko rasmi kwa mfalme Abdullah wa pili wa Jordan, waziri mkuu wa Israel Ariel Sharon na mwenyekiti wa mamlaka ya utawala wa Palestina Mahmoud Abbas, kwenye mkutano wa wakuu wa pande nne tarehe 8 huko Sharm el Sheikh ya Misri. Hivi sasa pande tatu zinazohusika zimekubali kikanuni kuhudhuria mkutano huo.
Miaka mingi iliyopita, Misri siku zote inachukuliwa na jumuiya ya kimataifa kuwa kiongozi wa dunia ya kiarabu, na inafanya kazi muhimu katika eneo la mashariki ya kati na dunia ya kiislamu. Hivi karibuni Misri imetumia fursa ambayo huenda maendeleo makubwa yatapatikana katika mchakato wa amani ya Palestina na Israel, imefanya juhudi nyingi za kidiplomasia kwa ajili ya kuimarisha hadhi yake ya nchi kubwa ya kidiplomasia katika eneo la mashariki ya kati. Wachambuzi wanaona kuwa, kama mkutano wa tarehe 8 mwezi huu mkutano kati ya Sharon na Abbas utafanyika bila matatizo, huu utakuwa mkutano wa kwanza kati ya viongozi hao wawili tokea mwezi Juni mwaka 2003, umuhimu wa mkutano huo unaonekana dhahiri. Ndiyo maana mkutano huo unaweza kuifanya dunia nzima ifuatilie juhudi za kidiplomasia zinazofanywa na Misri katika kusukuma mbele mchakato wa amani kati ya Palestina na Israel.
Hali halisi imeonesha kuwa, ili kuonesha umuhimu wake katika mchakato wa amani ya Palestina na Israel, na kupata heshima ya kuwa nchi mwenyeji wa mkutano wa wakuu kati ya Palestina na Israel, Misri imefanya juhudi kubwa za muda mrefu kabla ya hapo.
Kwanza Misri ilijitahidi kusuluhisha migongano ndani ya Palestina, kuondoa hitilafu kati ya makundi yenye msimamo mkali na makundi yenye msimamo wa kati, na kuyashawishi makundi ya Hamas, Jihad na mengineyo kukubali kusimamisha vita dhidi ya Israel. Hivi sasa duru jipya la mazungumzo ya maafikiano kati ya makundi mbalimbali ya Palestina linafanyika nchini Misri. Makundi mbalimbali ya Palestina yanatazamiwa kufikia kauli moja kuhusu kusimamisha vita dhidi ya Israel baada ya kumalizika kwa mkutano huo.
Aidha, Misri imerekebisha kwa wakati sera yake ya kidiplomasia kutokana na hali mpya ya mashariki ya kati baada ya kufariki dunia kwa mwenyekiti Yasser Arafat, na ikafanya juhudi za kuboresha uhusiano na serikali ya Ariel Sharon ya Israel. Mwanzoni mwa mwezi Desemba mwaka jana, Misri ilimwachia huru jasusi wa Israel aliyefungwa kwa miaka mingi, ikaondoa kikwazo kikubwa kwa uhusiano kati yake na Israel. Siku chache baadaye, Misri na Marekani na Israel zilisaini "Mkataba wa QIZ" kuhusu sehemu ya viwanda, mkataba huo umechukuliwa kuwa ni mkataba muhimu kabisa wa ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara tangu kuanzishwa kwa uhusiano wa kibalozi kati ya Misri na Israel.
Zaidi ya hayo, Misri imechukua msimamo wa kushirikiana na mpango wa hatua za upande mmoja wa serikali ya Sharon. Kwa upande mmoja, Misri inasisitiza kuwa lazima kuuweka mpango huo kwenye mpango wa amani ya mashariki ya kati, kwa upande mwingine, Misri pia inafanya maandalizi ili kukabiliana na hali baada ya jeshi la Israel kuondoka kutoka ukanda wa Gaza, na imeahidi kuwa itashirikiana vizuri na pande mbili Palestina na Israel kuhusu kazi mbalimbali baada ya jeshi la Israel kuondoka huko, juhudi hizo za Misri zimeaminiwa na kusifiwa na Palestina na Israel.
Misri inajua vilivyo kuwa kama ikitaka kuonesha umuhimu wake katika mchakato wa amani ya mashariki ya kati, inapaswa kuungwa mkono na Marekani. Ili kuondoa migongano na Marekani, Misri ilipendekeza kuitisha mkutano wa kimataifa kuhusu suala la Iraq na kuunga mkono uchaguzi mkuu wa Iraq, msimamo wake umelingana na mahitaji ya kimkakati ya Marekani kuhusu suala la Iraq, pia umesaidia kuondoa migongano mikubwa kati ya Misri na Marekani kutokana na vita vya Iraq, ambapo Marekani ingeisaidia Misri kuonesha umuhimu wake zaidi katika mchakato wa amani ya Palestina na Israel.
Idhaa ya Kiswahili 2005-02-03
|