Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-02-04 14:15:42    
Fursa ya kuleta amani ya mashariki ya kati yaonekana tena

cri

Serikali ya Misri tarehe 2 ilitangaza kuwa, kutokana na pendekezo la rais Hosni Mubarak wa Misri, wakuu wa nchi nne za Palestina, Israel, Misri na Jordan watafanya mkutano kuhusu amani ya mashariki ya kati huko Sharm el Sheikh, Misri, ambapo mwenyekiti wa mamlaka ya utawala wa Palestina na waziri mkuu wa Israel watahudhuria mkutano huo. Huu utakuwa mkutano wa kwanza wa moja kwa moja kati ya viongozi wakuu wa Palestina na Israel tokea mwezi Oktoba mwaka 2000, ambao unafuatiliwa sana jumuiya ya kimataifa.

Mkutano huo una umuhimu mkubwa wa kisiasa usio wa kawaida. Tokea mwezi Oktoba mwaka 2000, Palestina na Israel zilijitumbukiza katika duru jipya la migogoro ya kimabavu na kusababisha mchakato wa amani ya mashariki ya kati urudi nyuma vibaya. Kuchukua hatua za kimabavu kupambana na vitendo vya kimabavu, kuwaangamiza wapinzani mmoja baada ya mwingine, kufanya mashambulizi kwa kurusha makombora na kujenga ukuta wa kutenganisha pande mbili, yote hayo yalionesha kuwa mchakato wa mabadiliko ya uhusiano kati ya Palestina na Israel. Baada ya kufariki dunia kwa Yasser Arafat aliyekuwa mwenyekiti wa mamlaka ya utawala wa Palestina mwezi Novemba mwaka jana, dalili ya kuleta amani ilionekana katika uhusiano kati ya Palestina na Israel. Katika uchaguzi mkuu wa Palestina uliofanyika mwezi Januari, walichaguliwa viongozi wa awamu mpya wa Palestina wakiongozwa na Mahmoud Abbas. Baada ya kushika madaraka, Bwana Abbas amechukua hatua mbalimbali zenye unyumbufu kwa kuanzisha upya mchakato wa amani ya mashariki ya kati, ambapo alifanikiwa kufanya mazungumzo na makundi mbalimbali ya kijeshi ya Palestina na kuyashawishi yasimamishe vita kwa muda dhidi ya Israel, pia aliweka kikosi cha usalama kwenye ukanda wa mipaka kati ya Gaza na Israel ili kuwazuia watu wenye msimamo mkali wasishambulie shabaha ya Israel. Israel iliitikia juhudi hizo za Palestina. Wakati huo huo, jumuiya ya kimataifa pia imeongeza juhudi za kusukuma mbele amani ya mashariki ya kati. Yote hayo yameweka msingi kwa ajili ya mkutano wa Sharm el Sheikh.

Mkutano wa wakuu wa Palestina na Israel hakika utasukuma mbele kwa nguvu pande hizo mbili zijenge upya uaminifu na kuweka msingi kwa ajili ya kurudisha mazungumzo ya amani na kufufua utekelezaji wa mpango wa amani ya mashariki ya kati. Vyombo vya habari vilitoa maelezo yakisema kuwa, mkutano huo wenyewe ni mafanikio makubwa bila kujali mkutano huo utapata maendeleo halisi au la. Hivi sasa pande mbili za Palestina na Israel zote zina matarajio makubwa kwa mkutano huo. Waziri mkuu wa mamlaka ya utawala wa Palestina Ahmed Qurei alisema kuwa, mkutano huo ni hatua kubwa ya kuanzisha upya mazungumzo ya amani kati ya Palestina na Israel. Israel pia inatumai kuwa mkutano huo utakuwa mwanzo mpya wa uhusiano kati ya pande hizo mbili.

Watu wanaweza kusema kuwa, kwenye mkutano huo migongano kati ya Palestina na Israel hakika itaonekana dhahiri. Kwani kabla ya kufanya mkutano huo, migongano imetokea kati ya pande hizo mbili kuhusu ajenda za mkutano. Israel inataka Palestina kuacha mashambulizi ya kijeshi dhidi Israel, na inataka mkutano ujadili hasa suala la usalama; Palestina inataka kuweka utekelezaji wa mpango wa amani ya mashariki ya kati kwenye ajenda ya mkutano. Aidha, kama nguvu zenye siasa kali za pande hizo mbili zitazusha migogoro na kuweka vikwazo kwa mkutano huo au la, hili bado halijukani.

Kutatuliwa vizuri au la kwa suala la Palestina kunahusiana moja kwa moja na mambo makuu ya amani ya mashariki ya kati, kwa maana hiyo, mkutano wa wakuu wa pande nne wa Sharm el Sheikh hakika ni fursa muhimu katika kuleta amani ya mashariki ya kati.

Idhaa ya kiswahili 2005-02-04