Shirika la biashara duniani WTO linafanya mazungumzo ya wiki moja huko Geneva kuanzia tarehe 7. Kwa kuwa suala la kilimo ni ajenda kuu ya mazungumzo ya Doha, ambalo ni muhimu katika kuathiri ajenda nyingine, hivyo suala la hilo linafuatiliwa sana na watu.
Kutokana na ratiba iliyowekwa, nchi wanachama wa WTO zingefikia makubaliano kuhusu aina ya utaratibu halisi wa upunguzaji wa ruzuku na masuala mengine ya duru jipya la mazungumzo ya kilimo kabla ya mwishoni mwa mwezi Machi mwaka 2003; na mazungumzo yote yangemalizika kabla ya tarehe 1 Januari mwaka 2005. Basi sababu za kukwamisha mazungumzo hayo mara kwa mara ni zipi? Kwa kweli ni kutokana na maslahi mbalimbali tofauti ya nchi wanachama .
Nchi ya Marekani yenye uwezo mkubwa wa ushindani wa mazao ya kilimo ilijaribu kutumia mazungumzo kusukuma mbele biashara huria ya mazao ya kilimo, kufuta ruzuku kwa mazao zinazouzwa nje na kupunguza ushuru wa forodha. Na nchi za Umoja wa Ulaya kama vile Sweden, Norway na nchi nyingi kama Japan na Korea ya kusini zilijaribu kudumisha kwa ziwezavyo hifadhi na misaada kwa kilimo na kutetea kuendelea kuchukua aina ya mazungumzo ya Uruguay, na kuzipatia nchi wanachama unyumbufu zaidi. Na nchi nyingi wanachama zilitetea kuwapa wanachama wa nchi zinazoendelea huduma maalum, na kulenga zaidi kubadilisha hali iliyopotoshwa ya biashara ya mazao ya kilimo kutokana na utoaji ruzuku na misaada ya wanachama wa nchi zilizoendelea.
Kutokana na maslahi mbalimbali tofauti, kundi la nchi zinazouza nje mazao ya kilimo la Cains linaloongozwa na Australia na nchi ya Marekani ziliulaani Umoja wa Ulaya kwa utoaji ruzuku wake mkubwa wa dola za kimarekani milioni kadhaa, na Umoja wa Ulaya, Japan na Uswisi zinazilaani nchi hizo kutoweza kuzingatia ipasavyo hifadhi ya mazingira na sababu zisizo za kibiashara, hata Umoja wa Ulaya uliilaani Marekani kutoa "ruzuku za siri" kama vile kutoa mikopo kwa uuzaji mazao nje na kutoa ruzuku kwa chakula. Pande mbalimbali muhimu za mazungumzo hayo zililaumiana na kujibizana vikali, hivyo mazungumzo yalikwama mara kwa mara.
Baada ya kushindwa kwa mazungumzo ya Cancun mwezi Septemba mwaka 2003, mazungumzo yaliyopangwa awali kuhusu kilimo yalifutwa, na kila upande hautaki kubeba lawama, ila tu kueleza maoni na misimamo kwa kuchukua misimamo mbalimbali. Mpaka mwezi Machi mwaka 2004, Baraza kuu la Shirika la biashara duniani lilipothibitisha ratiba ya mkutano wa kamati maalum ya kilimo, ndipo mazungumzo ya kilimo yalipoanza kuwa "mazungumzo halisi" badala ya "maelezo ya kisiasa", na pande mbalimbali muhimu za mazungumzo hayo zilifanya juhudi za kufanya mazungumzo mara 5, hasa mwishoni zilifanya mashauriano ya saa zaidi ya 40 kwa mfululizo, zikafikia makubaliano kuhusu aina ya mazungumzo ya kilimo tarehe 1 Agosti mwaka 2004.
Katika makubaliano hayo, nchi zilizoendelea zimeahidi kuthibitisha tarehe ya kufuta ruzuku zao kwa mazao ya kilimo na kupunguza asilimia 20 ya misaada ya nchini mwao iliyopotosha biashara ya kilimo. Kuhusu kuyaruhusu mazao kuingia kwenye soko, makubaliano hayo yameweka kanuni kuhusu ushuru wa forodha, na kutambua "mazao maalum" ya nchi zinazoendela yanayostahili kupewa kipaumbele.
Lakini wachambuzi wanaona kuwa mustakbali wa mazungumzo hayo bado haufurahishi. Kwani pande mbalimbali bado zina maoni tofauti kuhusu ajenda ya mazungumzo; tokea mwaka huu uanze nchi nyingi wanachama zimelalamika kuwa hali ya uwazi haionekani katika mazungumzo hayo, ambapo nchi chache zinataka kuzilazimisha nchi nyingine wanachama nia yao; aidha makubaliano ya mwaka jana yalikwepa masuala mengi ya sugu. Hivyo mazungumzo ya kilimo bado yanakabiliwa na changamoto kubwa na yanatakiwa kukabiliana na taabu nyingi kubwa.
Idhaa ya Kiswahili 2005-02-07
|