Nchi nne za Misri, Jordan, Israel na Palestina zimeamua kufanya mkutano wa wakuu tarehe 8 huko Sharm el Sheikh nchini Misri, ambapo waziri mkuu wa Israel Ariel Sharon na mwenyekiti wa Mamlaka ya utawala wa Palestina Mahmmoud Abbas watakuwa na mazungumzo ya pande mbili kabla ya mkutano huo. Huu ni mkutano wa ngazi ya juu kabisa kati ya pande hizo mbili tangu Bw Yasser Arafat afariki dunia mwezi Novemba mwaka jana. Jumuiya ya kimataifa inatumai kuwa mkutano wa wakuu wa pande nne utakuwa na umuhimu mkubwa kwa mchakato wa amani ya mashariki ya kati.
Hivi sasa ajenda ya mkutano wa wakuu wa Sharm el Sheikh kimsingi imethibitishwa. Habari zinasema kuwa, mkutano huo huenda utapata matokeo kadhaa halisi, kama vile Palestina na Israel kutangaza rasmi kusimamisha vita, Israel kuwaachia huru baadhi ya wapalestina wanaofungwa, na jeshi la Israel kuondoka hatua kwa hatua kutoka miji mitano ya magharibi ya Mto Jordan. Lakini mtu wa karibu wa Bwana Sharon alidokeza kuwa, Israel haitajadili suala kuhusu utekelezaji wa mpango wa amani ya mashariki ya kati.
Kuwaachia huru wapalestina wanaofungwa kulikuwa kikwazo kikubwa kabisa kilichotishia mkutano wa wakuu kufanyika kutokana na mpango uliowekwa. Kabla ya hapo, Israel ilikubali kuwaachia huru wapalestina 900 waliofungwa, ilisema kuwa wapalestina 500 miongoni mwao wataachiliwa huru siku kadhaa mara baada ya kufanyika kwa mkutano wa wakuu, na wengine 400 wataachiliwa mfululizo kutokana na hali ya usalama ya sehemu hiyo. Israel ilipanga kuwaachia wafungwa waliohukumiwa vifungo chini ya miaka minne, lakini Palestina inashikilia kuitaka Israel iwaachie huru wafungwa waliohukumiwa vifungo vya maisha, na kuihimiza Israel kumwaachia kiongozi wa mkoa wa chama cha PLO Bw Marwan al Bargouti na viongozi wengine 6 wa mikoa wa kundi la Hamas. Hatimaye pande hizo mbili zilisuluhisha migongano mikubwa kati yao, na kukubaliana kuanzisha tume maalum ya kuthibitisha orodha ya wafungwa watakaoachiwa, suala hilo gumu litatatuliwa baadaye.
Lengo kubwa la mkutano wa wakuu wa Sharm el Sheikh ni kuzihimiza Palestina na Israel zifufue mawasiliano, ili hali ya Palestina na Israel irudi kwenye kiwango cha kabla ya kuanzishwa kwa mapambano ya kijeshi ya Palestina mwaka 2000. Mshauri wa kisiasa wa rais Mubarak wa Misri ambayo ni nchi mwenyeji wa mkutano wa wakuu Bwana Osama el Baz hivi karibuni alisema kuwa, mkutano huo wa wakuu utapima udhati wa Israel juu ya amani. Misri inaona kuwa, umuhimu wa mkutano huo ni kuwa mkutano huo utaweka msingi kwa ajili ya mchakato wa amani ya Palestina na Israel kuendelea kupata maendeleo siku zijazo. Kama matokeo ya mkutano huo yatatekelezwa, basi Palestina na Israel zitaongeza uaminifu, na zitatandika njia ya majadiliano kati ya pande hizo mbili kuhusu hadhi ya mwisho ya Palestina.
Wachambuzi wanaona kuwa, baada ya mkutano huo wa wakuu, mchakato wa amani ya Palestina na Israel bado utakabiliwa na changamoto, ambapo hali ya usalama bado itakuwa tishio kubwa kwa mchakato huo, makundi yenye msimamo mkali ya pande hizo mbili yote yataweza kuchukua hatua zinazoweza kuharibu mchakato wa amani; aidha serikali ya Sharon inakataa kutekeleza mpango wa amani, bali inashikilia kutekeleza mpango wake pekee; zaidi ya hayo msimamo wa Marekani kuhusu mchakato wa amani ya Palestina na Israel hauonekani wazi. Kama Marekani haiwezi kuchukua msimamo usiopendelea upande wowote, mchakato wa amani ya Palestina na Israel bado utakabiliwa na matatizo mengi.
Idhaa ya Kiswahili 2005-02-08
|