Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-02-08 19:48:13    
Barua za wasikilizaji

cri
    Msikilizaji wetu Xavier L. Telly Wambwa wa sanduku la barua 2287 Bungoma Kenya ametuletea barua akitutaka tupokee salamu za mwaka mpya wa 2005 kwa niaba ya wasikilizaji wote hodari wa Radio China kimataifa wa Bungoma Kenya. Anasema wao ni wazima na bila wasiwasi wowote wanasonga mbele hatua kwa hatua na Radio China kimataifa. Wanatumai kuwa nasi wahusika pamoja na wahariri tunachapa kazi kwa unyenyekevu.

    Anasema angependa kutuarifu kwamba hivi sasa umekwisha mwaka mmoja tangu kuanzishwa kwa "Tovuti yetu" ya idhaa ya kiswahili ya Radio China kimataifa mnamo tarehe 26 Desemba mwaka 2005. Anasema kwao hiyo ni furaha isyo kifani.

    Yeye akiwa kiongozi wa wasikilizaji wenzake wa Radio China kimataifa wa kutoka mkoani magharibi hapo Kenya, walishirikiana pamoja hivi karibuni katika mji wao wa Bungoma Kenya, katika kijiji cha Nalondo kwenye boma lake, waliweza kufanikisha sherehe yenye kufana sana tangu kufunguliwa kwa "Tovuti yetu" ya idhaa ya kiswahili ya Radio China kimataifa.

    Anasema kabla ya kutoa maoni, waliendesha baiskeli uwanjani kwa saa moja na kumalizia sherehe hiyo kwa kusikiliza kipindi cha Radio China kimataifa na hatimaye kububujika maoni motomoto kuhusu tovuti yetu ya idhaa ya kiswahili ya Radio China kimataifa.

    Baadhi ya maoni tofauti tofauti kutoka kwa wasikilizaji waliokuwa ni kama yafuatayo:

    Bwana Xavier L. Telly Wambwa alisema: "Tovuti yetu" ya idhaa ya kiswahili ya Radio China kimataifa inaangaza kama nuru gizani popote uendapo.

    Bwana John Wanjala Injini alisema: Mimi niliona mbali duniani kote baada ya kuifungua "Tovuti yetu".

    Bwana Gorge Simiyu Wandabwa alisema: "Tovuti yetu" ni kama mtoto wangu mpendwa mchanga niliyemzaa hivi karibuni.

    Bibi Dorothy Sitawa Telly Wambwa alisema: Lo! Lo!! Lo!!! Siwezi kulala bila kutazama "Tovuti yetu" ya Radio China kimataifa.

    Bwana Martin Nyongesa Nicasio alisema: "Tovuti yetu" ni mwalimu wa milele.

Bwana Edwin Wamalwa Wambeye alisema: Filamu gani? Ni nini? Aah, kumbe ni "Tovuti yetu" ya Radio China kimataifa. Loo!

    Bibi Naomi Nabwana Khisa alisema: Ukitamani kuona na kusoma, kusoma picha za kupendeza basi tembelea "Tovuti yetu" kwa anuani ya www.cri.cn.

    Bibi Betty Khaemba Zakaria alisema: Leo ni leo na safari nchini China kwa "tovuti yetu" ya Radio China kimataifa

Naye Magaret Naliaka Injini alisema: Sasa faida ni kwetu sisi wasikilizaji wote wa Radio China kimataifa na "Tovuti yetu".

    Bwana Sylaus Konje Anaseti alisema: Hebu kesho tuambatane pamoja na Bwana Xavier L. Telly Wambwa kwenda kuitembelea "Tovuti yetu ya Radio China kimataifa kule mjini Beijing kabla kupata kifungua kinywa.

    Haya ndiyo maoni ya baadhi ya wasikilizaji wetu na wamekubaliana kuitembelea "Tovuti yetu" kila mara na kusikiliza vipindi vya Radio China kimataifa kila siku saa 11 jioni kupitia Radio KBC. Nao ni wanachama 30 ambao wanasema kamwe hawatatikiswa bali wataendelea kusikiliza Radio China kimataifa.

    Hapa tunawashukuru sana wasikilizaji wetu hao wa Bungoma Kenya ambao walikuwa na mkutano wa kuadhimisha mwaka mmoja tangu kuanzishwa kwa tovuti ya idhaa ya kiswahili ya Radio China kimataifa. Maoni yao yametutia moyo sana, kweli tunawashukuru kwa dhati kwa upendo wao kwa tovuti yetu, ni matumaini yetu kuwa wasikilizaji wetu watatoa maoni na mapendekezo kwa kazi ya tovuti yetu, kwani sisi watangazaji na watayarishaji wa vipindi vya matangazo ya idhaa ya kiswahili hivi sasa tumeongezewa kazi ya kuifanya tovuti ya idhaa yetu iwe nzuri, kila siku tunachapa kazi sana bila kuweza kupata mapumziko ya kutosha, lakini tukifikiri kuwa wasikilizaji wetu wanatembelea tovuti yetu na kuipenda, tunaongeza juhudi bila kujali uchovu, tunataka wasikilizaji wetu watatusaidie kuifanya tovuti yetu iwe nzuri zaidi ili siku za usoni iwavutie wasomaji wengu zaidi.