Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-02-16 16:12:57    
Iraq na Afghanistan, "mfuko wa fedha uliotoboka" wa Marekani

cri

Rais Bush wa Marekani hivi karibuni amewasilisha nyongeza ya dola za Kimarekani bilioni 81.9 katika bajeti kwa ajili ya shughuli za jeshi lake nchini Iraq na Afghanistan mwaka huu. Wapinzani wa vita na wanachama wa Chama cha Democratic wanaona kuwa sera potovu za Bush zimesababisha malipo makubwa katika vita dhidi ya Iraq na Afghanistan, na nchi hizo mbili zimekuwa "mfuko wa fedha uliotoboka" wa Marekani.

Tokea "tukio la Septemba 11" litokee, Marekani "inatumia pesa kama maji" katika vita dhidi ya Iraq na Afghanistan. Fedha zilizotengwa kwa ajili ya shughuli za kijeshi na ugaidi zimezidi dola za Kimarekani bilioni 200 kwa jumla, na sasa ujenzi mpya wa Iraq na Afghanistan umekwishaigharimu Marekani dola bilioni 27. Katika majira ya siku za joto mwaka jana, ikulu ya Marekani iliomba bunge liongeze dola bilioni 25 kwa ajili ya shughuli za kijeshi na ujenzi mpya wa Iraq na Afghanistan katika mwaka 2005. Tarehe 14 rais Bush kwa mara nyingine tena aliliomba bunge liongeze dola za Kimarekani bilioni 81.9. Hadi sasa kwa jumla Marekani imetumia zaidi ya dola za Kimarekani bilioni 300 nchini Iraq na Afghanistan.

Nyongeza hiyo kubwa inapingwa kabisa na wabunge wa Chama cha Democratic na wapinzani wa sera za Bush. Baadhi wanaona kuwa kwa wastani Marekani inatumia dola za Kimarekani bilioni moja kwa wiki nchini Iraq, hata hivyo hadi wakati wa siku za uchaguzi mkuu nchini Iraq migogoro ya nguvu za kijeshi ilikuwa ikiongezeka badala ya kupungua, na mchakato wa ujenzi mpya wa Iraq unasuasua, fedha hizo za nyongeza hazitaisaidia kitu Marekani kujinasua kutoka kwenye matatizo ya Iraq. Mbunge wa Chama cha Democratic Bw. Robert Byrd alisema kuwa fedha hizo zitaweza tu kusaidia usalama wa jeshi la Marekani nchini Iraq, lakini hazitasaidia chochote kuleta usalama nchini Iraq. Wengine wana wasiwasi kuhusu nakisi ya bajeti inayoongezeka kwa mfululizo. Kwa makadirio, mwaka huu nakisi ya bajeti ya Marekani imevunja rekodi na kufikia dola za Kimarekani bilioni 427, na nyongeza hiyo iliyozidi dola bilioni 80 itaongeza pengo la bajeti.

Kitu kinachozingatiwa zaidi ni kuwa nyongeza hiyo haikuingizwa katika bajeti ya mwaka wa fedha 2006 iliyotolewa wiki iliyopita, bali ni nyongezo ya bajeti ya mwaka wa fedha 2005. Wachambuzi wanaona kuwa sababu ya Bush kutoingiza nyongeza hiyo katika bajeti, moja ni kwa ajili ya kuifanya akisi ya bajeti ya mwaka 2006 ionekane ndogo, pili ni kuzifanya gharama za kijeshi zisionekane kuwa ni "kiasi kikubwa cha kushtusha". Mfafanuzi wa mambo ya kijeshi wa Marekani Bw. Lexington alisema kuwa kiasi kikubwa cha nyongeza hiyo kitatumika katika kubadili silaha kuwa za aina mpya, kwa hiyo haihusishi usalama wa nchini Iraq. Kutokana na usemi huo nyongeza hiyo ni kisingizio tu cha kuongeza gharama za kijeshi.

Wachambuzi wanaona kuwa ingawa nyongeza hiyo inapingwa na baadhi ya watu lakini itapitishwa tu bila tatizo na bunge lililodhibitiwa na Chama cha Ripublican. Rais Bush tarehe 14 alitangaza kuwa kiasi kikubwa cha nyongeza hiyo kitatumika kusaidia jeshi la Marekani nchini Iraq ili lijizatiti kujilinda na kukamilisha majukumu yake. Na kiasi kingine kitatumika katika mapambano dhidi ya ugaidi na kujenga "Mashariki ya Kati iwe ya amani na demokrasia". Kwa hiyo bunge la Marekani halitapuuza nyongeza hiyo "inayohusu usalama na maslahi ya taifa". Isitoshe, wabunge walio wengi wa Chama cha Republican katika bunge wanatumai nyongeza hiyo itapitishwa. Mwenyekiti wa kamati ya fedha ya Baraza la Chini ambaye ni mwanachama wa Chama cha Republican, Bw. Jerry Lewis amesema kuwa anatazamia kuwasilisha nyongeza hiyo kwa rais na kutiwa saini ili kuanza kazi katika mwezi Aprili. Kwa hiyo mwanzoni mwa mwezi Machi kamati hiyo itapiga kura kuhusu nyongeza hiyo, na kisha kuiwasilisha kwenye Baraza la Chini ipigiwe kura.

Wachambuzi wanaona kuwa nyongeza hiyo iliyo zaidi ya dola za Kimarekani bilioni 80 inadhihirisha kuwa gharama kubwa zilizoongezeka katika ujenzi mpya wa Iraq na Afghanistan zimezidi kabisa makadirio ya Bush. Siku zote rais Bush atakumbwa na tatizo hilo lisiloepukika kama jeshi la Marekani halitaondoka kutoka Iraq na hali ya usalama wa Iraq inaendelea kuvurugika. Kama Bw. Nancy Pelosi, kiongozi wa chama kidogo katika Baraza la Chini, alivyouliza katika taarifa yake ya maandishi, kwamba nini lengo la Marekani nchini Iraq? Na ili kufikia lengo hilo tutatumia kiasi gani cha fedha?

Idhaa ya kiswahili 2005-02-16