Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-02-17 20:49:50    
Maisha ya Suzanne, M-Canada anayefundisha Kiingereza katika wilaya ndogo ya China

cri

    Bibi Suzanne Styles mwenye umri wa miaka 34 mwaka huu ameishi katika wilaya ya Pingtang, mkoani Guizhou kwa miaka minane. Yeye si kama tu anaweza kuongea vizuri kichina, bali pia anaweza kuongea kwa lahaja ya huko. Japokuwa wilaya ya Pingtang ni sehemu ndogo, tena iko pembezoni mwa mji, lakini inapendeza sana kutokana na kuzungukwa na milima na mito.

    Bibi Suzanne anafundisha Kiingereza katika shule ya sekondari ya kikabila ya Pingtang. Muda si mrefu uliopita, mwandishi wetu wa habari alipofika katika shule hiyo aliwakuta wanafunzi wake walivyosimulia jinsi wanavyompenda mwalimu wao Bibi Suzanne.

    "Suzanne ni mwalimu mzuri sana."

    "Tunamshukuru sana mwalimu Suzanne kwa kutusaidia kuendelea na masomo."

    "Tunapenda kumwambia matatizo yetu, hata kama tukiongea kwa lahaja yetu yeye anaweza kutuelewa."

    Bi. Suzanne mwenye nywele ndefu alipoulizwa imekuwaje ameweza kuishi wilayani humo kwa muda mrefu kiasi hicho, alisema:

    "Hakuna sababu maalum, nimeshazoea kuishi hapa, nawafahamu watu wengi wa hapa, najisikia kama niko nyumbani. Kila ninapokwenda naweza kukutana na wanafunzi wangu, na huwa nakaribishwa na wazazi wa wanafunzi kwa ukarimu. Kwa kweli ninaipenda wilaya ya Pingtang, nina kazi nyingi za kufanya hapa, hivyo siwezi kuondoka."

    Bibi Suzanne anaongea kichina kizuri kweli kweli. Alisema kuwa, alianza kuipenda China tokea utotoni, alitaka kujifunza utamaduni wa China, ndugu yake mmoja alifundisha Kiingereza katika chuo kikuu kimoja cha mkoa wa Guizhou, hivyo alimfuata kwenda huko kuanza kujifunza kichina mwaka 1996.

    Muda si mrefu baada ya kufika China, alikwenda katika shule ya sekondari ya makabila ya Pingtang kuonana na rafiki yake mmoja aliyekuwa anafundisha Kiingereza huko. Wakati huo huyo rafiki yake alikuwa akijiandaa kuondoka, hivyo shule hiyo ilikosa mwalimu wa Kiingereza. Kutokana na ushawishi wa rafiki yake na mwaliko wa shule, Bi. Suzanne aliacha masomo yake chuoni na kuwa mwalimu wa Kiingereza. Alifundisha Kiingereza huku akifundishwa kichina na walimu wa shule hiyo, baada ya mwaka mmoja, Bi. Suzanne aliweza kuongea na wachina kwa lugha ya kichina bila tatizo.

    Mkuu wa shule hiyo Bwana Liu Xiangyuan alisema kuwa, Bibi Suzanne aliwahamasisha sana wanafunzi hamu ya kujifunza Kiingereza kwa njia yake maalum na kiwango cha Kiingereza cha wanafunzi cha shule hiyo kimeinuka sana. zaidi ya hayo, ili kuwasaidia wanafunzi maskini, kuanzia mwaka 1998, Bibi Suzanne alianza kuwasiliana na jamaa na marafiki zake walioko huko Canada kuchangisha fedha nyingi za kuwasaidia wanafunzi maskini wa shule ya sekondari ya Pingtang ili waweze kumaliza masomo yao. Bwana Liu Xiangyuan alisema kuwa, Bibi Suzanne amepata upendo na heshima kutokana na upendo wake, hivi sasa yeye ni mtu anayefahamika sana katika wilaya ya Pingtang.

    "Mahali popote anapokwenda watu humwita mwalimu Su, na humwalika nyumbani kwa chakula. Watu wote wa wilaya hiyo wanamfahamu kama ni mtu mkarimu."

    Baada ya kufundisha Kiingereza kwa miaka minne katika shule ya sekondari ya Pingtang, Bi. Suzanne alifaulu mtihani wa shahada ya pili katika kituo cha utafiti wa utamaduni wa China na Marekani, kilichoko Nanjing, mji mkuu wa mkoa wa Jiangsu, mashariki mwa China. Baada ya miaka miwili, Bibi Suzanne alihitimu masomo yake na kurudi wilayani kuendelea na mafunzo.

    Sasa Bibi Suzanne amepanga nyumba yenye ghorofa mbili. Yeye mwenyewe anakaa ghorofa ya juu, ghorofa ya chini na ya kwanza amezifanya kuwa vyumba vya kufundishia na kuchezea kwa wanafunzi, hivyo wanafunzi wanapenda sana kwenda huko.

    Watu wote wa Pingtang wakikutana na Bi. Suzanne njiani humsalimia kwa tabasamu. Walipopita kwenye mkahawa unaoitwa "Jua jekundu", Bi Suzanne alimwambia mwandishi wa habari kuwa, yeye anapenda sana chakula cha mkahawa huo, hasa tambi zinazotengenezwa kwa unga wa mchele. Tajiri wa mkahawa huo alisema kuwa, Bi. Suzanne alipokula tambi, huweka pilipili nyingi kama wenyeji wa huko.

    Licha ya kujaribu kuzoea desturi za kienyeji, Bi Suzanne pia anajaribu kujizoeza maisha ya kila siku ya wakazi wa huko, hasa sherehe za aina mbalimbali za kienyeji. Akiwakuta marafiki zake wanaandaa harusi, mazishi na kadhalika yeye huwa hakosi kushirikiana nao, na kila mara hujaribu kujishirikisha katika pilikapilika, kama vile kusafisha mboga, na kuosha vyombo. Alisema kuwa, jambo linalomfurahisha zaidi ni kuwa watu wa Pingtang wameshamfanya kama mmoja wao, popote akienda, hujisikia kama yuko nyumbani. Hayo ndiyo maisha yake ya huko Pingtang.

Idhaa ya Kiswahili 2005-02-17