Mwendeshaji mkuu wa mashitaka wa Israel Bw. Menachem Mazuz jana alitangaza kuwa, kutokana na kutokuwa na ushahidi wa kutosha, waziri mkuu Ariel Sharon hatashitakiwa kwa kesi ya ufisadi iliyotokea miaka kadhaa iliyopita. Lakini Bw. Mazuz pia alisema kuwa, mtoto wa Bw. Ariel Sharon ambaye alihusika na kesi hiyo Bw. Omri Sharon atashitakiwa.
Shutuma dhidi ya Bw. Ariel Sharon na mtoto wake kuhusika na ufisadi kulifichuliwa mwezi Septemba mwaka 2001. Ripoti iliyotolewa na idara ya ukaguzi ya Israel ilisema kuwa, Bw. Sharon alipogombea nafasi ya mwenyekiti wa chama cha Likud mwaka 1999 na waziri mkuu wa Israel mwaka 2001, kampuni moja ambayo ina uhusiano na mtoto wake Bw. Omri Sharon iliwahi kukipatia chama hicho kumsaidia Bw. Sharon katika kampeni ya uchaguzi dola za kimarekani milioni 1. Baada ya ufisadi huo kufichuliwa, Bw. Ariel Sharon alisema kuwa hakujua jambo hilo hata kidogo, na kupenda kurejesha fedha hizo. Na baadaye alirejesha fedha hizo haramu. Lakini mwezi Januari mwaka 2003, vyombo vya habari vya Israel vilifichua kuwa, mfanyabishara mmoja wa Afrika ya Kusini aliwahi kumpatia Bw. Omar Sharon mkopo wa dola za kimarekani milioni 1.5 ili kulipa fedha hizoharamu. Baada ya hapo, idara za polisi na sheria zilifanya uchunguzi kuhusu kesi hiyo. Bw. Ariel Sharon alipoulizwa na polisi alisema kuwa, mambo yake yote ya fedha yanashughulikiwa na mtoto wake, na hakushiriki kwenye mambo hayo, lakini mtoto wake Omri Sharon hakusema kitu.
Kufichuliwa kwa kashifa ya ufisadi kulileta athari kubwa nchini Israel. Wakati huo Israel ilikuwa ikifanya uchaguzi mkuu, hivyo mustakabali wa kisiasa wa Bw. Ariel Sharon na uungaji mkono wa chama cha Likudi uliathiriwa vibaya. Mwendeshaji mkuu wa mashitaka wa Israel Bw. Mazuz kutangaza rasmi kutomshitaki Bw. Ariel Sharon kunamaanisha kuwa hatimaye Bw. Sharon ameondokana na usumbufu huo. Lakini mtoto wake huenda atashitakiwa kwa kudanganya na kutoa ushahidi usio wa kweli. Mashitaka hayo yakipitishwa, huenda atafungwa gerezani kwa miaka 7.
Baada ya Bw. Ariel Sharon kuwa waziri mkuu wa Israel tangu mwaka 2001, alishitakiwa mara kwa mara, na kuwa waziri mkuu wa tatu aliyefanyiwa uchunguzi na polisi nchini humo. Licha ya kesi hiyo ya ufisadi, pia alihusika na tukio la kisiwa cha Ugiriki. Tukio hilo lilitokea mwanzoni mwa mwaka 1999. Mfanyabiashara mmoja wa Israel aliyetaka kupata idhini ya kununua kisiwa kimoja nchini Ugiriki alishukiwa kumpatia Bw. Sharon ambaye wakati huo alikuwa waziri wa mambo ya nje rushwa isiyo ya moja kwa moja. Mwezi Machi mwaka jana idara ya uchunguzi ya Israel ilipendekeza kumshitaki Bw. Sharon kuhusu jambo hilo. Hii ilisababisha Bw. Sharon kukabiliwa na shinikizo kubwa la kujiuzuru, na utekelezaji wa mpango wake wa upande mmoja pia uliathiriwa. Lakini kumshitaki waziri mkuu si jambo dogo na halikuwahi kutokea katika historia ya Israel, hivyo idara ya sheria ilifikiria sana. Na mwezi Juni Bw. Mazuz alitangaza kutomshitaki Bw. Sharon kwa tukio la kisiwa cha Ugiriki kutokana na kutokuwa na ushahidi wa kutosha. Na jana uamuzi wa Bw. Mazuz ulimwondolea Bw. Sharon usumbufu tena. Bunge la Israel kupitisha juzi mswada wa sheria ya kuwapatia fidia wakazi wa Israel wanaoodoka kutoka ukanda wa Gaza katika mpango wa upande mmoja kumeuondolea mpango huo kizuizi kikubwa kabisa. Ingawa mambo hayo mawili hayana uhusiano wa moja kwa moja, lakini raia wa Israel wanaona kuwa, Bw. Sharon ambaye ameondokana na usumbufu wa mashtaka ataweza kufanya mambo mengi zaidi kwa kutimiza mpango wake wa kisiasa bila ya wasiwasi.
Idhaa ya Kiswahili 2005-02-18
|