Serikali ya Sudan na majeshi makubwa ya upinzani ya sehemu ya Darfur tarehe 17 yalikuwa na mazungumzo ya siku moja huko N'djamena, mji mkuu wa Chad, ambapo pande hizo mbili zimekubaliana kufufua mazungumzo ya amani kabla ya mwishoni mwa mwezi huu.
Mazungumzo ya jana yalifanyika kutokana na usuluhishi wa Umoja wa Afrika. Ofisa wa Chad aliyeshiriki usuluhishi wa pande hizo mbili alidokeza kuwa, wawakilishi wa serikali ya Sudan na majeshi makubwa mawili ya the Sudan Liberation Movement na the Justice and Equality Movement wameahidi wazi kutekeleza makubaliano ya usimamishaji vita yaliyofikiwa kati yao na kufufua mazungumzo ya amani.
Tangu kuibuka kwa mgogoro kwenye sehemu ya Darfur, magharibi ya Sudan mwezi Februari mwaka 2003, mgogoro huo umesababisha vifo na majeruhi ya watu wengi. Tokea nusu ya pili ya mwaka jana, chini ya usuluhishi wa Umoja wa Afrika, serikali ya Sudan na majeshi makubwa mawili ya upinzani ya Darfur vilifanya maduru matatu ya mazungumzo ya amani, lakini ni mafanikio kidogo tu yaliyopatikana. Ingawa kwenye duru la pili la mazungumzo, pande hizo mbili zilisaini makubaliano kuhusu usalama wa sehemu ya Darfur na misaada ya kibinadamu, lakini kutokana na taarifa ya Umoja wa Mataifa, makubaliano hayo hayajatekelezwa kwa ufanisi, na migogoro bado inatokea mara kwa mara.
Tarehe 16 mwezi huu, baraza la usalama la Umoja wa Mataifa lilifanya mkutano wa kusikiliza ripoti ya uchunguzi aliyotoa ofisa mwandamizi wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia mambo ya haki za binadamu Bwana Louise Arbour kuhusu suala la Darfur. Baada ya mkutano huo katibu mkuu Kofi Annan alisema kuwa, vitendo vya kushambulia vijiji, kuwaua raia wa kawaida na kuwalazimisha wakazi kuhama na vingine vya kukiuka sheria bado vinafanyika mara kwa mara huko Darfur. Chini ya uongozi wa Baraza la usalama, jumuiya ya kimataifa inapaswa kuchukua mara moja hatua mbalimbali za kuzuia vitendo hivyo na kuwalinda watu wanaokumbwa na tishio.
Lakini Umoja wa Afrika siku zote unatetea kuwa suala la Darfur linapaswa kutatuliwa barani Afrika, na kupinga shinikizo na kuingilia kati kutoka nje. Tarehe 16 viongozi wa nchi za Afrika kama vile Sudan, Chad, Gabon na Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo pamoja na mwenyekiti wa Kamati ya Umoja wa Afrika walikuwa na mazungumzo huko N'djamena kuhusu kufufua mchakato wa amani ya Darfur, baada ya mazungumzo walitoa taarifa wakiitaka jumuiya ya kimataifa iendelee kuunga mkono juhudi zinazofanywa na nchi za Afrika ili kusukuma mbele mchakato wa amani ya Darfur, kukwepa kuchukua hatua yoyote itakayoweza kusababisha kushindwa kwa juhudi hizo pamoja na kuweka vikwazo na kupeleka majeshi ya nje ya Umoja wa Afrika kwenye sehemu ya Darfur. Taarifa hiyo pia inatoa mwito wa kusimamisha vita kwa pande zote kwenye sehemu ya Darfur, na kuutaka Umoja wa Afrika uchukue hatua halisi ya kulinda amani huko Darfur kwenye msingi wa kuheshimu mamlaka ya nchi ya Sudan.
Wachambuzi wanaona kuwa, katika hali ya hivi sasa ingawa serikali ya Sudan na majeshi ya upinzani vimekubaliana kufufua mazungumzo ya amani mapema iwezekanavyo, lakini maendeleo ya mazungumzo hayo hayataweza kupatikana bila vizuizi. Kwani migongano iliyosababisha migogoro ya pande hizo mbili ilitokana na sababu nyingi za miaka mingi ambayo inahusiana na masuala nyeti ya dini na madhehebu, ambayo ni vigumu kutatuliwa kimsingi katika muda mfupi; aidha makubaliano yaliyofikiwa kati yao kwenye mazungumzo yaliyopita bado hayajatekelezwa kwa makini; zaidi ya hayo serikali ya Marekani inajaribu kuiwekea shinikizo serikali ya Sudan kwa kisingizio cha suala la Darfur, hii pia imeongeza hali zisizojulikana kwa mazungumzo hayo. Serikali ya Sudan inadhani kuwa Marekani inayaunga mkono majeshi ya upinzani, na majeshi ya upinzani yanataka kutegemea nguvu ya Marekani kujipatia maslahi mengi zaidi kwenye mazungumzo, hivyo ni vigumu kwa pande hizo mbili kujenga uaminifu unaotakiwa kwenye mazungumzo.
Idhaa ya kiswahili 2005-02-18
|