Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-02-18 20:55:39    
Barua 0213

cri

    Leo tarehe 13 Februari ni siku ya tarehe 5 Januari ya mwaka mpya 2005 kwa kalenda ya kichina. Siku hizi wananchi wa China wanasherehekea kwa furaha sikukuu ya Spring ambayo ni sikukuu ya jadi ya mwaka mpya wa kichina. Wafanyakazi wote wamepewa siku 7 za mapumziko, isipokuwa wafanyakazi wa shughuli maalum zisizoweza kusimamishwa hata kwa siku moja kama sisi watangazaji wa radio, ambao tunaweza kupumzika kwa zamu. Siku hizi tunachapa kazi kama kawaida, kwa kweli mwaka hadi mwaka, tunafanya vivyo hivyo, tumeshazoea kusherekea sikukuu katika hali kama hii. Kwa niaba ya wenzetu wote tunawatakia wasikilizaji wetu heri ya mwaka mpya wa kuku kwa kalenda ya China.

    Wiki iliyopita tuliwaletea wasikilizaji wetu maelezo kuhusu mwaka wa kuku, na katika siku za karibuni tulipata barua pepe kutoka kwa msikilizaji wetu ambaye anataka turudie maelezo hayo. Sasa kwanza tunarudia maelezo hayo kuhusu mwaka mpya wa kuku, halafu baadaye tutaendelea kuwasomea barua tulizopokea kutoka kwa wasikilizaji wetu.

    Msikilizaji wetu Juma Majaliwa wa Shirika la reli Tanzania sanduku la posta 20166 Dar es Salaam Tanzania hivi karibuni alituletea barua akiwa ameandika mashairi kadha wa kadhaa akitoa maoni yake kuhusu matangazo ya idhaa ya kiswahili ya Radio China kimataifa. Kwanza tunawaletea shairi lake la kwanza la kupongeza mwaka mpya wa 2005. Shairi hilo linasema: 2005 uwe Mwaka wa Baraka

1. Bismillah Rahmani, Rabi wetu Rahmani,

Tunakuomba Manani, muumba vyote duniani,

Baraka zake jueni, nasema tuziombeni,

Uwe mwaka wa baraka, elfu mbili na tano.

2. Hakika huu ni mwaka, uwe wa neema jamani,

Uwe mwaka wa baraka, pote hapa duniani,

Tumuombeni rabuka, mola wetu wa Manani,

Uwe mwaka wa baraka, elfu mbili na tano.

3. Dini zote tambueni, dua njema tuombeni,

Sehemu misikitini, na huko makanisani,

Viongozi na wa dini, mawaidha yatoeni,

Uwe mwaka wa baraka, elfu mbili na tano.

4. Masheikh nawaombeni, dua njema ziombeni,

Nanyi pia na ombeni, mapadiri tambueni,

Tupate mema jueni, na hapa petu nchini,

Uwe mwaka wa baraka, elfu mbili na tano.

5. Walisome na Mloka, hadi huko Visiwani,

Ziwepo zaka baraka, twakuomba na Manani,

Tuziombe kwa hakika, hilo ninawambieni,

Uwe mwaka wa baraka, elfu mbili na tano.

6. Beti sita kituoni, kuongeza sitamani,

Uwe wa heri jamani, mwaka huu sikieni,

Na mabaya eleweni, ayaepushe manani,

Uwe mwaka wa baraka, elfu mbili na tano.

Idhaa ya Kiswahili 2005-02-18