Rais Bush wa Marekani ameanza ziara yake barani Ulaya. Tarehe 21 huko Brussels, kwenye hotuba yake alitaka Marekani na nchi za Ulaya zianze tena "zama mpya" za uhusiano uliovuka bahari ya Atlantiki. Lakini kutokana na kuwa hitilafu muhimu kati ya Marekani na Ulaya hazikubadilika, wengi wa wachambuzi wanatia wasiwasi kwamba kweli uhusiano huo unaweza kuingia katika "zama mpya".
Rais Bush aliwasili mjini Brussels tarehe 20 jioni, siku ya pili saa nane mchana kwenye tafrija iliyofanyika katika ukumbi wa kifalme alitoa hotuba akieleza madhumuni ya ziara yake barani Ulaya.
Moja ya madhumuni ya ziara ya Bushi barani Ulaya ni kutia kiraka uhusiano uliochanika kati ya Marekani na Ulaya kutokana na vita dhidi ya Iraq. Kwa hiyo hakika uhusiano huo ulikuwa ni maudhui ya hotuba yake. Rais Bush alisema, Marekani inaunga mkono Ulaya iliyo na nguvu na Marekani inahitaji rafiki mwenye nguvu ili kusukuma mbele demokrasia duniani. Alisema, muungano kati ya Marekani na Ulaya ni nguzo ya kuhakikisha usalama katika zama mpya, na urafiki kati ya Marekani na Ulaya ni kitu muhimu kwa ajili ya amani na ustawi duniani, na kwamba mabishano na hitilafu yoyote ya muda haiwezi kutenganisha Marekani na Ulaya. Vyombo vya habari viligundua kwamba kwenye hotuba rais Bush alitumia neno "muungano" mara 12.
Kwenye hotuba rais Bush alikubali hitilafu kati ya Marekani na Ulaya katika suala la Iraq, lakini aliitaka Ulaya isahau tofauti hizo na kutoa misaada kwa ajili ya ujenzi mpya wa Iraq. Kadhalika, pia alisema kuwa nia ya Marekani na Ulaya ni kuleta amani ya Mashariki ya Kati, anaona kuwa hivi sasa Marekani na Ulaya zimekuwa na fursa nzuri ya kusukuma mbele mchakato wa amani ya Mashariki ya Kati, na zinaweza kutoa mchango kwa ajili ya amani hiyo.
Wachambuzi wanaona kuwa ingawa kwenye hotuba yake rais Bush alionesha tumaini lake la kurudisha uhusiano mzuri kati ya Marekani na Ulaya, lakini mawazo aliyoonesha kwenye hotuba yake ni yale yale ya zamani na kukosa hatua halisi za namna ya kuboresha uhusiano huo. Kuhusu hitilafu kati ya Marekani na Ulaya msimamo wa Marekani kimsingi haujabadilika.
Kwa mfano, kuhusu suala la Iran. Ingawa rais Bush alisema Marekani itaunga mkono juhudi za nchi za Uingereza, Ufaransa na Ujerumani, lakini hakuahidi kuondoa uwezekano wa Marekani kutumia nguvu za kijeshi, na pia hakusema kuwa Marekani itashiriki kwenye mazungumzo na Iran. Kama watu wote wajuavyo kwamba ni vigumu kupata mafanikio yoyote bila Marekani kushiriki katika mazungumzo na Iran. Hali kadhalika, kuhusu suala la "mkataba wa Kyoto", kwenye hotuba yake rais Bush alirudia ule ule msimamo wake wa kutatua suala la uchafuzi wa mazingira kwa kutegemea mageuzi ya teknolojia. Kuhusu suala hilo, mwanakamati wa Kamati ya Ulaya anayeshughulikia mambo ya uchafuzi wa mazingira Bw. Stavros Dimas aliwaambia waandishi wa habari kuwa mageuzi ya teknolojia ni haja ya lazima na Umoja wa Ulaya haujawahi kuacha juhudi zake, lakini tatizo la mabadiliko ya hali ya hewa duniani haliwezi kutatuliwa kwa kutegemea mageuzi ya teknolojia tu, bali pia linahitaji vitendo, na hasa vitendo vya kupunguza hewa chafu.
Baada ya shughuli za mchana tarehe 21, jioni rais Bush na rais Chiraq wa Ufaransa walikula chakula cha jioni pamoja. Kutokana na kuwa rais Shirak alikuwa katika mstari wa mbele kupinga Marekani kutumia nguvu za kijeshi dhidi ya Iraq, vyombo vya habari vinaona kuwa rais Bush alijaribu kukifanya chakula hicho kuwa kama ni dalili ya uhusiano mzuri uliorudishwa kati ya Marekani na Ufaransa. Lakini kabla ya chakula, rais Chiraq aliwaambia waandishi wa habari kuwa Marekani na Ufaransa zina uhusiano mzuri wenye historia ya zaidi ya miaka 200, lakini hii haina maana ya kuwa pande mbili zina maoni ya namna moja wakati wote katika matatizo yote.
Idhaa ya kiswahili 2005-02-22
|