Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-02-22 15:46:37    
Barua 0220

cri

Msikilizaji wetu Maluha Martin wa sanduku la posta 3021 Moshi Tanzania hivi karibuni ametuletea barua pepe akisema, ni matumaini yake kuwa sisi sote ni wazima wa afya na tunaendela vizuri na matangazo ya idhaa ya kiswahili ya Radio China kimataifa.

Tunamshukuru na tunamwambia kuwa sisi sote ni wazima, na tunaendelea kuchapa kazi hata katika wakati wa kusherehekea sikukuu ya jadi ya mwaka mpya wa China.

Bwana Martin anasema, anapenda kutushukuru kwa salamu zetu za mwaka mpya pamoja na kalenda ya mwaka 2005 tuliyomtumia. Anachotuomba tuendelee kudumisha urafiki wetu na kuwasiliana mara kwa mara, na yeye hata awe vipi licha ya masomo kumbana ataendelea kuwasiliana na sisi na kusoma vipindi vyetu kupitia tovuti yetu ya www.cri..cn. Anasema anatutakia mafanikio katika mwaka huu mpya wa 2005.

Bwana Mchana J. Mchana wa sanduku la posta 1878, Morogoro Tanzania ametuletea barua pepe akituandikia taarifa kuhusu bahasha ambazo gharama za stempu tayari zimekwishalipiwa, anasema bahasha hizo kule mkoani Morogoro zinakataliwa, wanadai hawana mkataba na Radio China, kwa hiyo barua zao nyingi hutupwa au hurudishwa. Anaomba tatizo hilo tuliangalie au tuwasiliane na posta za hapo nchini Tanzania, ili liweze kupatiwa ufumbuzi.

Kuhusu tatizo hilo idhaa yetu imetoa ripoti kwa idara husika ya Radio China kimataifa. Kwa sasa bado hatujui tatizo hilo litatatuliwa lini, tunaomba wasikilizaji wetu muwe na subira, kadiri siku zinavyokwenda tatizo hilo linaweza kutatuliwa vizuri. Katika baadhi ya sehemu ambako bahasha hizo zilikuwa zinakataliwa sasa tayari zinakubaliwa, baadhi ya sehemu za Tanzania kama vile Dar es salaam bahasha hizo zinakubaliwa, tunatumai kuwa katika siku zijazo itakuwa hivyo hata kwa Morogoro.

Msikilizaji wetu Tuju S. Ngassa ambaye hakuandika anuani yake ametuletea barua pepe anasema kuwa, salamu nyingi zitufikie kutoka Kahama Shinyanga Tanzania. Anatupa pole kutokana na shughuli nyingi za kuwapasha mambo mengi mazuri na mabaya yanayotokea duniani kote kila siku, anatushukuru sana kwa kazi yetu nzuri na ngumu ya kuwaandalia vipindi mbalimbali vya kuvutia katika idhaa ya kiswahili ya Radio China kimataifa, na anatutaka tuendelee na moyo huo.

Anasema miaka mingi imepita na hatimaye tumeingia mwaka 2005 tukiwa tuko pamoja na matangazo yakizidi kuwa mazuri, na hasa kwa sasa wasikilizaji wanapata matangazo kupitia mtandao wa internet. Anasema hakika matangazo yetu kupitia tovuti yetu yanapatikana vizuri na kwa urahisi zaidi, na anatoa pongezi kwa kazi hiyo nzuri. Anatuomba tuendelee kufanya mambo mengi mazuri ili kuboresha idhaa hii ya kiswahili ya Radio China kimataifa katika mwaka 2005.

Tunamshukuru kwa dhati msikilizaji wetu Tuju Ngassa kwa kututia moyo tufanye juhudi kubwa zaidi, ili kuvifanya vizuri zaidi vipindi vyetu na kuwaridhisha zaidi wasikilizaji wetu. Pia tunashukuru kwa maoni yake na tungependa kuwakumbusha wasikilizaji wetu wenye maoni wasisite kutuletea maoni na mapendekezo yanayoweza kutusaidia kuboresha vipindi vyetu.

Msikilizaji wetu Mbarouk Msabah wa sanduku la posta 52483 Dubai Falme za Kiarabu ametuletea barua pepe akiandika makala yake inayosema: "Tamko la Mzee Mandela ni ushujaa". Bwana Msabah ameandika makala hii akitaka isomwe kwa wasikilizaji kutokana na kuguswa na ujasiri wa aliyekuwa Rais wa Afrika ya kusini mzee Nelson Mandela kutangaza waziwazi kwa dunia nzima kuwa mtoto wake alifariki kutokana na ugonjwa wa Ukimwi.

Makala hiyo inasema, tamko alilolitoa bayana Mzee Nelson Mandela hivi karibuni kwamba mtoto wake pekee wa kiume aliyebakia Makgatho Mandela alifariki kutokana na ugonjwa hatari wa ukimwi, kwa kweli ni kitendo cha kishujaa na chenye kupaswa kuwa ni mfano mzuri kwa viongozi wengine wa kisiasa sio tu barani Afrika lakini pia kote duniani.

Anasema kwa kweli Mzee Nelson Mandela ni kiongozi mwenye kuheshimika na kupendwa mno kote ulimwenguni, kutokana na kujitolea kwake kuwakomboa waafrika wa Afrika kusini chini ya makucha ya utawala wa ubaguzi wa rangi uliokuwepo nchini humo. Pia Mzee Mandela amekuwa mstari wa mbele katika harakati mbalimbali za kisiasa za kimataifa na kusaidia katika kampeni nyingi za kijamii ikiwemo ile kampeni kubwa ya kupambana na ugonjwa hatari wa ukimwi.

Bila shaka yoyote mfano huo aliouoneshwa na Mzee Mandela kwa walimwengu kwa kutangaza wazi wazi bila kificho juu ya sababu za kifo cha mtoto wake, huenda ukatoa changamoto kubwa kwa viongozi wengine duniani kuwa wakweli katika swala zima la kupambana na ugonjwa huo hatari unaozidi kuteketeza maisha ya watu.

Bwana Mbarouk ameandika vizuri makala yake ya kumsifu Mzee Nelson Mandela, ambaye sisi sote tunamheshimu sana kutokana na juhudi zake za kujitolea katika ukombozi wa waafrika na harakati mbalimbali za jamii, Mzee Mandela anastahiki kusifiwa na watu wote duniani.

Msikilizaji wetu Nzumbi Madalo Kitebo ambaye hakuandika anuani yake tarehe 14 mwezi huu alitutumia barua pepe akisema kuwa, Salamu nyingi zitufikie huko tuliko. Anatushukuru na kutupongeza kwa juhudi zetu za kuwaletea habari muruwa za kimataifa. Anatushukuru kwa kumtumia kalenda ndogo ya mfukoni ya mwaka 2005 pamoja na barua ya kumtakia kila la kheri kwa mwaka mpya japokuwa ilichelewa kidogo.

Anasema yeye ni mmoja wa wasikilizaji wakongwe kabisa wa tangu kipindi kile Radio China Kimataifa ikijulikana kwa jina la Radio 'Beijing'. Na yeye kwa kipindi kile alikuwa akitumia jina la Kitebo Kulwa.

Kwa sasa anatumia jina la Nzumbi Madalo Kitebo au Joseph N. Madalo Anafuatilia taarifa zetu za kila siku kuhusu: Mabadiliko ya uchumi nchini China, kilimo, sayansi na teknolojia ya watu wa China, Mazingira pamoja ushiriki wa China katika mambo ya siasa ya kimataifa. Anasema anatarajia kusikia mengi kutoka kwetu kupitia tovuti yetu.

Tunamshukuru kwa dhati msikilizaji wetu huyo tangu zamani sana, ambaye mbali na kufuatilia matangazo yetu ya Radio pia anatufuatilia sana kwa vipindi vyetu kupitia tovuti yetu kwenye mtandao wa internet. Kila tunapopata barua pepe kama hiyo tunafurahi sana, kwani tunatambua wasikilizaji wetu pia ni wasomaji wa tovuti yetu. Mwaka huu tutafanya juhudi kubwa zaidi kujipatia wasomaji wengi zaidi wa tovuti yetu.

Idhaa ya kiswahili 2005-02-22