Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-02-22 16:25:54    
Makampuni ya kimataifa yapenda kuanzisha taasisi za utafiti nchini China

cri

Takwimu zilizotolewa hivi karibuni zinaonesha kuwa hadi hivi sasa zaidi ya taasisi 700 za utafiti zimeanzishwa na makampuni ya kimataifa nchini China. Taasisi hizo zinahusu sekta za elektroniki, dawa na kemikali. Wataalam wanasema kuwa baada ya kuanzisha viwanda na mfumo wa mauzo hapa nchini, makampuni mengi ya kimataifa yanachukulia kuanzisha taasisi za utafiti kuwa sehemu moja muhimu ya mkakati wa kuendeleza viwanda vyao na kuongeza mitaji yao katika upande huo.

Makampuni ya kimataifa yamekuwa yakianzisha taasisi za utafiti nchini toka miaka ya 90 ya karne iliyopita, na yamekuwa yakiendelea kuharakisha hatua zake. Katika mwaka 2004 peke yake, makampuni ya kimataifa karibu 300 yalianzisha taasisi za utafiti nchini China.

Kampuni ya Novonordisk yenye makao yake makuu Copenhagen nchini Denmark, ni kampuni ya kwanza kwa ukubwa duniani inayozalisha dawa za ugonjwa wa kisukari. Mwaka jana, kampuni hiyo, ambayo pato lake kutokana na mauzo linazidi dola za kimarekani bilioni 4, ilijenga taasisi ya utafiti hapa Beijing, China. Msimamizi wa taasisi ya utafiti ya kampuni hiyo iliyojengwa hapa Beijing Bw. Wang Baoping alimwambia mwandishi wetu wa habari kuwa katika miaka ya 60 ya karne iliyopita, dawa zilizozalishwa na kampuni ya Novonordisk zilianza kuingia kwenye soko la China, na kampuni hiyo iliamua kujenga kiwanda cha dawa nchini China miaka 11 iliyopita. Anaona kuwa kuweka taasisi ya utafiti nchini China kunaonesha kuwa kampuni ya Novonordisk inathamini sana soko la China. Alisema,

"China ni moja ya soko muhimu sana la kampuni ya Novonordisk duniani. Kampuni ya Novonordisk inazingatia sana jitihada za China katika kutibu wagonjwa wa kisukari, hivi sasa idadi ya wagonjwa wa kisukari nchini inaongezeka kwa kiwango kikubwa. Kujengwa kwa taasisi ya utafiti ni ahadi iliyotoa kampuni ya Novonordisk kuwekeza kwa muda mrefu nchini China.

Takwimu zinaonesha kuwa hivi sasa idadi ya wagonjwa wa kisukari hapa nchini imefikia kiasi cha milioni 30 na gharama ya tiba ya wagonjwa hao imezidi Yuan za Renminbi bilioni 20. Dk. Wang Baoping alisema kuwa soko kubwa la namna hiyo nchini China ni kivutio kikubwa sana kwa Kampuni ya Novonordisk.

Mbali na soko hilo kubwa, ikilinganishwa na nchi za viwanda, gharama za kujenga na kuendesha kituo cha utafiti nchini China ni ndogo, lakini kiwango cha utafiti siyo cha kiwango cha chini kikilinganishwa na cha nchi zilizoendelea. Hali hiyo ndiyo sababu inayovutia makampuni mengi ya kimataifa kujenga vituo vyao vya utafiti wa sayansi hapa nchini. Dr. Wang alisema kuwa endapo Kampuni ya Novonordisk itajenga katika nchi nyingine kituo cha utafiti kinacholingana na kile ilichojenga nchini China, gharama ya ujenzi peke yake itakuwa kubwa mara kadhaa kuliko ile iliyotumiwa katika ujenzi wa kituo chake nchini China. Licha ya hayo, gharama zinazotumika katika tiba za majaribio nchini China, pia ni ndogo ambayo ni pungufu ya kiasi cha 30% ikilinganishwa na ile inayohitajika katika nchi za Ulaya na Marekani. Pamoja na maendeleo ya elimu, wataalam wanaohitajika katika kituo cha utafiti pia ni wengi nchini China.

Mbali na mahitaji makubwa ya soko la China pamoja na rasilimali nyingi za utafiti wa sayansi, sera nafuu zilizobuniwa na serikali ya China pia zinaimarisha imani ya makampuni makubwa ya kimataifa kujenga vituo vya utafiti nchini China. Profesa Sang Baichuan wa chuo kikuu cha uchumi na biashara na nchi za nje cha China alisema,

"Sera husika zilizobuniwa na serikali ya China ni kuhamasisha makampuni makubwa ya kimataifa kujenga vituo vya utafiti hapa nchini, serikali ya China imejitahidi kuyarahisishia makampuni ya kimataifa kujenga vituo vya utafiti nchini China, kwa mfano, kuna sera nafuu katika matumizi ya ardhi na ni rahisi kuwapata wataalam wanaohitajiwa na makampuni hayo ya kimataifa nchini China. Licha ya hayo, zana zote zinazohitajiwa na vituo hivyo vya utafiti, ambazo zinatakiwa kuagizwa kutoka nchi za nje, zote zinasamehewa ushuru wa forodha, tena kodi za mapato zinapunguzwa kuliko kiwango cha kawaida."

Mazingira bora ya utafiti na uvumbuzi nchini China yanavutia makampuni ya kimataifa kuongeza uwekezaji hapa nchini. Mwaka 1998, kampuni ya Microsoft ilitenga dola za kimarekani milioni 80 kujenga taasisi ya utafiti nchini China, ilipofika mwaka 2004 vituo vya utafiti vilivyojengwa na kampuni za kigeni hapa China vilikuwa vitano, na uwekezaji ulifikia dola za kimarekani bilioni 2. Kampuni maarufu ya teknolojia ya mawasiliano ya Motorola hivi sasa imekwisha jenga vituo 18 vya utafiti nchini China, na uwekezaji wake umefikia dola za kimarekani milioni 150.

Kujenga vituo vya utafiti nchini China kwa mataifa makubwa ya kimataifa pia kunaathiri sekta husika za China. Wataalam wamesema kuwa ikilinganishwa na vituo vya utafiti vya China, makampuni ya kimataifa yana ubora katika vitendea kazi, mitaji na uwezo wa kutumia raslimali mbalimbali. Aidha, vituo vya utafiti vya makampuni ya kimataifa vimeanzisha mazingira ya kufungua mlango wazi na yanahamasisha ushirikiano na maingiliano kati ya watafiti wa China na nchi za nje. Kuhusu suala hilo mkurugenzi mkuu wa kampuni ya PSA Peugeot Citroen Bw. Jean-Martin Folz alisema,

"Hivi sasa, kampuni ya PSA Peugeot Citroen imekuwa na watafiti wengi. Katika mji wa Wuhan tuna watafiti zaidi ya 500, ambao wengi wao walipewa mafunzo kwa miezi au wiki kadhaa nchini Ufaransa ili kukuza uwezo wao wa uvumbuzi wa teknolojia, sisi hatukufikiria kuwazuia wahandisi wa kampuni hiyo nchini China wasipate baadhi ya teknolojia zetu."

Maendeleo ya kasi ya makampuni ya kimataifa nchini China yametia changamoto kwa kampuni na viwanda vya China, ambavyo vingi vinajifunza uzoefu wenye ufanisi wa makampuni ya kimataifa katika usimamizi wa rasilimali za nguvu kazi na uendeshaji wa kampuni, na kuendeleza utafiti wa teknolojia kwa kutegemea ubora wake.

Wataalam wamesema kuwa maendeleo ya kampuni ya kimataifa nchini China yatafanya makampuni hayo kujenga vituo vya utafiti vingi zaidi nchini China, ambapo viwanda vya China pia vitajiimarisha katika ushindani na kupata maendeleo makubwa.

Idhaa ya kiswahili 2005-02-22