Shirikisho la mshikamano wa Iraq, ambalo viongozi wake wengi ni Waislamu wa madhehebu ya Shia lililoshinda katika uchaguzi mkuu wa Iraq, tarehe 22 lilimteua kiongozi wa chama cha Dawa cha kiislam cha shirikisho hilo Bw. Ibrahim al-Jaafari kuwa mgombea wa waziri mkuu wa serikali ya mpito.
Bw. Ibrahim al-Jaafari alizaliwa mwaka 1947katika familia yenye heshima ya madhehebu ya Shia; mwaka 1966 alijiunga na chama cha Dawa cha kiislamu chenye historia ndefu kabisa nchini Iraq, baadaye alikuwa katibu mkuu na msemaji wa chama hicho. Mwaka 1980, serikali ya Saddam ilitangaza kukipigia marufuku chama hicho, hivyo watu wa familia yake walikimbilia nchini Iran, na mwaka 1989 walihamia mjini London, hivu sasa ana watoto watano, wavulana wawili na mabinti watatu, ambao wote wanaishi mjini London. Mwezi Aprili, mwaka 2003, Bw. Jaafari alikuwa mmoja wa kikundi cha kwanza cha viongozi wa kisiasa waliorudi nchini Iraq. Baada ya kurudi nchini Iraq, Bw. Jaafari alikiongoza chama cha Dawa kushiriki kwenye ukarabati wa kisiasa wa Iraq, na alikuwa mwenyekiti wa kwanza wa kamati ya usimamizi ya muda ya Iraq, sasa ni makamu wa rais wa serikali ya muda ya Iraq. Bw. Jaafari anachukuliwa kuwa "kiongozi mwenye msimamo wa katikati", hivyo anaungwa mkono na waumini wa dini, pia anapata uungaji mkono mkubwa na watu wa kawaida. Sasa yeye ni mtu wa pili katika shirikisho la mshikamano wa Iraq.
Wachambuzi wanasema kuwa, Bw. Jaafari akitaka kuchaguliwa kuwa waziri mkuu, bado anakumbwa na vikwazo.
Kwanza, Marekani inatilia shaka historia ya Bw. Jaafari. Ingawa Bw. Jaafari anachukuliwa kuwa kiongozi mwenye msimamo wa katikati, lakini wanachama wengi wa chama cha Dawa ni Waislam wa madhehebu ya Shia na walioishi nchini Iran. Kamati kuu ya mapinduzi ya kiislam ya Iraq, ambacho ni chama kikubwa kabisa cha umoja wa mshikamano wa Iraq kinachomuunga mkono Bw. Jaafari kina uhusiano mzuri na Iran. Katika siku za karibuni, Bi. Hilary Clinton aliyefuatana na ujumbe wa baraza la juu la bunge la Marekani kufanya ziara nchini Iraq, huko Baghdad alisema kisirisiri kuwa, historia ya Bw. Jaafari kuwahi kukaa Iran inaifanya Marekani iwe na wasiwasi kuwa kushika madaraka kwa Bw. Jaafari kunamaanisha kwamba Iran itaudhibiti utawala mpya wa Iraq.
Pili, Bw. Jaafari anakabiliana na changamoto ya waziri mkuu wa serikali ya muda Bw. Iyad Allawi. Tarehe 21, kundi lingine kubwa la kisiasa la madhehebu ya Shia, Jumuiya ya maafikiano ya kitaifa ya Iraq ilimteua rasmi Bw. Allawi kuwa mgombea wa waziri mkuu wa jumuiya hiyo. Ingawa kundi la Bw. Allawi lina viti 40 tu katika bunge la mpito, lakini Bw. Allawi pia ana nguvu yake: kwanza, kwa muda mrefu ameshirikiana na serikali ya Marekani, hivyo anaaminiwa na Marekani; pili, anachukuliwa kuwa ni mwislamu wa madhehebu ya Shia ya jadi, na kusaidiwa na Saudi Arabia na Kuwait, hivyo ni rahisi kupokewa na nchi jirani za kiarabu; tatu, maoni yake ya kisiasa yanafanana na ya shirikisho la Kurdistan, yaani kutetea kuanzisha utawala wa jadi na kutunga katiba ya jadi. Aidha, Bw. Allawi pia anapata uungaji mkono wa baadhi ya vikundi vya kidemokrasia.
Tatu, shirikisho la Kurdistan na kundi la Waislamu wa madhehebu ya Suni vina matakwa kwa madaraka na maslahi ya siku za usoni, hivyo shirikisho la mshikamano ni lazima litoe jibu. Shirikisho la mshikamano pia linatakiwa kutatua suala la kuwapatia Waislamu wa madhehebu ya Suni hadhi mwafaka ingawa viti vyao ni vichache tu.
Kwa hivyo, wachambuzi wanasema kuwa, kama Bw. Jaafari ataweza kuongoza serikali ya kwanza ya Iraq iliyochaguliwa kidemokrasia baada ya miaka 50 au la, bado inahitaji kusubiri matokeo ya mashauriano kati ya shirikisho la mshikamano na Marekani pamoja na vyama mbalimbali vya kisiasa vya Iraq.
Idhaa ya Kiswahili 2005-02-23
|