Tarehe 23 Shirika la Afya, Shirika la Chakula na Shirika la Afya ya Wanyama duniani yatafanya mkutano wa pili wa siku tatu mjini Ho Chi Minh, Vietnam, kujadili hatua za kukinga na kudhibiti ugonjwa wa mafua ya ndege barani Asia. Mkutano huo licha ya kupima hali ilivyokuwa katika juhudi za kudhibiti na kukinga maambukizi ya ugonjwa wa mafua ya ndege tokea mkutano wa kwanza ulipofanyika mwezi Februari mwaka jana, pia utajadili hatua gani mpya zitakazochukuliwa katika mapambano dhidi ya ugonjwa huo uliorudi tena siku za karibuni.
Tokea mwezi Desemba mwaka jana ugonjwa wa mafua ya ndege ulipotokea ulikuwa ukiathiri vibaya nchi za Asia ya Kusini Mashariki za Vietnam na Thailand na sasa ugonjwa huo umerudia tena, kwamba katika muda wa miezi miwili tu umewaua watu 13. Hali hiyo imeitahadharisha jumuiya ya kimataifa, na ililitia wasiwasi sana Shirika la Afya la Dunia ambalo linahimiza nchi hizo kuzidisha juhudi za kukinga na kudhibiti, na kutaka jumuyia ya kimataifa isisimame kando bila kukabiliana na ugonjwa huo kwa ushirikiano.
Virusi vya ugonjwa wa mafua ya ndege vinavyoambukiza sasa vinaitwa H5N1 ambavyo hapo mwanzo viligunduliwa mwaka 1997 huko Hong Kong. Mwanzoni mwa mwaka 2004 ugonjwa huo ulilipuka barani Asia na kuenea haraka katika nchi nyingi, kuku wengi walichinjwa. Tofauti na ugonjwa huo wa zamani, ugonjwa wa sasa ambao watu wanauita "tauni ya kuku" unawaambukiza wanadamu kupitia ndege. Wagonjwa walioambukizwa ugonjwa huo wamepatikana katika nchi za Vietnam na Thailand. Kutokana na kumbukumbu za serikali, watu 45 wamepoteza maisha yao ambao ni asilimia 72 ya watu walioambukizwa virusi vya H5N1. Isitoshe, ugonjwa huo umeleta hasara kubwa katika sekta ya mifugo, biashara na utalii.
Katika siku za karibuni, ufahamu kuhusu ugonjwa wa mafua ya ndege umekuwa wa kina zaidi. Ripoti iliyotolewa na taasisi ya tiba ya Uingereza tarehe 17 Februari ilitangaza kuwa watu walioambukizwa virusi vya H5N1 wanadhurika karibu kwenye viongo vyote vikiwa ni pamoja na mfumo wa kupumua, moyo, maini na figo.
Kituo kikuu cha kinga na udhibiti wa magonjwa ya kuambukiza nchini Marekani tarehe 21 kilionya kuwa virusi vya H5N1 ni virusi vya hatari sana duniani. Kutokana na kuwa mabadiliko ya virusi hivyo ni ya haraka, na binadamu hana uwezo wa kujikinga navyo, vikiwa virusi vitaweza kuwaambukiza wanadamu moja kwa moja baada ya mabadiliko, tishio kwa binadamu litakuwa kubwa. Na kasi ya maambukizi itakuwa kubwa kuliko nimonia isiyo ya kawaida iliyolipuka mwaka 2003, bila shaka itawaua kiasi cha milioni katika miezi kadhaa. Binadamu hawajasahau maafa yaliyosababishwa na mafua katika historia ya binadamu, kwamba mwaka 1918 mafua barani Ulaya yaliwaua watu milioni kumi kadhaa, mafua hayo yalisababishwa na virusi viitwavyo H1, na virusi vya sasa H5N1 vikilinganishwa na vile H 1 ni vikali zaidi.
Hata hivyo, matayarisho ya kupambana na tishio hilo bado hayatiliwa maanani duniani. Wataalamu wanasema kuwa idara za afya za nchi mbalimbali zote zimekusanya nguvu kwenye mapambano dhidi ya mafua ya kawaida. Lakini kama ugonjwa huo wa sasa ukilipuka miongoni mwa wanadamu, idara hizo zitakuwa muhali kugeuza muudo wa kupambana na mafua ya kawaida kwenye mapambano dhidi ya ugonjwa huo wa mafua ya ndege. Hii ndio sababu kwa nini Shirika la Afya Duniani limeshikwa na wasiwasi mkubwa. Watu wanatumai mkutano huo utakuwa na mapendekezo mapya katika kazi za kukinga na kudhibiti ugonjwa huo.
Idhaa ya kiswahili 2005-02-23
|