Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-02-24 15:48:37    
Wachina wa leo watafuta mapenzi ya dhati

cri

Katika miaka ya hivi karibuni, kutokana na kuinuka kwa kiwango cha maisha ya wachina, matarajio ya wachina juu ya mapenzi na ndoa yameonesha matumaini ya aina mbalimbali. Katika mazingira ya kijamii yanayokuwa na mtizamo ulio wazi siku hadi siku, raia wengi zaidi wa kawaida wanataka kutafuta wachumba na ndoa kwa wanavyopenda.

Kijana Guan Wanqiang kutoka sehemu ya kaskazini mashariki mwa China anafanya kazi katika kampuni ya chuma na chuma cha pua hapa Beijing, japokuwa ana kazi nyingi, lakini kila siku anaishi kwa furaha kutokana na kuwa na familia yenye furaha. Bwana Guan alikuja Beijing kutoka sehemu nyingine nchini kutafuta kazi kwa ajili ya mchumba wake bila kujali upinzani wa wazazi wake. Alisema:

"Wakati ule, jambo muhimu zaidi katika maisha yangu lilikuwa kumpata mchumba na kuishi pamoja naye. Sasa tunaishi vizuri sana, yeye ni mwalimu, mapato yetu yanatutosheleza. Sasa tumepata uungaji mkono wa wazazi wangu, na katika likizo ya majira ya joto ya kila mwaka sisi hurudi nyumbani kwa wazazi."

Alipokuwa mwanafunzi katika chuo kikuu kimoja cha Beijing, Bwana Guan Wanqiang alimpenda msichana wa Beijing Li Yinfeng. Kwa kuwa Li Yinfeng ni binti wa pekee nyumbani kwake, hivyo baada ya kuhitimu, alichagua kubaki mjini Beijing. Hivi sasa bwana Guan na mke wake wote wamekuwa na kazi nzuri, walifunga ndoa na kununua nyumba na wanaishi kwa raha.

Kama ilivyo kwa bwana Guan Wanqiang, hivi sasa wachina wengi zaidi na zaidi wanapenda kuishi maisha ya kufuatana na mapenzi yao. Wanaondokana na kipingamizi cha jadi, kutafuta mapenzi halisi na kuishi maisha mazuri.

Bibi Chen Xinxin kutoka taasisi ya utafiti wa suala la wanawake ya China ni mtaalam maarufu wa ndoa na familia nchini China. Alisema kuwa, katika miaka ya hivi karibuni, mawazo yaliyopitwa na wakati yamekuwa yakitoweka siku hadi siku, mtizamo wa wachina kuhusu mapenzi na ndoa unaelekea kuwa wa wazi zaidi na kuonesha nia yao wenyewe.

"Kutokana na kuinuka kwa hali ya maisha na kuongezeka kwa pato la wananchi, matakwa ya wachina kuhusu sifa ya ndoa pia yameongezeka, kwa mfano kama maisha ya kifamilia na kijinsia ni ya kusikilizana au la, kila mtu anatumai kuweka hali nzuri ya kifamilia ili kuishi maisha mazuri ya starehe."

Bibi Chen alisema kuwa, katika utafiti wake ameona mabadiliko dhahiri, kwamba wakati ndoa inapokumbwa na tatizo au watu wawili wakikosa furaha kuishi pamoja, zamani watu wengi walikuwa wanachagua njia ya kuvumilia, lakini hivi sasa watu wengi wanadhubutu kuachana.

Hivi sasa tovuti nyingi za mtandao wa internet zimeanzisha baraza la kubadilishana maoni kati ya watu waliotalikiana, watu wengi wanaeleza visa vyao kwenye tovuti. Bwana Zhang Bin mwenye umri wa miaka zaidi ya 40 ni mmoja kati ya watu hao. Alimwambia mwandishi wa habari sababu yake yeye kutengana na mke wake:

"Baada ya kuishi pamoja kwa muda mrefu tuliona kuwa tuna tofauti nyingi, hatukuwa na furaha tena ya kuendelea kuishi pamoja, hivyo tuliamua kutengana kwa utulivu."

Sasa Bwana Zhang Bin anaishi katika nyumba ya kukodisha, anaishi maisha huru na utulivu. Mwisho wa wiki anakutana na marafiki zake au kupiga soga kwenye mtandao. Anasema kama ataweza kukutana na mwanamke mwingine atakayempenda ataanzisha maisha mapya ya ndoa.

Kwa mujibu wa takwimu, hivi sasa idadi ya wachina wanaotalikiana inaelekea kuongezeka mwaka hadi mwaka. Ofisa husika wa wizara ya mambo ya raia Bibi Wang Hongli alisema:

"Katika miaka ya hivi karibuni, idadi ya wachina wanaotalikiana inaongezeka. Mwaka 1990, waume na wake laki nane walitalikiana, lakini ilipofika mwaka 2003, idadi hiyo ilifikia milioni 1.33, na sababu ya kuachana kwa wengi ilitokana na kutokuwa na mapenzi tena ya kuendelea kuishi pamoja."

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa hivi karibuni, umri wa miaka wa watu wanaotalikiana unaelekea kupungua, na idadi ya watu wanaojiandikisha kufunga ndoa inapungua, watu wengi wanachagua kuishi pamoja bila ndoa, hali hiyo ya kuishi pamoja bila ndoa inaelekea kukubalika nchini China.

Bibi Chen Xinxin alisema kuwa, mambo hayo yote yameonesha kuwa, mtizamo wa wachina kuhusu mapenzi na ndoa umekuwa wa makini zaidi na wa kujiamulia zaidi. Vijana wengi wanaona kuwa, hawawezi kuingia katika ndoa au kuvunja ndoa ovyo ovyo, hivyo wanachagua njia ya kumchunguza mwingine wakati wa kuishi pamoja kwa muda, kama wakiweza kusikilizana vizuri, wataamua kufunga ndoa.

Bibi Chen Xinxin alisema kuwa, baada ya kufanya utafiti kwa miaka mingi, yeye ameona kuwa bila kujali mabadiliko ya idadi ya watu wanaofunga ndoa na idadi ya watu wanaotalikiana, ndoa siku zote ni jambo lenye makini sana katika maisha ya wachina. Kuongezeka kwa ndoa huria kumewapa wachina nafasi nyingi zaidi katika kutafuta furaha ya ndoa.

Idhaa ya kiswahili 2005-02-24