Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-02-24 16:22:25    
Mji wa Dalian wafanya upimaji wa mwili kwa wanawake wa makamo wenye matatizo ya kiuchumi

cri

Hivi karibuni, sehemu ya Shahekou ya mji wa Dalian, mashariki mwa China ulifanya upimaji wa magonjwa ya wanawake bila malipo kwa wanawake wa makamo wenye matatizo ya kiuchumi, jambo hilo linasifiwa sana na watu wanaohusika.

Bibi Xiong Shuming mwenye umri wa miaka 45 mwaka huu alisema kuwa?kutokana na matatizo ya kiuchumi alikuwa hana uwezo wa kwenda hospitalini kuonana na daktari hata kama akipata mafua, sembuse kufanyiwa upimaji wa mwili. Kama isingekuwa serikali ya sehemu ya huko kuandaa upimaji huo, yeye mwenyewe asingeweza kufanya upimaji wa mwili daima. Bibi Xiong aliyasema hayo akitokwa na machozi ya furaha.

Asubuhi mapema ya tarehe 22 Februari mwaka huu, Bibi Xiong Shuming na wanawake wengine zaidi ya kumi wenye matatizo ya kiuchumi kutoka mtaa wa Jingyun wa sehemu ya Shahekou walikwenda hospitalini kufanywa upimaji wa mwili. Madaktari walifanya upimaji wa kila aina kwa makini. Bibi Xiong Shuming alisema kuwa:

"Hii ni fursa nzuri sana kwangu, kuanzia mwaka 1999 nilipopunguzwa kazi hadi leo, sijawahi kufanya upimaji wa mwili hata mara moja. Wakati wa kawaida, hata kama nikiugua huwa navumilia, nilikuwa sina uwezo wa kwenda hospitalini, sikuweza kupimwa mwili."

Bibi Xiong Shuming ambaye mtoto wake anasoma katika sekondari ya juu na mume wake ni mgonjwa, kila mwezi maisha ya familia hiyo yanategemea mshahara wake wa kufanya kazi ya kibarua, ambaye ni mmoja wa wanawake elfu moja wa makamo wenye matatizo ya kiuchumi wa sehemu ya Shahekou ya mji wa Dalian. Tokea mwaka jana, shirikisho la wanawake la sehemu hiyo liliendesha harakati ya kufuatilia afya ya wanawake, na kufanya kongamano maalum kuhusu hali ya afya ya wanawake, hasa wanawake wa makamo wenye matatizo ya kiuchumi. Matokeo yalionesha kuwa, magonjwa ya kijinsia ya wanawake ndiyo yanatokea mara nyingi zaidi kuliko magonjwa mengine. Asilimia 47 ya wanawake waliopimwa waligunduliwa kuwa na ugonjwa wa matiti, na asilimia 42 wana magonjwa mengine ya wanawake. Wanawake wa makamo waliopunguzwa kazini wenye matatizo ya kiuchumi wako katika kipindi cha kukoma hedhi ambacho ni rahisi kwao kupata magonjwa. Kutokana na matatizo ya kiuchumi, pamoja na kutofahamu umuhimu wa kupima mwili, ni wachache sana wanaoweza kufanya upimaji wa mwili kila baada ya muda fulani.

Shirikisho la wanawake la sehemu ya Shahekou ya mji wa Dalian lilizitaka idara husika kutoa sera maalum ya kuwapima mwili wanawake hao. Chini ya uungaji mkono wa serikali ya kisehemu, baada ya sikukuu ya jadi ya mwaka mpya wa China, harakati ya kupima mwili bila malipo kwa wanawake elfu moja wa makamo wenye matatizo ya kiuchumi ilianzishwa rasmi. Na hospitali ya Shahekou imeamua kupunguza gharama za kuwatibu wanawake hao wanaoumwa.

Idhaa ya kiswhaili 2005-02-24