Ingawa mhalifu aliyemwua waziri mkuu wa zamani wa Lebanon Bw. Rafik Hariri bado hajajulikana, lakini vyama vya upinzani vya nchi hiyo na nchi kubwa za magharibi zimechukua fursa hii kulaani kuwepo kwa jeshi la Syria nchini Lebanon. wachambuzi wanaona kuwa, hivi sasa Syria inakabiliana na shinikizo kutoka kwa nchi kubwa za magharibi na nchi za kiarabu, na Rais Bashar al-Assad wa Syria anakabiliana na uamuzi mgumu katika suala hilo.
Rais Mubarak wa Misri siku hiyo alitoa taarifa huko Sharam el-Sheikh kuwa, hali ya kimataifa na kikanda imebadilika, Syria haiwezi kukabiliana na shinikizo kutoka kwa jumuiya ya kimataifa, lazima itafute njia mwafaka ya kutatua suala hilo.
Siku hiyo, msemaji wa Ikulu ya Misri alitoa taarifa kuwa, Rais Mubarak wa nchi hiyo ameamua kumtuma waziri wa upelelezi wa nchi hiyo Bw. Omar Suleiman kufanya usuluhishi kuhusu mgogoro unaoukabili uhusiano kati ya Syria na Lebanon. msemaji huyo pia alisema kuwa, kutokana na hali ya hivi sasa, Misri ni lazima ichukue hatua mwafaka kwa haraka, ili kutatua suala hilo ndani ya jumuiya ya nchi za kiarabu.
Kabla ya hapo, katibu mkuu wa jumuiya ya nchi za kiarabu Bw. Amr Musa hivi karibuni alifanya ziara katika nchi hizo mbili. Baada ya kukutana na Bw. Bashar alisema kuwa, Syria inataka kuondoa jeshi lake kutoka nchini Lebanon kwa kufuata makubaliano ya Taif. Rais Emile Jamil Lahoud wa Lebanon jana alidokeza kuwa, Bw. Musa alipedekeza kufanya mkutano wa wakuu wa nchi za kiarabu kujadili kuhusu mustakbali wa uhusiano wa nchi hizo mbili, lakini Lebanon ilikataa pendekezo hilo. Rais Lahoud alisema kuwa, viongozi wa Syria na Lebanon wana msimamo mmoja, msingi wa uhusiano maalum kati ya nchi hizo mbili ni makubaliano ya Taif na makubaliano ya kindugu ya ushirikiano kati ya nchi hizo mbili. Hivyo, hakuna haja ya kufanya mkutano huo.
Wakati huohuo, Rais Bush wa Marekani kwenye mkutano na waandishi wa habari baada ya kukutana na Chansela wa Ujerumani Bw. Gerhard Schroeder jana, alisema kuwa, Marekani inasubiri jibu la Syria kuhusu msimamo wake katika suala la kuondoa jeshi, ama sivyo, Marekani itawasilisha suala hilo kwenye baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kuiwekea vikwazo Syria.
Aidha, mkutano wa wakuu wa Marekani na nchi za Ulaya ulitoa taarifa tarehe 22, ukihimiza Syria kutekeleza mara moja azimio No. 1559 la Baraza la Usalama na kuondoa jeshi lake nchini Lebanon. kwenye mkutano huo, Rais Chirac wa Ufaransa ameilaani Syria "kuikalia kijeshi" ardhi ya Lebanon.
Mpaka sasa, maafisa wa Syria na Lebanon hawajabadilisha msimamo wao kuhusu uhusiano wa nchi hizo mbili na suala la kuondoa jeshi. Lakini kifo cha Bw. Hariri kiliathiri sana hali ya nchini Lebanon, na serikali ya hivi sasa ya nchi hiyo inayoongozwa na waziri mkuu Bw. Omar Karami inakabiliwa na hali ya wasiwasi.
Wachambuzi wanaona kuwa, kuilazimisha Syria kuondoa jeshi lake nchini Lebanon ni hatua ya kwanza kwa nchi kubwa za magharibi kuingilia mambo ya ndani ya Lebanon. baada ya Syria kuondoa jeshi lake, hatua ifuatayo itakuwa ni kunyang'anya silaha kutoka kwa makundi haramu ya kijeshi nchini humo, na hiyo hakika itasababisha hali ya nchini humo kuvurugika zaidi. Hivyo, baadhi ya watu wanaopinga Syria kuondoa jeshi lake nchini Lebanon waliainisha kuwa, hivi sasa hali ya nchini Lebanon imefikia muda wa hatari, kama jeshi la Syria likiondoka nchini Lebanon, uhusiano maalum kati ya nchi hizo mbili utavunjika na hadhi ya nchi hizo mbili katika mchakato wa amani ya Mashariki ya Kati itaathiriwa vibaya, hata Lebanon huenda italazimishwa kulegeza masharti katika suala la wakimbizi wa Palestina kukaa nchini humo. Hiyo itavuruga uwiano wa nguvu katika jamii ya Lebanon, na hata kusababisha vita vikubwa vya wenyewe kwa wenyewe.
Idhaa ya Kiswahili 2005-02-24
|