Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-02-24 21:44:43    
Ziwa Taihu

cri

 

    Katika enzi za kale Ziwa Taihu liliitwa Zhenze, pia liliitwa Wuhu. Ziwa hilo ni ziwa kubwa la tatu lenye maji baridi nchini China, na eneo lake ni zaidi ya kilomita za maraba 2000. Kuna visiwa 48 na milima 72 katika eneo la ziwa hilo.

    Kando za mashariki, kaskazini, magharibi na visiwa vilivyoko katika ziwa hilo ni chimbuko la utamaduni wa Wu na Yue wa sehemu ya mashariki ya China. Kuna mabaki mengi ya kale, kama vile mabaki ya mji wa Helu na mji wa Yue wa Enzi ya Spring na Autumn, mfereji wa Jinghang uliochimbwa katika Enzi ya Sui, daraja la Baodai lililojengwa katika Enzi ya Tang, pamoja na hekalu la Zijin lililojengwa katika Enzi ya Song.

    Eneo la Ziwa Taihu linamilikiwa na mikoa ya Jiangsu, Zhejiang na Anhui na mji wa Shanghai. Eneo la mito hiyo mkoani Jiangsu ni kilomita za mraba 19399 ambalo linachukua asilimia 52.6 ya eneo lote; eneo hilo mkoani Zhejiang ni kilomita za mraba 12093 ambalo linachukua asilimia 32.8; mjini Shanghai ni kilomita za mraba 5178, yaani asilimia 14, na mkoani Anhui kilomita za mraba 225, yaani asilimia 0.6. Katika eneo hilo la ziwa, kuna jiji la Shanghai, miji ya Suzhou, Wuxi, Changzhou na Zhenjiang mkoani Jiangsu na mji wa Hangzhou, Jiaxing na Huzhou mkoani Zhejiang. Kwa ujumla kuna miji na wilaya 30. Miongoni mwa miji hiyo, kuna mji mmoja wenye wakazi zaidi ya milioni 5, mmoja wenye wakazi kati ya milioni 1 hadi milioni 5, mitatu yenye wakazi kati ya laki 5 na milioni 1, na sita yenye wakazi kati ya laki 2 hadi laki 5.

   Watu wa China walianza kutumia maliasili ya maji ya ziwa hilo tangu maelfu ya miaka maelfu kadhaa iliyopita, na wamekuwa na maarifa mengi ya uchimbaji wa mifereji na ujenzi wa miradi ya maji. Wameifanya sehemu hiyo iwe na maendeleo makubwa ya kiuchumi na uzalishaji mkubwa wa mazao na bidhaa.

    Ziwa Taihu linaweza kulimbikiza maji katika majira yenye mvua nyingi. Si kama tu sehemu ya chini ya mito ya eneo hilo inatumia maji ya Ziwa Taihu kwa umwagiliaji maji mashambani, bali pia sehemu kubwa ya juu ya mito hiyo pia inatumia maji hayo.

    Ziwa Taihu lenye eneo kubwa na kina kifupi limeweka mazingira mazuri kwa ufugaji wa samaki. Kuna aina zaidi ya 30 za samaki na kamba katika ziwa hilo, miongoni mwao, samaki wa whitebait, kamba weupe na samaki wa anchovy ni chakula kitamu sana. Ziwa Taihu ni kituo muhimu cha uvuvi wa maji baridi nchini China, uzalishaji wa samaki wa maji baridi unachukua asilimia 10 ya uzalishaji wote nchini China. Kuanzia mwishoni mwa karne iliyopita, watu wengi pia walianza kufuga kaa katika sehemu ya mashariki ya ziwa hilo.

    Kuna mandhari nzuri na majengo mengi ya kale katika eneo la Ziwa Taihu. Vivutio maarufu vya utalii ni pamoja na bustani ya Li, bustani ya Yuantouzhu, Mlima Mashariki na Mlima Magharibi. Ziwa Taihu limeunganisha pamoja miji miwili ya utalii ya Suzhou na Hangzhou, na kuunganisha sehemu zote zilizoko kusini ya Mto Changjiang mashariki mwa China.

    Ziwa Taihu linafanana na lulu iliyoko katika delta ya Mto Changjiang. Kutumia maliasili za ziwa hilo na kulihifadhi ni wajibu wa Wachina.

Idhaa ya Kiswahili 2005-02-24