
Tarehe 24 wajumbe wapya wa mamlaka ya utawala wa Palestina waliapishwa rasmi huko Ramallah. Wachambuzi wanaona kuwa baraza jipya litakaloongozwa na waziri mkuu Ahmed Qureia litakuwa muhimu kwa mustakbali wa Palestina na hali ya wasiwasi kati ya Palestina na Israel.
Mwenyekiti wa mamlaka ya utawala wa Palestina Mahmoud Abbas alisimamia sherehe ya kuapishwa kwa wajumbe hao. Alisema wajumbe walioapiswa ni wataalam vijana, akitumai kuwa wajumbe hao watawajibika vizuri katika kuwahudumia vyema watu wa Palestina, Bw. Mahmoud Abbas alionesha kuwa na imani kubwa wajumbe hao wapya.
Ofisa mmoja mwandamizi wa kundi la Fatah alieleza kuwa ikilinganishwa na viongozi wa zamani, baraza hilo sasa hivi limetilia maanani dhana ya "wataalam waliongoze taifa". Wajumbe wengi wamechaguliwa kutoka wataalam zaidi ya mia moja, na wana sifa za elimu ya juu na upeo mpana wa elimu. Imefahamika kuwa miongoni mwa wajumbe 24 wa baraza la mawaziri kumi wana shahada ya udaktari na wengine wana shahada ya pili.
Wajumbe wa baraza la mawaziri wamechaguliwa kwa kanuni ya "wenye elimu ndio wachaguliwe", ambayo imevunja kanuni ya zamani ya kuchagua wajumbe kutoka mirengo tofauti ya kisiasa. Kutokana na hayo, baadhi ya wajumbe ambao wana sifa mbaya au wanashukiwa kwa ufisadi "wamepembuliwa". Hali hiyo imeleta hewa safi ya kisiasa katika ulingo wa siasa nchini Palestina.
Wachambuzi wanaona kuwa serikali mpya itasaidia kuimarisha nafasi ya utawala wa Abbas na kutekeleza siasa iliyowekwa tayari kuhusu mambo ya ndani na nchi za nje. Wasaidizi wakubwa wa Abbas, jemedari mkuu Bw. Nasser Yusuf na waziri wa zamani wa usalama Bw. Mohammed Dahlan wamechaguliwa kuwa mawaziri wa mambo ya ndani na wa mambo ya raia. Bw. Yusuf siku zote anatetea kuchukua hatua kali kwa vikundi vyenye siasa kali nchini Palestina. Katika miaka ya 90 ya karne iliyopita aliamrisha kupambana vikali na kikundi cha Hamas, na kutokana na hayo aliteuliwa kuwa waziri wa mambo ya ndani anayeshughulikia jeshi la usalama la Palestina. Kufanya hivyo licha ya kuonesha nia thabiti ya kufanya mageuzi ya jeshi la usalama la Palestina pia kumetoa dalili kwa vikundi vya siasa kali vilivyokuwa vikitishia mamlaka ya utawala wa Palestina, na kufanya hivyo pia kumetoa mchango mkubwa kwa ajili ya kusimamisha vita kati ya Palestina na Israel na kutuliza hali ya wasiwasi nchini humo.
Licha ya kuwa baraza hilo jipya lina sifa ya "Wataalam", pia limebakiza kiasi fulani mfululizo wa serikali ya zamani ikionesha nia ya kushikilia umoja wa kitaifa. Kati ya wajumbe wa baraza la mawaziri 24, wako sita waliotoka kutoka serikali ya zamani ya Qureia. Waziri wa zamani wa mambo ya nje Bw. Nabil Shaath amekuwa naibu waziri mkuu na waziri wa habari, waziri wa zamani wa viwanda amekuwa waziri wa mpango, na waziri wa fedha wa zamani, waziri wa utamaduni na waziri wa wizara ya wanawake wanaendelea kama zamani. Mpwa wa kiongozi wa zamani wa Palestina hayati Arafat, ambaye alikuwa mwakilishi wa mamlaka ya utawala wa Palestina katika Umoja wa Mataifa, Bw. Nasser al-Kidwa amekuwa waziri wa mambo ya nje, na waziri wa mazungumzo Bw. Saeb Erekat hayupo katika orodha ya wajumbe wa baraza, lakini anaendelea kuwa mjumbe wa kwanza wa mazungumzo.
Wachambuzi wanaona kuwa baraza hilo jipya sio tu limeridhisha kilio cha watu wa Palestina, bali pia limeonesha nia na ujasiri kwa jumuiya ya kimataifa katika juhudi za kusukuma mbele mchakato wa amani na kutaka kuanzisha mazungumzo mapya ya amani na Israel. Kwa mujibu wa kanuni ya "ramani ya njia ya amani" ya Mashariki ya Kati, Palestina ni lazima ifanye kikamilifu mageuzi ya kisiasa kabla ya kuanza kutekeleza kanuni hiyo. Israel na Marekani siku zote zinatetea mageuzi ya kisiasa ya Palestina yawe sharti la mwanzo kabla ya kusukuma mbele mchakato wa amani kati ya Palestina na Israel, na mara nyingi zilizimamisha mazungumzo kwa kisingizio cha Palestina kutofanya mageuzi. Kuundwa kwa serikali hiyo mpya kumeondoa kisingizio hicho, na kutarekebisha na kuimarisha hadhi ya Palestina katika mazungumzo na kuondoa zaidi vikwazo vya kuanzisha tena mchakato wa amani.
Idhaa ya kiswahili 2005-02-25
|