Mkutano wa kimataifa kuhusu suala la mashariki ya kati unatazamiwa kufanyika tarehe mosi Machi huko London, Uingereza, mkutano huo utajadili hasa mageuzi ya Palestina katika sekta za siasa na usalama pamoja na utoaji misaada ya kimataifa kwa Palestina.
Hili ni tukio muhimu katika mchakato wa amani ya mashariki ya kati baada ya uchaguzi mkuu wa Palestina uliofanyika mwezi Januari mwaka huu, na mkutano wa wakuu wa pande 4 uliofanyika mwezi Februari huko Sharm el Sheikh nchini Misri mwaka huu. Vyombo vya habari vyote vina matumaini na mkutano huo na kuona kuwa Palestina na pande zote zinazohusika za jumuiya ya kimataifa zimefanya juhudi kubwa.
Kabla ya kufanyika kwa mkutano huo, Palestina imeanzisha serikali mpya baada ya mgogoro wa kuunda serikali. Serikali hiyo mpya iliwachagua watu wenye utaalam na heshima, badala ya wafuasi wa karibu wa kiongozi wa zamani Arafat na maofisa waliokuwa wanajihusisha na ufisadi. Baada ya kutangazwa kwa orodha ya majina ya wajumbe wa serikali hiyo mpya, orodha hiyo ilisifiwa na walimwengu wengi, hata waziri wa mambo ya nje wa Israel Bw Silvan Shalom aliisifu na kusema kuwa hii ina umuhimu mkubwa kwa mashariki ya kati ya siku za usoni. Hatua hiyo imechukuliwa kuwa ni mwanzo mpya wa mageuzi ya Palestina, pia inamsaidia Bwana Abbas kuitaka jumuiya ya kimataifa iweke shinikizo dhidi ya Israel kwenye mkutano wa London, na kumwezesha kujipatia misaada mingi ya kimataifa.
Aidha, Marekani inaona kuwa kama suala la Palestina na Israel halitaweza kutatuliwa, mpango wake wa demokrasia ya sehemu kubwa ya mashariki ya kati hautaweza kuenezwa, hivyo rais Bush aliongeza juhudi za kidiplomasia tangu aanze awamu ya pili ya urais. Mwanzoni mwa mwezi Februari mwaka huu, Bibi Rice akiwa waziri mpya wa mambo ya nje wa Marekani alifanya ziara ya kwanza kwenye sehemu ya Palestina na Israel, ambapo alieleza matumaini kuwa mchakato wa amani ya Palestina na Israel utaweza kupata maendeleo makubwa. Ili kueleza uungaji mkono kwa kiongozi mpya wa Palestina Bwana Abbas, Bibi Rice aliahidi kuwa serikali ya Marekani itasaidia Palestina kufufua uchumi na kujenga upya kikosi cha usalama cha Palestina. Baadaye rais Bush alimtuma tena Bibi Rice kuhudhuria mkutano utakaofanyika huko London. Wachambuzi wanaona kuwa mabadiliko yaliyotokea ndani ya Palestina baada ya Arafat kufariki dunia yameifanya Marekani kupoteza kisingizio cha kuendelea kuitenga Palestina. Hivi sasa Marekani imeanza kuzingatia kidhahiri maombi ya Palestina, na inaanza kurekebisha kwa kiasi fulani msimamo wake wa kuipendelea tu Israel.
Baada ya Arafat kufariki dunia mwezi Novemba mwaka jana, maendeleo mapya yamepatikana katika mchakato wa amani ya mashariki ya kati uliokwama. Jumuiya ya kimataifa inapofurahia pia inafanya juhudi kuzihimiza Palestina na Israel zifufue mazungumzo ya amani. Hii pia ni nia ya Uingereza kupendekeza kuitisha mkutano wa kimataifa wa London kuhusu suala la mashariki ya kati. Uingereza inatumai kutegemea juhudi zake huo kuinua heshima yake duniani na kujenga upya sura yake iliyoharibika vibaya kutokana na kuifuata Marekani kuanzisha vita dhidi ya Iraq.
Ingawa hayo yote yanaleta matumaini kwa mkutano huo, lakini bado ni vigumu kukadiria kuwa ahadi na makubaliano yatakayofikiwa kwenye mkutano huo yataweza kutimizwa au kutekelezwa au la. Waziri mkuu wa Uingereza Tony Blair tarehe 25 alisema kuwa, mkutano wa London ni hatua moja tu ya kutimiza amani ya kudumu ya mashariki ya kati, vilevile ni mwanzo mpya tu, bado kuna njia ndefu katika kutatua kikamilifu suala la Palestina na Israel.
Idhaa ya kiswahili 2005-02-28
|