Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-02-28 16:03:31    
Russia na Iran zasaini mkataba wa kutoa vifaa vya nishati ya nyuklia na kurejesha mabaki yake

cri

Russia na Iran tarehe 27 zilisaini mkataba wa kukipatia kituo cha kuzalisha umeme kwa nishati ya nyuklia cha Busher cha Iran vifaa vya nishati ya nyuklia na kurejesha mabaki ya vifaa hivyo. Wachambuzi wanaona kuwa kusainiwa kwa mkataba huo kumeondoa vikwazo kwa kuanza kufanya kazi kwa kiwanda hicho kuonesha kuwa ushirikiano kati ya Russia na Iran katika eneo la nishati ya nyuklia umepata maendeleo makubwa.

Mkuu wa idara ya nishati ya atomiki ya Russia Bw. Alexander Rumyantsev aliyefanya ukaguzi katika kituo cha Busher na makamu wa rais wa Iran Bw. Gholarem R. Agazade walisaini mkataba huo siku hiyo. Kutokana na mkataba huo, Iran imekubali kurejesha mabaki yote ya vifaa vya nishati ya nyuklia kwa Russia. Katika msingi huo, Russia itakipatia kituo hicho vifaa hivyo na kufungua kinu cha nishati ya nyuklia. Russia inaona kuwa mkataba huo unazuia kabisa Iran isitengeneze silaha za nyuklia kwa mabaki ya vifaa hivyo. Habari zinasema kuwa uzito wa sehemu ya kwanza ya vifaa hivyo vitakavyotolewa na Russia kwa Iran ni tani 90.

Bw. Alexander Rumyantsev aliposaini mkataba huo alieleza kuwa Russia na Iran zitafuata kwa makini sheria husika za kimataifa katika ushirikiano wa kutumia nishati ya nyuklia kwa amani.

Mwaka 1995, Russia na Iran zilisaini mkataba kuhusu Russia kuisaidia Iran kujenga kituo cha kuzalisha umeme kwa nishati ya nyuklia cha Busher. Hivi sasa kimsingi kituo hicho kimekamilika.

Wachambuzi wanaona kuwa kusainiwa kwa mkataba huo kunatokana na maslahi ya pamoja ya pande hizo mbili.

Kwanza, pande hizo mbili zote zitapata faida kubwa ya uchumi kutokana na ushirikiano huo. Russia itapata faida ya dola za kimarekani bilioni moja katika ujenzi wa kituo hicho na Iran itaondoa upungufu wa nishati na kuendeleza viwanda na teknolojia husika nchini humo.

Pili, ushirikiano kati ya Russia na Iran una maslahi ya pamoja ya kimkakati. Katika miaka kadhaa iliyopita, Marekani iliongeza nguvu zake katika ghuba ya uajemi na bahari ya Caspian. Russia na Iran zina maslahi ya pamoja katika kudumisha hali ya uwiano wa kimkakati katika sehemu hiyo.

Tatu, ushirikiano kati ya nchi hizo mbili unasaidia utulivu wa sehemu hiyo, kwani Russia na Marekani zote hazitaki kupambana kijeshi katika sehemu hiyo. Tena Russia ilitaka kwa uthabiti kusaini mkataba na Iran kuhusu kurejesha mabaki ya vifaa vya nishati ya nyuklia. Kwa hiyo ushirikiano kati ya Russia na Iran kuhusu nishati ya nyuklia unasaidia kutatua suala la nyuklia ya Iran kwa mazungumzo.

Wachambuzi wanakadiria kuwa Russia na Iran pia zinatazamiwa kupanua ushirikiano katika mambo ya kijeshi na sekta ya mafuta.

Idhaa ya kiswahili 2005-02-28