Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-03-01 14:17:40    
Barua 0227

cri
    Msikilizaji wetu Michael Mkufya wa sanduku la posta 10263 Mwanza Tanzania ametuletea barua akianza kwa kutoa shukrani na pongezi nyingi kwa uongozi wote wa Radio China Kimataifa, hasa kutokana na vipindi mbalimbali vya radio na matangazo yanayopatikana kwenye tovuti ya internet. Anasema anatoa pongezi kutokana na jinsi tunavyopangilia habari mbalimbali na anapendekeza tuongeze muda wa matangazo. Pia anasema kama kuna uwezekano ule muda ambapo tunarusha matangazo saa 11 jioni kupitia kampuni ya KBC, anapendekeza yawe yanarushwa moja kwa moja, pamoja na yale yanayopatikana kwenye mtandao wa internet.

    Tunaona mapendekezo yake ni mazuri, siku hizi tunazingatia na tunajitahidi kufanya maandalizi, mara tukipata nafasi tutafanya vivyo hivyo ili kuboresha vipindi vyetu kwenye tovuti.

    Pia anapendekeza kuwa ili kuboresha matangazo na kuongeza uhondo kwa wasikilizaji wetu, ana maoni mengine ambayo anaomba yafikiriwe. Yeye mwenyewe anapenda midahalo. Sasa basi anasema yeye yuko tayari kuleta mada mbalimbali ambazo zitamtia kila msikilizaji hamu ya kusikiliza vipindi na kushiriki kwenye mdahalo. Ikiwezekana liwekwe hata shindano na mshindi atakayechangia sana mada hiyo, basi apewe zawadi, hata kama ni gazeti.

    Bwana Mkufya anasema, kila nchi ina vituko vya kuchekesha kama utani au vikatuni vya kuchekesha. Ametoa mfano unaosema: Huko Mwanza kuna mtoto alizaliwa na kuanza kuomba maji na kusema kuwa, anajisikia vizuri kuwepo duniani kwani tumboni mwa mama yake alikuwa anasikia kiu. Huu ni mfano tu, kunaweza kukawa na visa vingi vya kuchekesha na kusisimua, anasema vile vile tunaweza hata kuwaletea wasikilizaji visa vya kichina ili wasikilizaji wafaidi zaidi.

    Pia ana kichekesho kingine kinachosema usukumani kuna kijiji ambacho watu wakisikia gari wanakimbilia polisi, wanadhani kuwa ni majambazi wanakuja, au mtu ukivaa koti refu anaweza kuuawa kwa kudhaniwa kuwa ni jambazi, maana makoti makubwa wanasema yanatumiwa na wezi pamoja na majambazi.

    Bwana Mkufya pia anatoa pongezi nyingi kwa tovuti ya idhaa ya kiswahili ya Radio China kimataifa, anasema hivi sasa tovuti hiyo imeboreshwa na wanaomba tuiboreshe zaidi ili hata wasikilizaji wetu wanaosikiliza radio siku moja moja, wasiwe nyuma na wale wanaosikiliza kila siku. Ili kuboresha radio yetu zaidi, anapendekeza kuwe na maswali yanayoulizwa kila mwisho wa kipindi, na yawekwe pia kwenye tovuti yetu.

    Anaomba pia kila mwezi, tutoe mada za kujadili kutoka sehemu nyingine mbalimbali kuhusu mambo ya kiuchumi, kijamii na hata kimazingira. Yeye mwenyewe yuko tayari kuleta mada zitakazojadiliwa na iwe kama mashindano, mshindi anaweza kupewa hata kadi, hii inatosha. Anasema anatumai kuwa ombi lake litafikiriwa, na yeye yuko pamoja nasi katika mwaka huu 2005 ili kuboresha matangazo yetu.

    Mwisho Bwana Mkufya anamalizia kwa ujumbe kuhusu ugonjwa wa ukimwi. Anasema, "Sisi binadamu tunashangaza sana, watu wanaogopa mafuriko na kunyeshewa na mvua, tena wanajikinga kwa miamvuli na makoti ya mvua, lakini hawaogopi Ukimwi.

    Anasema cha ajabu ni kwamba watu wanajua kabisa kuwa ukimwi unaua na hauna dawa, lakini bado wanafanya ngono bila kujikinga." Sasa basi inakuwaje watu wanaogopa mvua na maji kuliko ukimwi? Tusaidiane!!! Hii ni laana, ujinga au ni nini? Ni kama mtu anaona tangazo "usikojoe hapa" lakini anakojoa pale pale alipokatazwa, sasa kwa njia hii ukimwi utaisha?

    Tunamshukuru kwa dhati Bwana Mkufya kwa barua yake, maoni na ujumbe wake. Ni matumaini yetu kuwa ataendelea kutuletea barua na kutoa mapendekezo ya kutusaidia tuboroeshe vipindi vyetu.