Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-03-01 14:54:13    
Maendeleo ya hali ya mambo kuhusu suala nyuklia la Iran yafuatiliwa na watu

cri

    Mkutano wa siku 4 wa majira ya mchipuko wa Shirika la nishati ya atomiki duniani ulifunguliwa tarehe 28 Februari huko Vienna. Ajenda ya mkutano huo ni kuhusu suala la nyuklia la Iran, kama ilivyokuwa kwenye mikutano iliyofanyika katika miaka miwili ya hivi karibuni. Lakini kutokana na ziara aliyoifanya rais Bush wa Marekani barani Ulaya, na Russia na Iran kusaini mkataba wa nishati ya nyuklia tarehe 27, maendeleo ya hali ya mambo kuhusu suala la nyuklia la Iran yanafuatiliwa tena na watu.

    Kabla ya kufunguliwa kwa mkutano huo, katibu mkuu wa Shirika la nishati atomiki duniani Bw Mohamed El Baradei alisema kuwa, shirika hilo litaendelea na uchunguzi kuhusu miradi ya nyuklia ya Iran, ili kueleweshwa kila kitu cha miradi yote ya nyuklia ya Iran na kuthibitisha kuwa Iran haifanyi kazi yoyote isiyoripotiwa kwa shirika hilo. Kufanya hivyo ndio kunaweza kuiwezesha Iran kuwa na uaminifu katika jumuiya ya kimataifa. Bwana Baradei anatumai kuwa Iran inaweza kufanya ushirikiano zaidi na jumuiya ya kimataifa katika siku zijazo, na kupashana habari zaidi na shirika la nishati ya atomiki duniani kuhusu miradi yake ya nyuklia. Ofisa aliyehudhuria mkutano huo alidokeza kuwa, kwenye mkutano huo shirika hilo bado halijaweza kutoa azimio kuhusu suala la nyuklia la Iran, azimio muhimu litatolewa kwenye mkutano wa baraza la shirika hilo utakaofanyika mwezi Juni mwaka huu.

    Katika muda mrefu uliopita, kuizuia Iran ni sehemu muhimu ya sera ya Marekani kwa mashariki ya kati, na kuilazimisha Iran kuacha mpango wake wa nyuklia ni kazi muhimu zaidi ya sera ya Marekani kwa Iran. Marekani siku zote inailaani Iran kuendeleza kisirisiri silaha za nyuklia kwa kisingizio cha matumizi ya amani ya nishati ya nyuklia, na inaeneza bila kusita propaganda yake ya "Tishio la nyuklia la Iran". Mbali na kuilazimisha Iran iache mpango wa nyuklia, kusudi lake pia ni kujipatia kisingizio cha kuiwekea Iran vikwazo vya kiuchumi ama kuichukulia hatua za kijeshi katika siku za usoni. Tokea katikati ya mwezi Januari mwaka huu, Marekani imetilia mkazo zaidi kuiwekea Iran shinikizo. Rais Bush, waziri mpya wa mambo ya nje Condoleezza Rice na waziri wa ulinzi Donald Rumsfeld wote walieleza msimamo wao kwa maneno makali.

    Lakini msimamo huo wa Marekani umepingwa na nchi tatu Ufaransa, Ujerumani na Uingereza za Umoja wa Ulaya. Siku chache zilizopita, wakati Bush alipozitembelea nchi za Ulaya, viongozi wa nchi za Umoja wa Ulaya walisisitiza nia yao imara ya kufanya mazungumzo ya amani ili kutatua suala la nyuklia la Iran, tena wameitaka Marekani ishiriki kwenye juhudi hizo. Kutokana na hali na mahitaji ya Marekani yenyewe, katika ziara yake ya Ulaya, rais Bush hakuwa na la kufanya ila tu kuunga mkono Umoja wa Ulaya kufanya mazungumzo na Iran.

    Katika muda mrefu uliopita, kumekuwa na migongano mikubwa kati ya Russia na Marekani kuhusu suala la nyuklia la Iran. Tarehe 27 Februari Russia na Iran zilisaini makubaliano kuhusu Russia kutoa nyenzo za nyuklia kwa kituo cha Iran cha kuzalisha umeme kwa nishati ya nyuklia.

    Habari zinasema kuwa, Marekani imekasirishwa sana na kusainiwa kwa makubaliano hayo kati ya Russia na Iran. Marekani inaona kuwa Russia inaisaidia Iran kufanya mambo mabaya. Umoja wa Ulaya umeeleza kuwa, ushirikiano huo kati ya Russia na Iran hauna mgongano na lengo la Umoja wa Ulaya, kwani Umoja wa Ulaya haupingi Iran kutumia kiamani nishati ya nyuklia, tena unapenda kutoa nishati na teknolojia za nyuklia kwa Iran. Wachambuzi wamedhinisha kuwa, kutokana na hatua ya Russia, migongano kati ya Marekani na nchi nyingi wanachama wa shirika la nishati la atomiki duniani kuhusu suala la nyuklia la Iran inaonekana wazi.