Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-03-01 15:43:41    
Soko maarufu la uuzaji wa vitu vilivyokwishatumika mjini Beijing

cri

Kwenye ramani zilizochapishwa na nchi nyingi duniani kuhusu utalii mjini Beijing, mbali na sehemu maarufu za jadi zilizowekwa alama za sehemu ya utalii kama vile: Ukuta mkuu, Majumba ya Zamani ya Wafalme na bustani ya Majira ya Joto ya Wafalme, pia kuna Soko la Vitu Vilivyokwishatumika la Panjiayuan, ambalo liko kwenye sehemu ya mashariki ya Beijing. Kila ifikapo Jumamosi na Jumapili, kuna watalii wengi kutoka sehemu mbalimbali za nchini na nchi za nje wanaotembelea soko hilo kwa lengo la kununua vitu vya zamani vilivyohifadhiwa na vitu vya sanaa vya jadi vya kichina.

Bibi Gail Cohen kutoka Marekani ni mmoja wa watalii waliofika kwenye soko hilo, alisema,

"Kitabu cha utalii kinasema kuwa hiyo ni sehemu ambayo heri usikose kuitembelea. Hivi sasa nimevutiwa na michoro ya kale iliyochorwa kwenye gamba la mti."

Sababu za kuvutia watu kwa soko la Panjiayuan licha ya kwamba watu wanaweza kupata vitu vya sana ya jadi pamoja na vitu vyenye thamani ya kuhifadhiwa vya kichina kwa bei rahisi, watu wanaweza kupata hati na michoro ya watu mashuhuri wa China pamoja na vitu vya sanaa vyenye asili ya jadi. Kwa mfano, kulikuwa na mtu aliyetumia Yuan 15 kupata upanga mmoja, na aliuuza upanga huo kwa Yuan laki 1 na elfu 50. Matukio kama hayo yanatokea mara nyingi.

Msimamizi wa soko la Panjiayuan Bw. Cui Xinwei alimwambia mwandishi wetu wa habari kuwa chanzo cha matukio hayo ni kuwa vitu vinavyouzwa katika soko hilo vinatoka sehemu mbalimbali nchini kwa kupitia wafanyabiashara ambao baadhi yao hawana uwezo wa kuthibitisha thamani ya vitu vya kale, hivyo inaleta nafasi nyingi za kupata vitu vyenye thamani kubwa kwa wanunuzi. Aliongeza kuwa katika soko hilo kila siku kuna watu wanaotunza vitu vya sanaa ambao wanaangalia vitu kutoka kibanda kimoja hadi kingine cha mwuzaji huku wakitazama vitu mikononi kwa kutumia vioo vya kukuzia (magnifier), na wengi walipata vitu walivyovitafuta. Alisema,

"Wanunuzi magwiji huwa wanafika sokoni mnamo saa kumi alfajiri wakati soko linapofunguliwa. Watu hao wana kiwango fulani cha elimu kuhusu vitu vya kale, hivyo wana shauku ya kununua vitu vyenye thamani ya kuhifadhiwa."

Soko la Panjiayuan lilianzishwa miaka 13 iliyopita, ambapo baadhi ya wakazi wa karibu walipeleka samani na vyombo vya umeme vya nyumbani wasivyovitaka tena kuuzwa huko. Muda si muda wauzaji wakawa wengi, hapo baadaye, idara husika ya serikali ya huko ikajenga soko. Ingawa soko hilo linajulikana kwa uuzaji wa vitu vilivyokwishatumika, lakini ukweli ni kwamba wanunuzi wanaweza karibu kupata vitu vyote wanavyovihitaji.

Hivi sasa, eneo la soko hilo limepanuliwa hadi mita za mraba zaidi ya elfu 50 na limekuwa la kwanza kwa ukubwa hapa nchini, hata katika bara la Asia. Hivi sasa katika soko hilo vimejengwa vibanda zaidi ya 4,000 na kuwa na wafanyabiashara na wafanyakazi karibu elfu kumi kwa jumla.

Bw. Cui alisema kuwa nafasi kubwa ya biashara na msingi mkubwa wa kiutamaduni vimeleta nafasi kubwa ya maendeleo kwa soko la Panjiayuan, kutokana na kuwa vitu vinavyouzwa katika soko hilo vilitoka moja kwa moja katika sehemu zenyewe zinazozalisha bidhaa, hivyo bei za vitu za soko hilo ni nafuu kuliko sehemu nyingine, hivyo biashara yetu inaendelezwa motomoto. Mwaka 2003, thamani ya bidhaa zilizouzwa katika soko la Panjiayuan ilizidi Yuan milioni 400.

Katika soko la Panjiayuan wanunuzi wanaweza kupata vitu adimu vyenye thamani kubwa na kuona vitu vya aina mbalimbali vya sanaa za jadi ya China, ambavyo ingawa vilizalishwa miaka ya karibuni, lakini ni vyenye umaalum wa sanaa za jadi ya China. Hivi sasa, soko la Panjiayuan si kama tu limekuwa mahali pa kupata vitu wanavyovipenda mashabiki wa kuhifadhi vitu vya kale, bali imekuwa daraja la kufahamu utamaduni wa China kwa wageni wa kutoka nchi za nje. Huko bibi Hillary Clinton ambaye ni mke wa Bw. Bill Clinton, rais wa zamani wa Marekani alinunua buli iliyotengenezwa kwa stannum miongo kadhaa iliyopita. Binti mfalme wa Thailand, waziri mkuu wa Romania na waziri mkuu wa Ugiriki pia wamewahi kufika huko. Habari zinasema kuwa kiasi cha 80% ya bidhaa zinazouzwa kwenye mtaa wa vitu vya kale mjini Seoul, Korea ya Kusini zinatoka katika soko la Panjiayuan, Beijing. Wafanyabiashara wanaouza vitu kwenye mtaa wa vitu vya kale mjini Osaka, Japan hawakosi kufika soko la Panjiayuan kila mwezi, na kila mara hununua vitu vya malori zaidi ya kumi.

Hivi leo, mashirika mengi ya utalii yanayoshirikisha watalii kutembelea Beijing huwa yanapeleka watalii wao kutembelea soko la vitu vya kale la Panjiayuan, ambalo linajulikana kama Ukuta Mkuu, chakula cha bata wa kuokwa na majumba ya wafalme wa zamani.

Hivi karibuni soko la Panjiayuan limechapicha karatasi zenye maandishi ya lugha za kigeni za kuelekeza watalii kuhusu soko hilo, na kuwekwa vibao vya kuelekeza njia kwa lugha za kigeni, licha ya hayo limejiandaa kuwa na waongozaji wanaofahamu lugha za kigeni bila malipo kwa ajili ya wageni kutoka nchi za nje katika siku za Jumamosi na Jumapili. Dada Kang Qian, ambaye ni mmoja wa waongozaji wa watalii katika soko hilo, alisema,

"Mimi ninawatembeza wageni, kwanza kabisa nitawaambia ninawapatia huduma bila malipo yoyote, kisha ninawapa maelezo kidogo na kuwapeleka kununua vitu wanavyotaka."

Mwaka 2008, Beijing itaandaa michezo ya 29 ya Olimpiki, jambo ambalo litaleta nafasi mpya ya maendeleo kwa soko la Panjiayuan. Hivi sasa soko hilo limeorodheshwa na idara husika ya Beijing kuwa moja ya sehemu muhimu ya ununuzi wa vitu, utalii, burudani, utamaduni na huduma.

Idhaa ya kiswahili 2005-03-01