Mkutano wa London unaounga mkono mamlaka ya utawala wa Palestina ulimalizika tarehe 1. Pande zote zilizohudhuria mkutano huo zilifikia maafikiano kuhusu hatua halisi za kujenga nchi ya Palestina kutokana na mpango wa amani ya Mashariki ya Kati na kuahidi kutoa misaada kwa siasa, mageuzi ya usalama na maendeleo ya kiuchumi na kijamii ya Palestina.
Waziri mkuu wa Uingereza Bw. Tony Blair aliendesha mkutano huo ambao uliwashirikisha katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Kofi Annan, waziri wa mambo ya nje wa Marekani Bi. Condoleezza Rice, mwenyekiti wa mamlaka ya Palestina Bw. Mahmood Abbas na wajumbe waandamizi kutoka nchi 23 na jumuiya 6 za kimataifa. Mkutano huo ulitoa taarifa ikisema kuwa pande mbalimbali zilizohudhuria mkutano huo zilieleza kwa kauli moja kusaidia Palestina ifanye mageuzi kuhusu usalama kwa kupitia kikundi cha uratibu wa suala la usalama kinachoongozwa na Marekani na kuupatia ukarabati wa kikosi cha usalama cha Palestina misaada ya fedha.
Pande zote zilizohudhuria mkutano huo zimekubali kwa kauli moja kuupatia fedha na misaada halisi uchaguzi wa Palestina na ujenzi wa miundo ya kisheria na kuzitia moyo nchi zinazokubali kuichangia Palestina zitoe misaada kwa Palestina mapema iwezekanavyo. Pande hizo pia zinakubali kuitisha mkutano wa kimataifa wa kuichangia Palestina mwishoni mwa mwezi Juni na kutoa misaada kwa mpango wa maendeleo ya kipindi cha katikati ya Palestina.
Taarifa hiyo pia imeitaka Palestina iimarishe ushirikiano na Israel na kutimiza ahadi iliyotolewa na pande hizo mbili katika kutekeleza mpango wa amani. Taarifa hiyo pia inasisitiza kuwa baada ya Israel kuondoka kutoka kwa Gaza na baadhi ya sehemu za kando ya magharibi ya mto Jordan, jumuiya ya kimataifa itashirikiana na Israel katika kuzuia kuharibiwa kwa miundo mbinu ya sehemu hiyo na kutoa misaada kwa ukarabati wa Gaza.
Bw. Tony Blair alieleza kwenye mkutano na waandishi wa habari kuwa jumuiya ya kimataifa inaona kuwa nchi ya Palestina inayoweza kuendeshwa inahitaji ardhi kamili na miundo ya taifa inayoendeshwa kwa manufaa.
Bw. Mahmood Abbas aliwasilisha mpango kuhusu mageuzi ya Palestina kwenye mkutano huo, mpango ambao unaahidi kuimarisha kupambana na ufisadi mbali na kuendelea na mageuzi kuhusu usalama, na kufanya uchaguzi wa bunge mwezi Julai mwaka huu.
Idhaa ya kiswahili 2005-03-02
|