Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-03-04 14:17:56    
Suala la nyuklia la Iran latatuliwa kwa ubaridi

cri

    Mkutano wa spring wa Shirika la Nishati ya Atomiki Duniani(IAEA) tarehe 3 ulifungwa huko Geneva. Mkutano huo haukuwa na mengi ya kuzingatiwa, lakini umaalum wake ni kuwa shirika hilo lilitatua suala la nyuklia la Iran kwa ubaridi. Suala hilo kutatuliwa kwa njia hiyo kunatokana na uhusiano mpya kati ya mataifa makubwa, ugumu wa kazi ya ukaguzi na shinikizo kubwa kutoka kwa jumuiya ya kimataifa.

    Hoja ya mwisho ya mwenyekiti iliyotolewa tarehe 3 kwenye mkutano huo haina matakwa mengi, isipokuwa kuitaka Iran kuongeza uwazi na kushirikiana zaidi na IAEA. Maneno hayo hayana tishio kali kama lililotakiwa na Marekani, wala hayaelezi wazi kuwa IAEA itachukua hatua ikiwa Iran haitashirikiana nayo.

    Wachambuzi wanaona kuwa, uhusiano mpya wa mataifa makubwa ni sababu muhimu ya suala la nyuklia la Iran kuwa baridi. Baada ya rais Bush kukutana na viongozi wa nchi za Umoja wa Ulaya na viongozi wa Russia mwezi uliopita, Marekani, ambayo ilisisitiza kuchukua msimamo mkali kwa Iran, sasa kwa mara nyingi inaeleza kuwa itauunga mkono Umoja wa Ulaya kufanya mazungumzo ya amani na Iran.

    Rais Bush alipokuwa ziarani mjini Brussels mwezi uliopita alisisitiza kuwa, suala la nyuklia la Iran bado liko katika kipindi cha kushughulikiwa kwa njia ya kidiplomasia. Alisema kuwa Marekani imeshindwa kutekeleza sera ya upande mmoja katika suala la Iraq, hivyo haitumai kushindwa tena katika suala la Iran. Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Bi. Condoleezza Rice wiki hii huko London alisisitiza tena umuhimu wa juhudi za kidiplomasia za nchi tatu za Umoja wa Ulaya kwa kutatua suala la nyuklia la Iran.

    Marekani pia haiwezi kutozingatia uhusiano kati ya Russia na Iran. Russia imeshirikiana na Iran kwa muda mrefu katika nyanja ya nyuklia. Hivi karibuni Russia inaeleza kuwa inataka kutatuliwa kwa suala la nyuklia la Iran kwa njia ya kidiplomasia, jambo ambalo pia linaifanya Marekani ilegeze msimamo katika suala la nyuklia la Iran.

    Aidha, ingawa IAEA ilifanya ukaguzi kwa Iran, lakini haijapata matokeo kutokana na sababu mbalimbali. Mkuu wa shirika hilo Bw. Baradei na uamuzi wa mwisho wa mkutano huo unaihimiza Iran kushirikiana zaidi na shirika la IAEA na kuongeza uwazi ili kazi ya ukaguzi iweze kuendelea. Bw. Baradei aliona kuwa, kwa kuwa Iran haikushirikiana kikamilifu na shirika hilo, hivyo wakaguzi hawakupata nyaraka zote husika za Iran, hivyo kazi ya ukaguzi haikupata maendeleo makubwa. Katika hali hiyo ya kutokuwa na ushahidi, kutatua suala la nyuklia la Iran kwa ubaridi kunaonekana kuwa ni busara.

    Sauti ya nchi nyingi wanachama kwenye mkutano huo kuunga mkono kutatua suala hilo kwa amani pia inachangia kutatua suala la nyuklia la Iran kwa ubaridi. Shirika la IAEA lina nchi wanachama 35, ambazo nyingi zinaunga mkono kutatua suala hilo kwa njia ya kidiplomasia, hivyo ni vigumu kwa Marekani kuendelea kushikilia msimamo mkali. Kwenye mkutano huo nchi tatu za Umoja wa Ulaya zilisema kuwa, Umoja wa Ulaya unasisitiza kutatua kiamani suala la nyuklia la Iran, na kuhimiza mazungumzo ya nyanja mbalimbali ili kutekeleza makubaliano yaliyofikiwa huko Paris. Mjumbe wa Iran pia alisisitiza kuwa Iran inapenda kufanya mazungumzo na Umoja wa Ulaya, na kushirikiana na shirika la IAEA, hivyo kutatua suala kwa mazungumzo ya amani pia ni chaguo la kwanza kwa Iran.

    Jambo linalopaswa kuzingatiwa ni kwamba, ingawa sababu nyingi zinalifanya suala la nyuklia ya Iran kuwa baridi, lakini mkakati wa Marekani kuhusu Mashariki ya Kati haubadiliki, na Iran hivi sasa bado ni kikwazo muhimu kwa Marekani kutimiza mpango wake wa Mashariki ya Kati. Kama juhudi za kidiplomasia za Umoja wa Ulaya katika suala la nyuklia la Iran hazitapata matokeo yanayotakiwa na Marekani, basi Marekani huenda italifanya suala hilo kupamba moto tena.

Idhaa ya Kiswahili 2005-03-04