Mkutano wa 123 wa baraza la mawaziri wa mambo ya nje la Umoja wa nchi za kiarabu ulifunguliwa jana huko Cairo. Ingawa mawaziri wa Syria na Lebanon wote hawakuhudhuria mkutano huo, lakini mgogoro kati ya nchi hizo mbili ulikuwa suala muhimu lililojadiliwa kwenye mkutano huo. Wakati huo huo, ili kutafuta njia ya kusuluhisha mgogoro huo, nchi za kiarabu pia zilichukua shughuli nyingi za kidiplomasia nje ya mkutano.
Habari zinadokeza kuwa, kwenye mkutano wa faragha uliofanyika baada ya ufunguzi wa mkutano huo, mawaziri hao walisisitiza kuwa, mgogoro wa Syria na Lebanon lazima utatuliwe ndani ya nchi za kiarabu. Pia walisema kuwa wanapinga kithabiti nchi nyingine kuingilia suala hilo. Kwenye ufunguzi wa mkutano, katibu mkuu wa Umoja wa nchi za kiarabu Bw. Amr Moussa alitoa mwito akitaka nchi za kiarabu zichukue hatua zote kusuluhisha mgogoro huo ili kuboresha hali mbaya nchini Lebanon. Waziri wa mambo ya nje wa Yemen Bw. Abu Bakr al-Kurbi alisema kuwa, Yemen inaunga mkono msimamo wa busara wa Syria katika mgogoro huo. Pia alitaka pande husika zitatue suala hilo kwa njia ya mazungumzo ili kuepuka kuingiliwa na nchi nyingine na kusuluhisha mgogoro huo ndani ya nchi za kiarabu.
Wakati huo huo, Rais Hosni Mubarak wa Misri alifanya mazungumzo na waziri wa mambo ya nje wa Saudi Arabia Bw. Soud al-Faisal tarehe 3 huko Sharm el-Sheikh ili kutatua suala hilo. Rais Bashar al Assad wa Syria pia alikwenda Riyadh kukutana na mrithi wa ufalme wa Saudi Arabia Abdulla ili kutafuta njia inayofaa ya kusuluhisha shinikizo kubwa kwa Syria na mgogoro nchini Lebanon. Habari zinasema kuwa, Saudi Arabia na Misri zimependekeza jeshi la Syria nchini Lebanon liondoke kutoka Lebanon "bila aibu" kabla ya mwishoni mwa mwezi Aprili. Muda huo pia ni muda wa mwisho kwa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa kuwasilisha ripoti ya tathmini ya utekelezaji wa azimio ya 1559 kwenye Baraza la Usalama na Lebanon kufanya uchaguzi wa bunge. Kutokana na mapendekezo ya Misri na Saudi Arabia, nchi za kiarabu zimesisitiza tena kuwa jeshi la Syria liliingia Lebanon kwa mujibu wa azimio husika lililofikiwa na Umoja wa nchi za kiarabu mwaka 1976, na Syria lazima itoe ratiba wazi ya kuondoa jeshi lake kutoka Lebanon.
Nchi za kiarabu zinafuatilia sana na kufanya juhudi kusuluhisha mgogoro kati ya Syria na Lebanon kutokana na hali maalum nchini Lebanon, uhusiano maalumu kati ya Lebanon na Syria na athari zao kubwa kwa nchi za kiarabu.
Inajulikana kuwa katika nchi za kiarabu, Lebanon ni nchi pekee ambayo makundi makubwa ya kidini yenye nguvu sawa nchini humo. Wachambuzi wanaona kuwa, jeshi la Syria nchini Lebanon limetoa mchango mkubwa katika kutuliza hali nchini Lebanon na kudumisha asili yake ya kiarabu na kiislamu. Kama jeshi la Syria litaondoka haraka kutoka Lebanon kutokana na shinikizo la kimataifa, asili ya Lebanon itakabiliwa na changamoto kubwa, na jambo hilo si matumaini ya nchi zote za kiarabu na kiislamu.
Aidha, uhusiano maalum kati ya Syria na Lebanon pia ni uhusinano wa kimkakati wa kuipinga Israel kwa nchi za kiarabu na kiislamu. Sehemu ya kusini mwa Lebanon iliwahi kuwa uwanja wa vita wa moja kwa moja wa kuizuia na kuipinga Israel mbali na Palestina. Uhusiano huo uliwahi kutoa mchango mkubwa katika kuimarisha hadhi ya nchi za kiarabu katika mgogoro kati yao na Israel, kurejesha ardhi ya nchi za kiarabu na haki za Wapalestina. Hivyo uhusiano huo ni suala muhimu linalohusu maslahi ya nchi zote za kiarabu. Nchi za kiarabu zina wajibu wa kutatua mgogoro huo. Hivyo nchi nyingi za kiarabu zinataka Syria iondoe jeshi lake kutoka Lebanon zikisisitiza kutatua mgogoro huo ndani ya nchi za kiarabu.
Idhaa ya Kiswahili 2005-03-04
|