Baadhi ya wabunge wa Somalia tarehe 5 waliitisha mkutano na waandishi wa habari huko Nairobi, mji mkuu wa Kenya, ambapo walitoa mwito wa kuitaka jumuiya ya kimataifa iisaidie Somalia kutafuta utatuzi wa suala la takataka zenye uchafuzi zilizomwagwa kwenye bahari iliyoko karibu na Somalia.
Wajumbe wa bunge la mpito la Somalia walisema kuwa baadhi ya mashirika ya Ulaya yalitupa makontena ya takataka za nyuklia kwenye bahari iliyoko karibu na Somalia, na takataka hizo ziliibuka wakati maafa ya tsunami yalipotokea mwishoni mwa mwaka jana, na kuathari vibaya afya ya watu wanaoishi huko. Takataka za nyuklia zimesababisha ugonjwa wa ngozi, matatizo ya kupumua na kutokwa na damu tumboni.
Mbunge mmoja alisema kuwa takataka hizo zimeathari vibaya afya za watu wa huko, pia zimekuwa tishio kubwa kwa wanyama baharini na uvuvi wa Somalia.
Baadhi ya mashirika ya Ulaya yalitumia fursa ya kutokuwepo kwa serikali nchini Somalia, kuanzia mwanzoni mwa miaka ya tisini ya karne iliyopita, yalimwaga takataka nyingi zenye madhara katika bahari iliyoko karibu na nchi hiyo. Katika miaka 10 iliyopita mashirika hayo yalitupa makontena elfu kadhaa ya takataka zenye sumu.
Msemaji wa shirika la mazingira la Umoja wa Mataifa siku chache zilizopita alisema, ripoti moja ya Umoja wa Mataifa imethibitisha kuwa baadhi ya watu waliokumbwa na maafa ya tsunami huko kaskazini mwa Somalia wameanza kutokwa na damu mdomoni na tumboni. Pia alisema, ripoti hiyo imetoa onyo kuwa takataka zilizotupwa kwenye bahari iliyoko karibu na Somalia vilevile zimeathari vibaya mazingira ya nchi jirani za Somalia.
Somalia ilikuwa katika hali ya kutokuwa na serikali kutokana na migogoro ya mfululizo kuanzia mwaka 1991. Mwaka 2004, pande zote zilikubaliana na marekebisho ya katiba ya mpito, na bunge la mpito na baadaye rais wa muda akachaguliwa. Hivi sasa bunge la mpito, rais wa muda na karibu watumishi wote wa serikali ya mpito wako mjini Nairobi ili kutokana na sababu za usalama.
Idhaa ya Kiswahili 2005-03-07
|