Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-03-08 16:44:09    

Barua 0308


cri
Msikilizaji wetu Daniel James Msunzu wa sanduku la posta 840 Kahama-Shinyanga Tanzania ametuletea barua akisema kuwa, anatushukuru watangazaji wa Radio China kimataifa kuendelea kurusha matangazo ambayo wasikilizaji wanayasikia vyema huko kahama, Shinyanga. Anasema ameona ni vyema atushukuru kwa sababu nyingi zinazoonesha jinsi tunavyoonekana kuwajali wasikilizaji wetu, na jinsi tunavyoendelea kufuatilia au kuwaandalia wasikilizaji wetu chemsha bongo nyingi zinazohusu China ya sasa.

Anasema kuwa, taifa la China ni taifa linaloendelea duniani na ni taifa linalozingatia haki za wananchi wake, kwa sababu hiyo tumeweza kuona kuwa makabila madogo madogo ya China yanaweza kupata haki ya kujiendesha wenyewe, na China inalinda haki na maslahi ya raia maskini, kutenga fedha kwa ajili ya matibabu na elimu, na kusisitiza kulinda amani ya dunia bila kutumia nguvu za mabavu. Hayo yote yanastahiki kupongezwa.

Msikilizaji wetu Raje wa Raje wa sanduku la posta 884 Shinyanga Tanzania ametuletea barua akisema kuwa, anafuraha kutuma barua hii ya maombi ya kuhitaji ratiba ya vipindi vyetu, ili aweze kufahamu vizuri tunaanza matangazo yetu saa ngapi, na ni vipindi gani vitatangazwa kwa siku hiyo.

Anasema alifurahishwa na kipindi kilichokuwa kikimwelezea ndugu ambaye hakumbuki jina lake, ila ni wa kabila la uygur ambaye aliwahi kupona kuuwawa na majambazi kwa sababu ya kuimba kwake. Alikuwa haelewi yanayoimbwa kwenye wimbo huo, lakini alifurahia nyimbo zake.

Pia alifurahishwa na maelezo kuhusu hekalu la kale. Kwa jinsi mtangazaji alivyokuwa akielezea, ilikuwa kana kwamba analiona hekalu hilo kwa macho yake. Kwa machache haya anatuomba tumtumie ratiba hiyo ya vipindi, na utaratibu wetu wa matangazo kwa ujumla.

Tunafurahi kusikia wasikilizaji wetu kuwa mnafurahishwa na vipindi vyetu, kuwafurahisha ni moja ya malengo yetu. Kwa kukukumbusha basi, Mwimbaji huyo unayemzungumzia anaitwa Rozi Amuti wa kabila la Uygur, na anatoka mkoa wa Xingjiang.

Msikilizaji wetu Damas. M. Bundala ambaye barua zake huhifadhiwa na Mathias B. Kilima wizara ya afya sanduku la posta 52 Victoria Mahe, visiwa vya shelisheli ametuletea barua akitusalimu, na akitushukuru kwa barua ambazo tumemtumia. Pia anatuomba msamaha kwa kuchelewa kutuandikia barua kutokana na kuwa mgonjwa, na pia mwezi uliofuata alikuwa kwenye pilikapilika za mitihani, na hata hivyo anasema bado ana pilikapilika nyingine za mitihani, ndiyo maana hakuweza kutuandikia kwa wakati.

Kwanza tunampa pole msikilizaji wetu Damas Bundala kutokana na kuumwa, na tunampa pole kutokana na maandalizi ya mitihani. Pia tunapenda kumwambia kuwa, asiwe na wasiwasi kutokana na mwaka jana kuchelewa kutujibu kutokana na sababu mbalimbali, lakini mwaka huu tunatumai kuwa atapata nafasi tena ya kushiriki kwenye mashindano ya chemsha bongo yatakayoandaliwa na idhaa ya kiswahili ya Radio China kimataifa.

Idhaa ya kiswahili 2005-03-08