Mwenyekiti wa mamlaka ya utawala ya Palestina Bwana Mahmoud Abbas jana alikutana na waziri wa ulinzi wa Israel Bwana Shaul Mofaz katika kituo cha ukaguzi cha Erez kilichoko mpakani kati yake na Israel. Japokuwa Bw. Mofaz alisema kuwa, Israel itaikabidhi Palestina madaraka ya udhibiti wa usalama wa miji miwili iliyoko kando ya magharibi ya mto wa Jordan, lakini hakutaja siku halisi ya kukabidhi miji hiyo. Hiyo imeonesha kuwa, mabishano ya kisiasa na kidiplomasia kati ya pande hizo mbili kuhusu kukabidhi madaraka ya udhibiti ya miji ya kando ya magharibi ya mto Jordan yatakuwa makali.
Kutokana na makubaliano yaliyofikiwa kwenye mkutano wa wakuu wa pande nne wa mashariki ya kati uliofanyika mwezi uliopita huko Misri, Israel itaikabidhi Palestina hatua kwa hatua madaraka ya udhibiti wa miji 5 ya kando ya magharibi ya mto Jordan, na kuwaachia huru wafungwa mia kadhaa wa Palestina kwa vipindi mbalimbali. Baada ya hapo, maofisa wa pande hizo mbili waliwahi kufanya mashauriano mara kadhaa kuhusu jambo hilo, lakini kutokana na tukio la mlipuko wa kujiua lililotokea huko Tel Aviv tarehe 25 Februari, Israel ilisimamisha mpango wa kukabidhi madaraka hayo. Pande hizo mbili zilirejesha mazungumzo hayo tarehe 6 mwezi huu.
Suala la kukabidhi madaraka ya udhibiti wa usalama wa miji ya kando ya magharibi ya mto Jordan si kama tu linamaanisha kumaliza ukaliaji wa Israel kwa miji hiyo baada ya mwaka 2000, bali pia linaonesha uhalisi wa sera ya Abbas ya kufanya mazungumzo ya amani, linahusiana sana na heshima ya Abbas kwa watu wa Palestina na utulivu wa hali ya ndani ya serikali ya Palestina, hivyo Palestina ina hamu kubwa ya kuharakisha mchakato huo.
Ili kuvunja hali ya kukwama kwa ushirikiano wa usalama kati ya Palestina na Israel, Bw. Abbas jana alifanya mazungumzo ya moja kwa moja na Bw. Mofaz kuhusu ukabidhi wa madaraka. Baada ya mkutano huo Bw. Mofaz alisema kuwa, Israel itaikabidhi Palestina madaraka ya udhibiti wa usalama wa miji ya Jericho na Tulkarm katika siku chache zijazo, na kukubali kuanzisha kamati husika ili kujadili jinsi ya kulegeza vizuizi dhidi ya wapalestina. Lakini Bw. Mofaz hakutaja tarehe ya ukabidhi huo, alisema kuwa, kuhakikisha usalama wa watu wa Israel ni jukumu la kwanza kwa serikali ya nchi hiyo, hivyo inapaswa kuwa na tahadhari kuhusu jambo hilo. Zaidi ya hayo, pande hizo mbili bado zina tofauti kuhusu maeneo yanayotawaliwa na miji itakayokabidhiwa na kuondoa vizuizi barabarani na vituo vya ukaguzi karibu na miji hiyo.
Vyombo vya habari vinaona kuwa, baada ya kutokea tukio la mlipuko wa kujiua huko Tel Aviv, Israel imeongeza masharti ya kisiasa ya kufanya mazungumzo na Palestina, hairidhiki tena na hatua ya Abbas ya kujaribu kuyashawishi makundi mbalimbali ya Palestina kuacha mapambano dhidi ya Israel, ikisema kuwa, sharti la kwanza la kuanzisha mchakato wa amani kati ya Palestina na Israel ni kuvisambaratisha vikundi vyenye siasa kali. Wakati huo huo, hatua zilizochukuliwa na Abbas katika kufufua utaratibu wa jamii na sheria nchini Palestina kwa kiwango fulani zimewachochesha wanamgambo wa Palestina. Hivyo bado haijulikani kama Bw. Abbas ataweza kuilazimisha Israel kurudi nyuma na kukabidhi madaraka ya udhibiti wa usalama wa miji ya kando ya magharibi ya mto Jordan au la.
Idhaa ya Kiswahili 2005-03-09
|