|
Tarehe 9 idara ya usalama ya Russia imethibitisha kuwa kiongozi wa vikundi vya magaidi vya Chechnya aliuawa tarehe 8 katika oparesheni ya kijeshi ya Russia. Mkuu wa polisi wa Russia anayeshughulikia uchunguzi wa maiti Bw. Grigory Fomenko alisema kwamba, kwa mujibu wa sheria za Russia, maiti ya Maskhadov haitakabidhiwa kwa jamaa zake bali itazikwa kisiri baada ya kukamilisha taratibu za kisheria.
Wataalamu wa masuala ya Chechnya wanasema ingawa Maskhadov alikuwa ni mwenyekiti wa heshima tu wa vikundi vya magaidi vya Chechnya na alikuwa akipata misaada wa fedha kutoka kwa matajiri wa ugaidi na wanasiasa wa nchi za Magharibi, lakini kifo chake hakitaleta athari yoyote kwa hali mbaya ya Chechnya.
Kwanza, kurudisha hali tulivu ya Chechnya ni matakwa ya watu wote wa Chechnya. Mwenyekiti wa Duma Bw. Boris Gryzlov, tarehe 9 aliisifu sana oparesheni ya kumsaka Maskhadov, anaona kuwa oparesheni hiyo itasaidia kutuliza hali ya Chechnya. Rais wa Jumhuri ya Chechnya Alu Alkhanov alisema, Maskhadov ni mmoja tu wa magaidi wa Chechnya, kifo chake hakitaleta athari yoyote kwa hali ya Chechnya na pia alisisitiza kuwa "Wananchi wa Chechnya wameamua mustakbali wao na hatima yao, kwamba wataungana na Russia na kurejesha maisha ya utulivu na ya amani".
Pili, Nguvu za ufarakanishaji za Chechnya pengine zitafarakana kwa mara nyingine tena. Hivi sasa vikundi vya magaidi vya Chechnya vinafanya mashambulizi kama vitakavyo. Maskhadov alipokuwa hai vikundi vya ugaidi vilionekana kama vinaongozwa naye lakini kwa heshima tu. Kabla ya kupata kiongozi mwingine, pengine kutatokea migongano kuwania madaraka ya uongozi kati ya vikundi hivyo. Kwa hiyo baada ya Maskhadov kuuawa, makamu wa kwanza wa waziri mkuu wa Jamhuri ya Chechnya, Ramzan Kadyrov, mara alivitaka vikundi vya ugaidi visimamishe vitendo vyao na kurudi kwenye maisha ya amani.
Tatu, kuna uwezekano wa magaidi wa Chechnya kulipiza kisasi. Suala al ugaidi nchini Chechnya ni sugu na la utatanishi, haliwezekani kumalizika kutokana na kifo cha kiongozi huyo tu, bali magaidi wataendelea kufanya matukio mbalimbali ili kufanikisha malengo yao ya kisiasa. Mwenyekiti wa kamati ya Shirikisho la Russia, Sergei Mironov, alisema kuuawa kwa Maskhadov ni mafanikio ya mapambano dhidi ya ugaidi, lakini sio mafanikio ya mwisho. Kwa makadirio, kifo cha Maskhadov pengine kitabadilisha mbinu za kivita za magaidi katika sehemu ya kaskazini ya Caucasus. Tarehe 9 msemaji wa mke wa Maskhadov aliyekuwa uhamishoni Uingereza, Akhmed Zakaev, alipohojiwa na waandishi wa habari wa kituo cha redio cha "Mwangwi wa Moscow" alisema, kifo cha Maskhadov sio tu kitasababisha wimbi jipya la kulipiza kisasi huko Chechnya bali pia nchini kote Russia. Ili kuandaa mapambano dhidi ya mashambuzi ya magaidi wa Chechen tarehe 9 usalama uliimarishwa ndani na nje ya mji wa Moscow, na maaskari wa doria pia wameongezeka, na tahadhari imeimarishwa katika subway, viwanja vya ndege na vituo vya garimoshi.
Wachambuzi wa Russia wanaona kuwa kwa sababu suala la Chechnya linaloka mbali kuanzia enzi ya kifalme ya Tsar, sasa linaibuka tena kutokana na nguvu za taifa za Urusi kufifia. Kwenye suala la Chechnya kuna tofauti za kikabila, na pia kuna athari za mazingira ya sasa ya ugaidi wa kimataifa. Kwa hiyo kifo cha Maskhadov hakimaanishi kumalizika kwa magaidi, suala la Chechnya halitaweza kutatuliwa kwa usiku mmoja tu. Hata hivyo, kifo cha Maskhadov pia ni hasara kwa jeshi haramu la Chechen, athari yake ipo, pengine magaidi wataanzisha mashambulizi mapya. Lakini kutokana na kifo cha Maskhadov matumaini ya amani na maisha ya utulivu ya watu wa Chechnya yamekuwa makubwa zaidi na nia ya Russia ya kulinda amani itakuwa imara zaidi.
Idhaa ya kiswahili 2005-03-10
|