Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-03-10 15:23:24    
Haki na Maslahi ya wafanyakazi wanawake wa China yahakikishwa siku hadi siku

cri

Kwa mujibu wa sheria za China, wanawake wana haki sawa na wanaume katika kupata kazi na mshahara. Lakini katika maisha ya kila siku, shughuli za kuingilia haki na maslahi ya wafanyakazi wanawake zinatokea hapa na pale. Ili kulinda haki na maslahi ya kina mama, shirikisho kuu la wafanyakazi la China lilianzisha kamati ya wafanyakazi wanawake, na idara husika zimechukua hatua maalum ili kulinda haki na maslahi ya wafanyakazi wanawake.

Katika miaka ya hivi karibuni, uchumi wa watu binafsi umekuwa ukiongezeka kwa haraka, na idadi ya wanawake wanaofanya kazi katika kampuni za watu binafsi inaongezeka siku hadi siku. Mji wa Nanjing, mkoani Jiangsu, mashariki mwa China, una kampuni nyingi za watu binafsi. Zamani kutokana na kutokuwa na mfumo kamili, yamewahi kutokea matukio ya kukiuka haki na maslahi ya wafanyakazi wanawake, kama vile ubaguzi wa kijinsia na kutoweza kulindwa haki zao wakati wanapopata uja uzito au kujifungua. Mwishoni mwa mwaka jana, mji wa Nanjing ulitunga makubaliano maalum ya kulinda haki na maslahi ya wafanyakazi wanawake, na kuwataka wanakampuni waahidi kulinda haki na maslahi ya kina mama hao.

Kampuni ya chakula na burudani ya Fenglinyage ni hoteli inayomilikiwa na mtu binafsi, zaidi ya asilimia 80 ya watumishi wa hoteli hiyo ni wanawake. Meneja mkuu wa kampuni hiyo Bi. Liang Yuqing alifahamisha kuwa, kampuni hiyo imesaini makubaliano maalum na kila mtumishi mwanamke.

"Makubaliano maalum yalitungwa kutokana na sheria ya kazi, sheria ya chama cha wafanyakazi, utaratibu wa kulinda kazi ya wafanyakazi wanawake na hali halisi ya kampuni yetu. Mambo muhimu yaliyomo katika makubaliano hayo ni kuwa, wanaume na wanawake wanafanya kazi ya aina moja na kupata mshahara sawa."

Bi. Ting Youti mwenye umri wa miaka 30 ni kiongozi wa idara inayopangisha vyumba vya hoteli, amefanya kazi kwenye hoteli hiyo kwa miaka mitatu. Alisema kuwa, kampuni hiyo iliwapatia watumishi wanawake wanaotoka nje ya mji sehemu ya kulala, katika siku za joto inawapatia vinywaji vya baridi, na huwakumbuka watumishi wake kwa kuwapatia keki ya kusherehekea siku ya kuzaliwa. Alisema:

"Sisi tunapata mshahara sawa na wanaume. Najisikia vizuri kufanya kazi hapa."

Imefahamika kuwa, kampuni nyingi za mkoa wa Jiangsu na mikoa mingine nchini China zinaichukulia kazi ya kulinda haki na maslahi ya wafanyakazi wanawake kama kazi muhimu ya kampuni.

Nchini China, wanawake wengi wanafanya kazi katika viwanda vya nguo, hivyo viwanda vya nguo vimekuwa sekta muhimu ya kulinda haki na maslahi ya wafanyakazi wanawake. Taarifa iliyotolewa na shirikisho la viwanda vya nguo la China ilisema kuwa, kampuni za nguo za China zote zinafuatilia kulinda haki na maslahi ya wafanyakazi wanawake, ambao hupewa likizo wakati wa uja uzito na kujifungua kutokana na vifungu vilivyowekwa kwenye sheria. Bi. Ma Xiai anafanya kazi katika kiwanda cha nguo cha mji wa Shijiazhuan mkoani Hebei, chama cha wafanyakazi cha kiwanda hicho kilisaini makubaliano maalum ya ushirikiano wa kulinda haki na maslahi ya wafanyakazi wanawake na kiwanda hicho. Mwaka jana, kiwanda hicho kilitenga kiasi fulani cha fedha kwa ajili ya kuwapima mwili wafanyakazi wanawake. Alisema:

"Sisi wafanyakazi wanawake baada ya kupata uja uzito kwa miezi saba tunaanza likizo ya uzazi, wakati huo tunapewa marupurupu na mshahara kama kawaida. Kila mwaka kiwanda hutupangia kupimwa mwili mara moja. Kufanya kazi katika kiwanda cha nguo tunatakiwa kutembea sana, kiwanda kina bafu, hivyo kila siku tunaweza kuoga kabla ya kurudi nyumbani."

Uchukuzi wa reli ni sekta nyingine inayofuatilia kulinda haki na maslahi ya wafanyakazi wanawake. Afya ya wafanyakazi wanawake wa sekta hiyo imeathirika kutokana na kutokuwa na hali nzuri ya tiba kwenye reli na kuweko katika hali ya kuhamahama kwa muda mrefu. Kwa hiyo chama cha wafanyakazi cha uchukuzi wa reli kimewakatia bima maalum ya afya kina mama. Licha ya kukata bima za maradhi makubwa, wafanyakazi wanawake pia wanaweza kukata bima za magonjwa ya wanawake.

Kupata uja uzito, kunyonyesha watoto na kipindi cha hedhi ni mambo maalum ya kimwili kwa kina mama, wanatakiwa kupewa matunzo maalum tofauti na kina baba, hivyo sheria husika za China zimeweka vifungu maalum vya kulinda haki na maslahi ya wafanyakazi wanawake. Shirikisho kuu la wafanyakazi la China limeunda idara ya wafanyakazi wanawake ili kulinda haki na maslahi yao maalum. Bi. Jinying kutoka idara hiyo alifahamisha:

"Katika miaka ya hivi karibuni, kazi ya kulinda haki na maslahi ya wafanyakazi wanawake nchini China imepata mafanikio kadhaa, hasa katika mashirika ya kitaifa ambako mfumo kamili umeundwa. Lakini katika makampuni kadhaa yasiyo ya umilikaji wa umma, haki na maslahi ya wafanyakazi wanawake bado hayawezi kuhakikishwa. Hivyo hivi sasa jukumu letu kubwa ni kulinda haki halisi na maslahi maalum ya wafanyakazi wanawake, kuzihimiza idara za kazi kukamilisha sheria na taratibu husika, na kuyasimamia makampuni yatekeleze sheria hizo ipasavyo."

Mwaka jana, Shirikisho kuu la wafanyakazi la China lilizitaka kampuni zilizowekezwa na watu kutoka nje kuunda chama cha wafanyakazi ili kuimarisha kazi ya kulinda haki na maslahi ya kina mama nchini China.

Idhaa ya kiswahili 2005-03-10