|
Ili kuadhimisha mwaka mmoja baada ya tukio la mlipuko wa Machi,11 huko Madrid, mkutano wa kimataifa kuhusu demokrasia, usalama na mapambano dhidi ya ugaidi unaolenga kutafuta mbinu za kupambana na ugaidi, ulifunguliwa jana huko Madrid, mji mkuu wa Hispania. Mwandalizi wa mkutano huo yaani mwenyekiti wa "Klabu ya Madrid", ambaye pia ni rais wa zamani wa Brazil Bw. Fernando Henrique Cardoso kwenye ufunguzi wa mkutano huo alisisitiza kuwa, njia sahihi ya kukabiliana na ugaidi ni kujitahidi kuimarisha uaminifu kati ya serikali na wananchi wa nchi mbalimbli, kuanzisha ushirikiano wa kimataifa na kuzuia matukio ya kigaidi yasitokee. Na kupitia njia hiyo tu, tutaweza kuondoa kikamilifu ugaidi.
Tukizungumzia ugaidi na mapambano dhidi ya ugaidi, watu hukumbuka Marekani. kwa kuwa Marekani si kama tu ilishambuliwa moja kwa moja katika tukio la Septemba 11, bali pia baada ya tukio hilo, nchi hiyo ilianzisha mashambulizi ya kijeshi dhidi ya Afghanistan na Iraq kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi. ingawa Marekani ilipata ushindi wa vita hivyo viwili kwa urahisi, lakini matukio ya kigaidi bado yanaongezeka na kuzidi kuwa ya utatanishi na kuenea zaidi duniani, kwa mfano tukio la utekaji nyara huko Beslan nchini Russia, mlipuko wa kigaidi kwenye kisiwa cha Bali nchini Indonesia, mlipuko mkubwa huko Madrid na matukio ya kuwateka nyara wageni nchini Iraq yaliyotokea mara kwa mara?? shughuli za kigaidi zinaenea hatua kwa hatua nje ya Marekani. Vita vya kupamabana na ugaidi vilivyoanzishwa na Marekani hatimaye vimewafanya watu wafikirie zaidi.
Katika miaka ya karibuni, ugaidi wa kimataifa umezidi kuvuruga dunia, na hali hiyo inahusiana na sera ya upande mmoja ya serikali ya Marekani. kwa mfano wa hali ya nchini Iraq, katika miaka miwili iliyopita, Marekani ilianzisha vita dhidi ya Iraq bila kujali upinzani wa nchi nyingine na bila kupata kibali kutoka kwa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa, kitendo hicho kwa kiwango fulani kilichochea migogoro ya kikabila na kidini nchini Iraq na kusaidia ugaidi. Aidha, kwa mujibu wa wahusika wa mlipuko wa Madrid, lengo la shambulizi hilo lilikuwa ni kupinga serikali ya Hispania kuunga mkono Marekani kuanzisha vita dhidi ya Iraq. Ndiyo kama Bw. Cardoso alivyosema, nchi yoyote lazima ziheshimu sheria ya kimataifa na haki za binadamu katika mapambano dhidi ya ugaidi na haipaswi kutatua suala hilo kwa kitendo cha upande mmoja kama vita dhidi ya Iraq. "sera ya upande mmoja inadhoofisha mfumo wa hivi sasa wa usalama wa kimataifa, na kufanya dunia iwe hatari zaidi."
Katika dunia ya leo, amani na maendeleo yanahitaji ushirikiano wa kimataifa, kutatua migogoro ya kikanda na kuondoa ugaidi pia kunahitaji ushirikiano wa kimataifa. Taasisi ya amani ya kimataifa ya Stockholm ilisisitiza kuwa, hali ya usalama ya kimataifa baada ya tukio la Septemba 11 imeonesha kuwa, majadiliano ya pande nyingi na ushirikiano wa kimataifa umekuwa mbinu mwafaka kabisa ya kuondoa tishio la kigaidi na kutatua migogoro ya kikanda. Rais Hu Jintao wa China kwenye mkutano usio rasmi wa viongozi wa nchi wanachama wa APEC mwezi Novemba mwaka jana pia alisisitiza kuwa, jumuiya ya kimataifa inapaswa kuchukua hatua imara za pamoja katika kupambana na ugaidi wa aina yote ndani ya mfumo wa Umoja wa Mataifa na kwenye msingi wa katiba ya Umoja wa Mataifa na kanuni husika za sheria ya kimataifa.
Idhaa ya Kiswahili 2005-03-11
|