|
Mlipuko wa mabomu ya kujiua ulitokea tarehe 10 kwenye msikiti mmoja wa madhehebu ya Shia huko Mosul, mji wa kaskazini mwa Iraq, na kusababisha vifo vya watu 47 nawengine zaidi 90 kujeruhiwa. Vyombo vya habari vinaona kuwa, katika kipindi ambacho makundi mbalimbali ya Iraq yanafanya mazungumzo kuhusu kuanzisha serikali mpya, na mkutano wa kwanza wa bunge la mpito utafanyika tarehe 16, duru jipya la mashambulizi ya mabavu limeanza nchini Iraq.
Katika siku za karibuni, makundi ya kijeshi ya Iraq yamelishambulia mara kwa mara jeshi la Marekani nchini Iraq na idara ya polisi ya Iraq, kuwaua askari na maafisa kisirisiri, na kuwateka nyara maofisa waandamizi wa serikali, na kuwashambulia mara kwa mara watu wakurd na waislamu wa madhehebu ya Shia, tarehe 10 wakamanda wawili wa polisi ya Baghdad walishambuliwa na kuuawa, mfanyakazi wa kituo cha televisheni cha Kurd alipigwa risasi na kuuawa, na mashambulizi ya mabomu ya kujiua yalitokea karibu na mkahawa mmoja wa Baghdad, na ofisa mwandamizi wa wizara ya mambo ya ndani ya Iraq Bw. Ghazi Mohammed Issa alipigwa risasi na kuuawa mjini Baghdad.
Inastahili kuzingatia kuwa, makundi ya kijeshi ya Iraq yameanza tena kuwateka nyara wageni wanaoshiriki kwenye ukarabati wa Iraq. Kundi la kijeshi "Islamic Army in Iraq" la madhehebu ya Suni ya Iraq tarehe 9 kwenye tovuti ya internet lilitoa video iliyoonesha kuwa kundi hilo liliwateka nyara maderewa wawili wa Sudan waliofanya kazi kwenye kampuni ya Uturuki.
Wachambuzi wanaona kuwa, mashambulizi hayo yalizushwa na makundi mawili. Kikundi kimoja ni kikundi cha kijeshi kilichoongozwa na kiongozi wa tatu wa kundi la Al-Qaeda Abu Musab al-Zarqawi, na kikundi kingine ni chakijeshi cha madhehebu ya Suni ya Iraq, baadhi yao wanapinga Marekani kuikalia Iraq na wengine hawajafurahishwa na madhehebu ya Suni kupata nafasi chache katika uchaguzi mkuu. Watu hao wana njama ya kuzuia mchakazo wa kisiasa kwa kuwashambulia wakurd na waislamu wa madhehebu ya Shia na kuathiri mchakato wa ukarabati wa Iraq kwa kuwatishia wageni wanaofanya kazi nchini Iraq. Kundi la Zarqawi siku zote limekuwa likivuruga hali ya Iraq kwa mashambulizi ya mabavu na kutaka kupata huruma na uungaji wa wananchi wa Iraq wanaopinga Marekani kwa kutumia njia ya kulishambulia jeshi la Marekani, maofisa, waislamu na wakurd wa madhehebu wanaoonekana kushirikiana na Marekani na kuchochea watu wenye msimamo mkali wa kimadhehebu wa nchi nyingine kujiunga kwenye kundi lao la ugaidi.
Vyombo vya habari vya Kiarabu vinaona kuwa, mkutano wa bunge la umma la mpito wa Iraq utaanza tarehe 16, makundi mbalimbali ya Iraq yametambua kuwa, ikiwa hayawezi kufikia makubaliano kuhusu kuanzisha serikali mpya, hali ya usalama ndani ya Iraq huenda itazidi kuwa mbaya.
Vyombo vya habari vya kiarabu pia vilionesha kuwa, mashambulizi ya mabavu nchini Iraq hayatasimama katika siku za karibuni, ili kurudisha usalama na utulivu wa Iraq, madhehebu ya Sunni yanapaswa kushiriki kwenye serikali mpya na mchakato wa kisiasa wa siku za baadaye, na baada ya serikali ya mpito kuundwa inapaswa kuongeza nguvu kwa askari polisi wa Iraq na kulinda kihalisi usalama wa Iraq na kuhakikisha sheria za Iraq zimetungwa bila matatizo na uchaguzi mkuu rasmi unafanyika kwa mpango, ili kurudisha utawala wa Iraq na kuondoa jeshi la Marekani nchini Iraq, huu ni usuluhishi wa kudumu wa kutimiza usalama wa Iraq.
Idhaa ya Kiswahili 2005-03-11
|