Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-03-14 16:42:47    
Mazungumzo kuhusu kuundwa kwa baraza la serikali nchini Iraq yanasuasua

cri

Chama cha Umoja wa Iraq (the United Iraqi Alliance) cha waumini wa madhehebu ya Shia kilichokuwa cha kwanza kwa idadi ya kura na Chama cha Muungano wa Vyama vya Kurd kilichokuwa cha pili kwa idadi ya kura katika uchaguzi mkuu tarehe 13 vilitangaza kuwa havikufikia makubaliano katika mazungumzo kuhusu kuundwa kwa baraza la serikali, pande mbili zilisema zitaendelea na mazungumzo hayo, na vitajitahidi kuafikiana kabla ya mkutano wa kwanza wa bunge la mpito utakaofanyika tarehe 16.

Kwa mujibu wa katiba ya muda ya Iraq, mkutano wa kwanza wa bunge la Iraq utamchagua spika na kuchagua kamati ya rais itakayoundwa na rais na makamu wa rais, na kamati hiyo itateua muungano wa vyama vya siasa kumteua waziri mkuu na kuunda baraza la serikali, na waziri mkuu na wajumbe wa baraza la serikali wataanza kazi rasmi baada ya kupitishwa na bunge. Chama cha Umoja wa Iraq kinachukua nafasi 140 kati ya nafasi 275 za bunge, ni chama kikubwa katika bunge la mpito, lakini waziri mkuu na wajumbe wa baraza la serikali waliotajwa lazima wapitishwe na theluthi mbili ya wabunge. Kwa hiyo kuna haja ya lazima kwa Chama cha Umoja wa Iraq kushirikiana na Chama cha Muungano wa Vyama vya Kurd, chama kikubwa cha pili kilichopata nafasi 75 katika bunge. Vyama hivi viwili vilianza mazungumzo kuanzia tarehe 10 na kimsingi vilikubaliana kuwa vitampendekeza kiongozi wa Chama cha Dawa cha Kiislamu katika Chama cha Umoja wa Iraq Bw. Jaafari awe waziri mkuu, na kiongozi wa Chama cha Umoja wa Wazalendo cha Kurdistan Bw. Talabani awe rais; na Iraq haitakuwa nchi ya Kiislamu; nafasi za makamu wa rais, spika wa bunge la mpito na nafasi moja ya uwaziri zitaachwa kwa ajili ya madhehebu ya Sunni.

Lakini vyama hivi viwili vinatofautiana katika masuala makubwa.

Kwanza, pande mbili zinatofautiana katika suala la utawala wa mji wa Kirkuk. Chama cha Muungano wa Vyama vya Kurd kinashikilia mji wa Kirkuk utawaliwe na Wakurd na uamuzi huo uandikwe kwenye katiba ya taifa. Habari zilizopatikana tarehe 10 zilisema kuwa pande mbili zimekubaliana kwamba baada ya serikali mpya kuundwa zitajadiliana suala la Wakurd kurudi Kirkuk na kufanya mazungumzo ya kuuweka mji huo ndani ya sehemu inayojitawala ya Kurd. Lakini msaidizi mwandamizi wa kiongozi wa roho wa madhehebu ya Shia tarehe 11 alipinga mapendekezo hayo. Alisema, suala la Kirkuk halimo katika mazungumzo ya kuundwa kwa baraza la serikali, na Chama cha Umoja wa Iraq hakikusema lolote kuhusu suala hilo.

Pili, Chama cha Muungano wa Vyama vya Kurd hakina imani na waziri mkuu anayependekezwa na Chama cha Umoja wa Iraq. Wakurd wanashikilia kuwa nchi ya Iraq itakuwa nchi yenye mfumo wa shirikisho, lakini chama kinachoongozwa na Jaafari ni cha watu wa madhehebu ya Shia na watu wenye asili ya Iran. Watu wa Kurd wana wasiwasi kuwa mfumo huo utatikiswa baada ya yeye kushika nafasi ya waziri mkuu. Ingawa kimsingi Chama cha Muungano wa Vyama vya Kurd kinakubali awe waziri mkuu lakini katika mazungumzo kuhusu kuundwa kwa baraza la serikali chama hicho kinatoa masharti mengi ya kumsumbua kwa makusudi. Wachambuzi wanaona kuwa sababu za kufanya hivyo kwa chama cha Kurd moja ni kwa ajili ya kuwapatia maslahi makubwa zaidi watu wa Kurd, nyingine ni kumsumbua kwa makusudi ili kurefusha mazungumzo na kumfanya atake kuacha nafasi hiyo kutokana na matatizo mengi.

Wakati pande mbili zinapofanya mazungumzo milipuko inaendelea kuzuka nchini Iraq. Vyombo vya habari vinaona kuwa katika mazingira kama hayo vyama hivi viwili vinatakiwa kuacha migongano na kuunda haraka baraza la serikali. Kama mazungumzo yakiendelea kwa muda mrefu na hata mwishowe yakivunjika, juhudi zote zilizofanywa na pande mbalimbali kwa ajili ya kuboresha hali zitakuwa bure na mchakato wa ujenzi mpya wa Iraq pia utaathirika vibaya.

Idhaa ya kiswahili 2005-03-14