Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-03-15 16:12:54    
Waziri mkuu wa China asisitiza juhudi zifanyike kujenga jamii yenye masikilizano

cri

Waziri mkuu wa China Wen Jiabao tarehe 5 alipotoa ripoti ya kazi ya serikali kwenye mkutano wa Bunge la umma la China alisisitiza kufanyika kwa juhudi katika kutatua masuala makubwa yanayohusiana moja kwa moja na maslahi ya wananchi, kulinda utulivu wa jamii na kuunda na kujenga jamii yenye masikilizano.

Waziri mkuu Wen Jiabao alisema kuwa, serikali ya China itaendelea kutekeleza sera ya kuongeza ajira na kuwasaidia wafanyakazi waliopunguzwa kazi kutoka kwenye mashirika ya kiserikali kupata ajira tena. Mwaka huu serikali kuu itatenga fedha za renminbi yuan bilioni 10.9 kusaidia kuongeza ajira, ambapo serikali za mitaa pia zitatenga fedha kuwasaidia watu waliopunguzwa kazi kupata ajira tena, kutoa maelekezo ya kutafuta ajira, kutoa mafunzo ya kazi na kutoa huduma kwa watu wanaotafuta ajira. Pia alisistiza kufanya vizuri kazi ya kutafuta ajira mijini, na kuimarisha ukaguzi kuhusu huduma za kazi.

Waziri mkuu Wen Jiabao alisema kuwa, China itaharakisha ujenzi wa mfumo wa huduma za jamii, kukamilisha utaratibu wa bima ya uzeeni kwa wafanyakazi wa mashirika, na kusukuma mbele kazi ya kuwahakikishia wafanyakazi waliopunguzwa kwenye mashirika wapate bima ya ukosefu wa ajira ili kupata uhakikisho wa kuishi maisha ya kiwango cha chini. Serikali ya China itapanua zaidi bima za jamii za uzeeni, ukosefu wa ajira, matibabu na kadhalika ili kuwashirikisha watu wengi zaidi kukata bima. Pia alisema serikali itakamilisha zaidi utaratibu wa kutoa fedha za kuhakikisha wakazi wasio na ajira mijini wanaweza kuishi maisha ya kiwango cha chini, katika sehemu yenye hali nzuri utaratibu huo utapanuliwa vijijini. Na serikali ya China itaendelea kuongeza mapato ya wakazi wa mijini na vijijini, hasa mapato ya kiwango cha wastani na cha chini.

Serikali ya China itasukuma mbele mageuzi ya utaratibu wa ugawaji wa mapato, itarekebisha na kukamilisha utaratibu wa ugawaji, kukamilisha utaratibu wa ushuru wa mapato ya watu, kuongeza marekebisho ya ugawaji wa mapato, kujitahidi kuondoa pengo kubwa la mapato kati ya watu , ili kuhimiza hali ya usawa kwenye jamii.

Pia waziri Mkuu alisema China itazingatia zaidi kazi ya kuwasaidia watu wenye matatizo ya kiuchumi wa mijini na vijijini kumudu maisha ya kiwango cha chini, na sehemu mbalimbali nchini zitaanzisha utaratibu wa utoaji misaada ya jamii kwa watu wenye matatizo maalum ya kiuchumi mijini na vijijini, ambapo itawasaidia kutatua matatizo halisi ya kupata matibabu, kupata makazi na kuwawezesha watoto wao kwenda shuleni. Pia itawasaidia watu wa sehemu maskini kuendeleza uzalishaji ili kuondokana na umaskini, na kufanya vizuri kazi ya kupunguza kodi za sehemu zitakazokumbwa na maafa na kuwasaidia watu watakaokumbwa na maafa katika uzalishaji na maisha .

Waziri mkuu Wen Jiabao alidhihirisha kuwa, China itafanya juhudi kusukuma mbele kwa hatua madhubuti mageuzi ya mfumo wa kisiasa, na kuimarisha ujenzi wa siasa ya demokrasia ya ujamaa. Serikali ya China itafanya vizuri kazi ya utungaji wa sheria, kuweka mkazo katika kuimarisha na kukamilisha utaratibu wa marekebisho na udhibiti wa uchumi, kutunga sheria kuhusu kukabiliana na matukio mbalimbali ya dharura, na kuhakikisha haki na maslahi halali ya wafanyakazi. Pia alisistiza kusukuma mbele mageuzi ya mfumo wa sheria na kulinda haki ya utekelezaji wa sheria, pamoja na haki na maslahi halali ya wanawake, watoto na walemavu. Pia alieleza kuwa serikali itazingatia kwa makini kazi ya kudumisha utulivu wa jamii, kupambana vikali na shughuli za uhalifu wa aina mbalimbali hasa uhalifu unaohatarisha usalama wa taifa, uhalifu wa mabavu na uhalifu wa makundi ya majambazi, na uhalifu wa dawa za kulevya ili kuhakikisha usalama wa wananchi. Aidha, China itaongeza uwezo wa kukabiliana na matukio ya dharura yanayohusiana na usalama wa umma, kupunguza hasara zinazoletwa na maafa ya kimaumbile, ajali na matukio ya dharura. Pia itaongeza mwamko wa usalama wa taifa, itaunda na kujenga mfumo wa kulinda usalama wa taifa.

Idhaa ya kiswahili 2005-03-15