Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-03-15 16:15:53    
Barua 0315

cri

Kwanza tuanze na barua ambazo kimsingi zina salamu na shukurani kwa Radio China kimataifa. Msikilizaji wetu James Muchelasia wa Shule ya msingi Kibisi sanduku la posta 628 Webuye Bungoma Kenya, ametuletea barua akisema kuwa amepata barua tulioyomtumia hivi karibuni, na anatushukuru sisi sote wafanyakazi wa idhaa ya Kiswahili ya Radio China kimataifa kwa uungaji mkono kwa wasikilizaji wote.

Msikilizaji wetu Ndeeche Mwanga Ommaala wa sanduku la posta 3385 Mombasa Kenya ametuletea barua akitoa salamu kwa watangazaji na wafanyakazi wa idhaa ya kiswahili ya Radio China kimataifa. Anasema wao huko Afrika ni wazima wanaendelea kuchapa kazi kama ilivyokuwa mwaka 2004. Anasema amezipokea barua zetu kwa hali nzuri na ya kupendeza, na sasa anasubiri kwa hamu sana tuchapishe jarida dogo la "Daraja la Urafiki".

Msikilizaji wetu Phillip B. Himu wa Ngunka Talaga sanduku la posta 525 Shinyanga Tanzania, ametuletea barua akiomba tumtumie jarida dogo la "Daraja la Urafiki". Anasema yeye akiwa msikilizaji wa Radio China kimataifa anaomba na yeye ajiunge katika usikilizaji wa idhaa ya Kiswahili ya Radio China kimataifa, na anaomba tumtumie majarida mbalimbali likiwemo jarida dogo alilotaja, ambalo tulitangaza kuwa tunafanya maandalizi ya kulichapisha kwa ajili ya wasikilizaji wetu.

Tunafurahi sana kufahamu kuwa wasikilizaji wetu wengi wanasubiri kwa hamu jarida hilo la "Daraja la Urafiki". Lakini kwa kuwa kazi ya kuliandaa na kuchapisha jarida hilo inahitaji muda, bado hatujakamilisha kazi zote zinazotakiwa. Hivi sasa tunaendelea na juhudi za kuliandaa jarida hilo, huku tukichapa kazi kila siku kwa ajili ya matangazo yetu ya kila siku. Hivyo tunataka wasikilizaji wetu msubiri na mvumilie hadi tutakapokamilisha kazi, ndipo mtakapoweza kupata jarida hilo. Vile vile bado tunaendelea kupokea maoni mbalimbali kutoka kwa wasikilizaji wetu, kuhusu baadhi ya mambo ambayo mnapenda yahusishwe kwenye jarida hilo

Msikilizaji Kilulu Kulwa wa Sanduku la posta 161 Bariadi Shinyanga Tanzania ametuletea barua akianza kwa salamu kwa watangazaji na wafanyakazi wote wa idhaa ya kiswahili ya radio China kimataifa. Anasema yeye ni mzima wa afya njema anaendelea tu na shughuli za kila siku za ujenzi wa taifa la Tanzania. Anatumai sisi sote hatujambo sana na tunaendelea kuchapa kazi ya kuwahudumia wasikilizaji wetu.

Anasema, mara nyingi amekuwa akituandikia barua kutueleza jinsi usikivu wa matangazo yetu yanayotoka moja kwa moja mjini Beijing , China kwa njia ya masafa mafupi ulivyo, na vile vile amekuwa akisikiliza idhaa ya Kiswahili ya Radio China Kimataifa kupitia kampuni ya KBC ya Nairobi, Kenya. Kenya ikiwa ni moja ya nchi za Afrika mashariki, wasikilizaji wa Radio China Kimataifa wanafurahi sana kusikiliza matangazo kutoka China kupitia KBC Nairobi.

Ingawa hali ya usikivu wa matangazo kutoka KBC kwa saa za mchana na jioni huko Tanzania si mzuri sana, lakini kwa ujumla wanafurahishwa na matangazo. Zamani katika miaka ya tisini KBC ilipokuwa inatumia masafa mafupi hasa katika matangazo yake ya jioni katika mitabendi 41, ilikuwa inasikika vizuri sana huko Shinyanga, lakini siku hizi KBC inatumia masafa ya kati, na hali ya hewa inapokuwa mbaya matangazo yanasikika kwa shida. Hivyo wanaomba wataalam na mafundi mitambo waendelee kujitahidi ili wasikilizaji wayapokee matangazo kwa njia iliyo bora zaidi.

Bwana Kulwa anasema, anaitumia fursa hii kutushukuru sana watayarishaji wa kipindi cha sanduku la barua na salamu na hasa mtangazaji maarufu wa idhaa ya Kiswahili ya Radio China Kimataifa mama Chen kwa kuendelea kuwaletea barua na makala motomoto katika kipindi cha sanduku la barua, na maoni ya kutoka kwa wasikilizaji wetu wa Idhaa ya Kiswahili. Kwa mfano mnamo jumapili ya tarehe 12 mwezi wa 12 mwaka 2004, tulinukuu na kusoma redioni barua zake mbili alizokuwa ametutumia kwa nyakati tofauti. Anasema kwa kweli alifurahi sana, na anaahidi kuendelea kusikiliza Radio China Kimataifa na kutoa maoni na mapendekezo yake mbalimbali ili kuboresha vipindi na matangazo yetu, ambayo yanaendelea kuwavutia na kuwachangamsha wasikilizaji wetu.

Anasema anapenda pia kutoa shukrani zake za dhati kwa wasikilizaji wenzake wa Kenya, Uganda, Rwanda, Umoja wa Falme za Kiarabu, Shelisheli na Tanzania ambao wamekuwa wakimkumbuka kwa kumtumia barua au kumtumia salamu kupita idhaa ya Kiswahili ya Radio China Kimataifa. Anawashukuru sana na anaamini kuwa wataendelea kuwasiliana sana na kukumbukana kupitia Radio China Kimataifa. Anamaliza kwa kuwatakia heri watangazaji na wasikilizaji wote wa Idhaa ya Kiswahili ya Radio China Kimataifa, furaha tele na mafanikio makubwa katika shughuli na maisha katika mwaka mpya wa 2005.

Msikilizaji wetu Daniel Chacha wa sanduku la posta 156 Tarime Mara Tanzania ametuletea barua akisema kuwa, anapenda kuipongeza Radio China kimataifa kuwathamini wasikilizaji wake kama wadau muhimu, kwa kuwatumia zawadi mbalimbali ambazo zimewafanya waendelee kuipenda Radio China kimataifa.

Anasema matumaini yake ni kuwa wasikilizaji wenzake wataendelea kutoa mapendekezo ya jumla kuhusu matangazo na vipindi mbalimbali vya Radio China kimataifa. Anaipongeza serikali ya China kuwa rafiki mzuri wa bara la Afrika, na hasa Tanzania. Pia anawapongeza wanasayansi wa China kuiletea China maendeleo ya kisayansi.

Anasema China imekuwa na setilaiti nyingi angani, ambapo imewawezesha wakulima wa mpunga kupata mbegu nzuri na bora ambazo zitaongeza mavuno, mapato na hata akiba ya chakula. Anaipongeza serikali ya China kuweka mikakati mizuri ya kudhibiti ongezeko la wagonjwa wa ukimwi.

China ingawa ina watu wengi lakini maambukizi ya ugonjwa wa ukimwi ni kidogo. Kati ya watu bilioni 1.3 ni watu laki nane na nusu ndio walioambukizwa gonjwa hili hatari ambalo halina dawa wala chanjo. Mwisho anasema anatumai kuwa tutaendelea kumtumia kadi za salamu, bahasha maalum na zawadi mbalimbali.

Idhaa ya kiswahili 2005-03-15