Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-03-16 16:00:08    
Mazungumzo kati ya makundi mbalimbali ya Palestina yafanyika mjini Cairo

cri

    Mazungumzo kati ya makundi mbalimbali ya Palestina yalifanyika tena tarehe 15 huko Cairo. Huu ni mkutano wa kwanza uliofanyika kati ya makundi baada ya Palestina kupata mamlaka ya utawala mwezi Januari. Wachambuzi wanasema kuwa, mkutano huo utasaidia umoja wa Palestina na kukabiliana na changamoto kwa pamoja.

    Viongozi na wawakilishi wa makundi makubwa 13 ya chama cha ukombozi wa Palestina wakiwemo viongozi wa Fatah, Hamas walihudhuria mkutano huo wa siku 5. Walijadili masuala ya kusimamisha vita na Israel na siasa nchini Palestina. Pande zote zitasaini Azimio la Cairo tarehe 19 wakati mkutano ukifungwa.

    Kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika tarehe 15, mwenyekiti wa mamlaka ya utawala wa Palestina Bw. Abbas alisema kuwa, katika wiki kadhaa zilizopita, makubaliano ya kusimamisha vita yaliyofikiwa kati ya mamlaka ya utawala wa Palestina na makundi mbalimbali ya Palestina yamepata mafanikio, na Wapalestina wameanza kujenga upya makazi yao yaliyoharibika. Bw. Abbas alisisitiza kuwa Palestina na Israel lazima zitekeleze ahadi zao. Alisema, kutokana na maslahi ya Wapalestina, Palestina inafuata makubaliano ya kusimamisha vita yaliyofikiwa kati yake na Israel, hivyo Palestina pia inaitaka Israel ibebe wajibu wake wa kuondoa jeshi lake kutoka sehemu za Palestina zilizokaliwa kutokana na vita ya mwaka 1967, na kufuata maazimio husika ya kimataifa, hususan azimio No. 194 la baraza la usalama kuhusu kutatua suala la wakimbizi wa Palestina.

    Bw. Abbas pia alizitaka makundi yote ya Palestina yaheshimiane na kufikia makubaliano katika masuala yote kwa njia ya mazungumzo na kujenga utaratibu wa utekelezaji na usimamizi. Alisema, chama cha ukombozi wa Palestina ni mwakilishi pekee halali wa Wapalestina, na pande zote za Palestina lazima ziimarishe umoja ndani ya chama hicho.

    Lakini, kuhusu suala la kusimamisha vita, hotuba ya waziri mkuu wa Israel Bw. Ariel Sharon iliyotolewa kabla ya hapo ilileta wingu jeusi kwa mkutano huo. Katika hotuba hiyo, Bw. Sharon alikanusha mpango wa Palestina kuhusu kusaini makubaliano kati ya Palestina na Israel. Bw. Sharon pia alieleza wazi kuwa, anapinga Bw. Abbas kufanya mazungumzo na makundi yenye siasa kali ya Palestina na kumhimiza Bw. Abbas kuchukua hatua kali kuvunja makundi hayo. Kutokana na msimamo mkali wa Bw. Sharon naibu waziri mkuu, ambaye pia ni waziri wa habari wa serikali ya Palestina Bw. Nabil Shaath alitoa taarifa akimlaani Bw. Sharon kuharibu hali ya kusimamisha vita kati ya Palestina na Israel. Mwakilishi wa Hamas anayehudhuria mkutano huo alisema kuwa, pande zote zinazohudhuria mkutano huo haziwezi kuafikiana kuhusu kusimamisha vita na Israel kwa muda mrefu, ikiwa Israel haitawaachia huru Wapalestina wote waliofungwa na kusimamisha kuvamia sehemu za Palestina, kwa hiyo Hamas itakubali tu "kudumisha hali ya utulivu kwa masharti".

    Kuhusu suala la ratiba ya siasa nchini Palestina, mwakilishi wa kundi la Fatah Bw. Zakaria al-Agha siku hiyo alisema kuwa, Fatah itatoa mpango wa kuanzisha muundo wa muda ambao pande zote za Palestina zinaweza kushiriki na kujadili mambo ya kisiasa kwa msingi wa pande zote za Palestina kushiriki kwenye uchaguzi wa kamati ya utungaji sheria ya Palestina. Alieleza kuwa, kama Hamas na al-Jihad zitashiriki kwenye kamati ya utungaji sheria kwa kupitia uchaguzi, basi zitaweza kuwa wanachama wa kamati ya utendaji wa chama cha ukombozi wa Palestina na kushiriki katika maamuzi ya masuala muhimu. Wakati huo, mwakilishi wa kamati ya siasa ya Hamas Bw. Mohammed Nazal alisema kuwa, Hamas itashiriki kwenye uchaguzi wa utungaji sheria wa Palestina tu, na haitashiriki katika serikali ya Palestina ya hivi sasa. Alisema, Hamas kushiriki uchaguzi wa utungaji sheria kuna lengo la "kusimamia serikali ya Palestina kuendesha mamlaka".

    Wachambuzi wanasema kuwa, baada ya mwenyekiti wa zamani wa mamlaka ya utawala wa Palestina Bw. Arafat kufariki dunia mwezi Novemba, mwaka jana, madaraka ya Palestina yamekabidhiwa kwa utulivu, na katika uongozi wa Bw. Abbas na juhudi za pande husika za jumuiya ya kimataifa, hali ya Palestina na Israel imekuwa tulivu. Serikali ya Bw. Abbas inatumai kwa kupitia mkutano huo wa Cairo kusawazisha misimamo ya Palestina ili kuanzisha tena mazungumzo kati ya Palestina na Israel.Wapalestina na jumuiya ya kimataifa inatumai pande zote zilizohudhuria mkutano huo zifuate maslahi ya kitaifa na kuaminiana ili mkutano huo kupata mafanikio.

Idhaa ya Kiswahili 2005-03-16