Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-03-16 16:22:51    
Madhumuni ya ziara ya Condoleezza Rice Asia Kusini

cri

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Bi. Condoleezza Rice tarehe 15 usiku aliwasili mjini New Delhi na kufanya ziara ya siku moja nchini India. Baadaye ataitembelea Pakistan. Baada ya kuteuliwa kuwa waziri wa mambo ya nje wa Marekani, Rice anaitembelea Asia kwa mara ya kwanza na kuweka lengo lake katika Asia Kusini, ambalo linaonesha lengo la Marekani kuhusu kufuatilia utulivu na kupata faida kubwa katika kanda ya Asia Kusini.

Kwanza, Marekani inatumai kuimarisha zaidi uhusiano wa kiwenzi na kimkakati kati yake na India kwa kupitia ziara hiyo ya Rice. India inayoendelea kiuchumi inaivutia sana Marekani. Tangu India na Marekani zilipoanzisha tena mazungumzo kuhusu uhusiano wa kiwenzi na kimkakati wa hatua ijayo mwaka jana, uhusiano kati ya nchi hizo mbili uliendelezwa kwa haraka. Mwaka jana thamani ya biashara kati ya nchi hizo mbili iliongezeka kwa asilimia 17. Marekani pia iliondoa marufuku ya kuiuzia India mfumo wa ulinzi wa makombora ya Patriot. Inawezekana kuwa India imekuwa soko la wafanyabiashara wa silaha wa Marekani.

Pili, Marekani inataka kuhimiza maafikiano kati ya India na Pakistan na kulinda utulivu wa hali ya Asia Kusini. Lengo la Marekani katika Asia Kusini ni kuepusha vita kati ya nchi hizo mbili, kufuatilia ufumbuzi wa mwisho wa mgogoro wa Kashmir na kuifanya sehemu ya Asia Kusini isiwe mahali pa kujificha kwa waislam wenye msimamo mkali. Mapambano kati ya India na Pakistan bila shaka yataathiri utekelezaji wa mkakati wa Marekani wa kupambana na ugaidi na kuharibu maslahi ya Marekani katika sehemu ya Asia Kusini. Kwa hiyo mada muhimu ya ziara ya Rice katika sehemu ya Asia Kusini ni kuzihimiza India na Pakistan zirekebishe zaidi uhusiano kati yao, ili kuzihakikishia nchi hizo mbili zishirikiane na Marekani katika vita vya kupambana na ugaidi.

Tatu, ni kuimarisha uhusiano kati ya Marekani na Pakistan katika vita vya kupambana na ugaidi. Baada ya kutokea tukio la tarehe 11 mwezi Septemba, Pakistan imeisaidia sana Marekani katika shughuli za kupambana na ugaidi duniani. Mwezi Machi mwaka 2004, Marekani ilitangaza kuwa Pakistan ni mshirika mwema wa Marekani nje ya NATO bila kujali malalamiko ya India. Kutokana na mkakati wa Marekani wa kupambana na ugaidi duniani, kuendeleza ushirikiano wa kupambana na ugaidi kati ya Marekani na Pakistan ni lengo lingine muhimu la ziara ya Rice katika sehemu Asia Kusini.

Lakini kwa kuwa suala la Kashmir halijatatuliwa hadi leo na bado kuna tofauti kadhaa kati ya Marekani na India, kwa hiyo si jambo rahisi kwa Marekani kufanikisha kikamilifu maslahi yake ya kimkakati katika kanda ya Asia Kusini.

Idhaa ya kiswahili 2005-03-16