Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-03-17 14:49:14    
Israel kuikabidhi Palestina mji wa Jericho

cri

Baada ya mazungumzo magumu ya wiki kadhaa, mwishowe mnamo tarehe 16 Israel iliikabidhi Palestina haki ya udhibiti wa usalama wa Jericho, mji wa kando ya magharibi ya Mto Jordan. Kuanzia hapo jeshi la Israel litaanza kuondoa kutoka kando ya magharibi ya Mto Jordan.

Adhuhuri ya tarehe 16, jeshi la Israel mjini Jericho liliteremsha bendera ya Israel, na jeshi la Palestina liliingia Jericho na kuanza kulinda usalama wa mji huo wa Palestina. Kutokana na makubaliano ya pande hizo mbili ya hivi sasa, Israel itaikabidhi Palestina mji wa Jericho na kijiji cha Al Awja, na kuondoa vituo viwili vya ukaguzi vya jeshi la Israel vilivyoko kaskazini na kaskazini-magharibi ya Jericho, hivyo maelfu ya Wapalestina wanaweza kuingia na kutoka kwenye mji wao kwa uhuru, lakini kwenye dungu kuna askari wa Israel kushika doria. Aidha, jeshi la Israel bado linadhibiti kituo cha ukaguzi kilichoko kusini mwa Jericho. Israel ilisema kuwa, kama Palestina inaweza kuthibitisha kuwa inaweza kudhibiti hali, basi jeshi la Israel litaondoa kituo hicho ndani ya mwezi mmoja. Hata hivyo hivi sasa jeshi la Israel pia limelegeza udhibiti, na Wapalestina wanakaguliwa wanapotoka nje tu forodhani.

Watu wa Jericho wanafurahi sana kuona jeshi la Israel linaondoka na jeshi la Palestina kuingia. Mwakilishi wa kwanza wa mazungumzo wa Palestina Bw. Saeb Erekat, ambaye anaishi mjini Jericho, alisema kuwa Palestina na Israel zinafanya juhudi ili kumaliza mgogoro. Alisema anatumai kuwa pande hizo mbili zitashauriana kwa amani na kuirudisha hali kama hali ya zamani kabla ya mgogoro wa Palestina na Israel kutokea.

Mji wa Jericho ni mji mdogo wenye watu elfu 40. Kwa kuwa mji huo uko mbali na makazi ya Wayahudi, hivyo kwa mara nyingi umekuwa "mji wa majaribio" wa kutuliza mgogoro wa Palestina na Israel. Mwaka 1994, Israel iliwahi kuchukua mji huo kuwa mji wa kwanza na kuanza mchakato wake wa "ardhi kwa amani". Mwezi uliopita viongozi wa Palestina na Israel kwenye mkutano wa wakuu wa Sharm el sheikh nchini Misri waliafikiana kuhusu suala la kukabidhi haki ya udhibiti wa usalama wa miji mitano ya kando ya magharibi ya Mto Jordan. Kwa kuwa hali ya mji wa Jericho ilikuwa tulivu katika miaka minne iliyopita, hivyo ulikuwa mji wa kwanza kukabidhiwa. Baadaye kazi ya ukabidhi wa mji wa Tulkarem pia itaanza. Miji mingine mitatu ni Qalqiliya, Bethlehem na Ramallah.

Kuhusu suala la haki ya udhibiti wa usalama wa miji hiyo ya Palestina, Palestina na Israel zilianzisha mazungumzo magumu. Kwa kuwa pande hizo mbili zinatofautiana kuhusu eneo la ukabidhi wa haki ya udhibiti katika vituo vya ukaguzi vya jeshi la Israel, barabara No. 90 na kijiji cha Al Awja, pamoja na tukio la mlipuko wa kujiua lililotokea huko Tel Aviv tarehe 25, mwezi Februari, hivyo mazungumzo yalikwama. Lakini hatimaye pande hizo mbili zimefikia makubaliano na hivyo kazi ya ukabidhi ikaweza kuendelea. Lakini kazi hiyo haitakuwa rahisi.

Wachambuzi wanasema kuwa, kazi ya ukabidhi wa mji wa Jericho kuendelea vizuri kutamsaidia Bw. Mahmoud Abbas kuimarisha heshima yake na hadhi yake ya uongozi, pia kutamsaidia kuhimiza sera zake za kuanzisha nchi kwa amani. Hivi sasa, makundi mbalimbali ya Palestina yanafanya mazungumzo huko Cairo kuhusu kusimamisha vita na suala la siasa nchini Palestina. Ukabidhi wa Jericho utaleta fursa nzuri kwa Bw. Abbas kuyashawishi makundi hayo ya Palestina kukubali kusimamisha vita na Israel na kuanzisha tena mchakato wa amani kati ya Palestina na Israel.

Idhaa ya kiswahili 2005-03-17