Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-03-17 20:35:35    
Hifadhi ya kimaumbile ya Xishuangbanna nchini China

cri

Jina la Xishuangbanna lilianza kutumika kuanzia mwaka 1570 katika Enzi ya Ming. Wakati huo serikali ya huko ililigawanya eneo hilo katika sehemu 12 ambazo kila sehemu iliitwa qiantian (eneo la utawala). Katika Lugha ya Wadai, "Xishuang" inamaanisha kumi na mbili, na "banna" inamaanisha qiantian. Jimbo linalojiendesha la kabila la Wadai la Xishuangbanna liko kusini mwa mkoa wa Yunnan na kupakana na Laos na Myanmar. Katika jimbo hilo lenye eneo la kilomita za mraba elfu 19.7 kuna watu wa Makabila ya Wadai, Wahani, Wabulang, Walahu, Wajinuo, Wawa, Wayi na Wahan. Jimbo hilo linajulikana kwa mandhari nzuri na maliasili nyingi. Mwaka 1983 eneo hilo liliwekwa na baraza la serikali ya China kwenye orodha ya vivutio maarufu vya kitalii nchini China.

Hifadhi ya kimaumbile ya Xishuangbannan iko kwenye jimbo hilo, na imechukua wilaya tatu yaani Jinghong, Mengla na Menghai. Hifadhi hiyo yenye eneo la hekta 241776 imegawanywa katika sehemu 5, ambazo zinasimamiwa na taasisi ya Mengla, taasisi ya Shangyong, taasisi ya Menglun, taasisi ya Mengyang na taasisi ya Mangao.

Hali ya kijiografia katika Hifadhi ya Xishuangbanna ni ya mabonde na milima midogomidogo. Mto Luosuo na Mto Nanla ambayo ni matawi ya Mto Lancang ni mito mirefu yenye matawi mengi na maji mengi. Kando ya mito hiyo miwili kuna misitu mikubwa ya aina ya ukanda wa joto. Sehemu yenye urefu mdogo kutoka usawa wa bahari iko kwenye sehemu ambako Mto Nanla unaingia kwenye mto Lancang, urefu wake ni mita 45.7 kutoka usawa wa bahari ; na sehemu yenye urefu mkubwa kutoka usawa wa bahari iko mlimani Nangong, ambako urefu kutoka usawa wa bahari ni mita 2007.

Hali ya hewa huko ni ya aina ya pepo za misimu ya ukanda wa joto wa kizio cha kaskazini. Wastani wa joto kwa mwaka mzima ni nyuzi 15.1 hadi nyuzi 21.7 sentigredi. Kwa ujumla kuna majira ya joto marefu na hakuna majira ya baridi. Katika mwezi wa Julai na Agosti mvua nyingi hunyesha, na katika mwezi Februari mvua ni kidogo. Tena mvua nyingi zaidi hunyesha katika sehemu ya mashariki kuliko magharibi.

Mazingira ya kimaumbile katika hifadhi ya Xishuangbanna ni mazuri. Misitu mikubwa na ya aina nyingi imetoa mazingira mazuri kwa maisha ya viumbe mbalimbali. Kuna vyakula vingi na mahali pazuri pa kujificha. Katika mfumo kamili wa viumbe, viumbe mbalimbali vinaishi pamoja kwa uwiano.

   

Sifa za maliasili ya wanyama pori ya hifadhi ya Xishuangbanna ni kuwa, katika sehemu hiyo kuna aina nyingi za viumbe, ambazo baadhi yake zinaishi katika peninsula ya Indochina tu; sehemu hiyo ni sehemu ambako kuna wanyama wengi zaidi wa aina za eneo la mashariki(Oriental realm) nchini China, viumbe vingi adimu na viumbe ambavyo viko katika habari ya kutoweka. Hivyo kuhifadhi maliasili ya wanyama pori huko ni muhimu sana.


1  2