|
Miaka miwili iliyopita, Marekani iliupuuza Umoja wa Mataifa kuanzisha vita dhidi ya Iraq, na kusababisha mgogoro mkubwa kabisa wa kimataifa baada ya kumalizika kwa vita baridi. Athari zilizoletwa na vita hivyo kwa mfumo wa uhusiano wa kimataifa na kanuni za sheria ya kimataifa zimedhihirika zaidi kutokana na wakati unavyopita.
Kwanza, vita vya Iraq vimeweka mfano mbaya wa kubadilisha hali ya utawala ya nchi yenye mamlaka kwa kutumia nguvu. Mwaka 2002 Marekani ilitoa mkakati wa "kuchukua hatua kabla ya kushambuliwa" kwenye ripoti yake ya usalama wa taifa, na kufanya jaribio kwanza katika vita vya Iraq. Hatari ya mkakati huo ni kuwa, Marekani inaweza kufanya mashambulizi kwa kisingizio kisichofuata ukweli wa mambo dhidi ya nchi zile zisizokuwa na tishio kwake, lakini haizipendi. Hali hiyo bila shaka italeta hofu na vurugu kwa jumuiya ya kimataifa.
Kiini cha kanuni za uhusiano wa kimataifa ni kuheshimu mamlaka na ukamilifu wa ardhi wa nchi nyingine, kutoshambulia na kutoingilia kati mambo ya ndani ya nchi nyingine. Vita vya Iraq vimewaonesha binadamu kuwa, Marekani inajaribu kuunda "utaratibu mpya" wa dunia kutokana na nia yake kwa kutegemea nguvu zake kubwa katika sekta ya kijeshi, sayansi na teknolojia na uchumi. Marekani imekuwa mchokozi na mharibifu mkubwa kabisa wa utaratibu wa kimataifa.
Pili, vita vya Iraq vimesababisha uhusiano kati ya Marekani na nchi za Ulaya kubadilika. Hii ni mara ya kwanza kwa uhusiano kati ya pande hizo mbili kuwa na wasiwasi na malumbano katika miaka zaidi ya 40 iliyopita. Vyombo vya habari vya Ulaya vinaona kuwa, nchi za Ulaya sasa zinafahamu kabisa sera ya Marekani ya "ubeberu mpya". Marekani inazigawa nchi za Ulaya kuwa "Ulaya kongwe" na "Ulaya Mpya" kwa kigezo chake cha kuiunga mkono katika vita ya Iraq, na kujaribu kuzuia mchakato wa umoja a Ulaya kwa kutumia migongano ya ndani ya nchi za Ulaya. Hayo yote yameongeza tofauti kati yao.
Tatu, vita vya Iraq vimeathiri uhusiano kati ya Marekani na dunia ya kiislamu. Japokuwa nchi za kiislamu zina misimamo tofauti kuhusu vita hivyo, lakini nchi nyingi zilipinga vita dhidi ya Iraq. Marekani hairidhishwi na mfumo wa kisiasa na itikadi za nchi za kiislamu, lengo lake kubwa la kuishambulia Iraq ni kueneza "mpango wake wa demokrasia katika sehemu ya mashariki ya kati". Marekani inatumai kuwa Iraq itakuwa mfano wa kuigwa kwa nchi nyingine za mashariki ya kati ili kueneza demokrasia yake katika sehemu hiyo. Isitoshe vita vya Iraq vimechochea hisia za uhasama wa waislamu duniani dhidi ya Marekani, na kusababisha kuongezeka tena kwa nguvu zenye siasa kali na magaidi.
Nne, kabla na baada ya vita vya Iraq, Marekani ilipuuza umuhimu wa Umoja wa Mataifa, na kuharibu vibaya heshima ya Umoja huo. Baadhi ya vyombo vya habari na wasomi wa Marekani hata walidai kuanzisha "muungano wa nchi za kidemokrasia" badala ya Umoja wa Mataifa. Mwishoni mwa mwaka jana, baada ya kutokea maafa ya tsunami katika bahari ya India, Marekani ilipendekeza kuundwa kwa "chombo cha kuongoza harakati ya kupambana na maafa" kinachoundwa na Marekani, Japan, Australia na India. Kusudi lake ni kujaribu kusukuma pembeni Umoja wa Mataifa. Hayo yote sio sadfa hata kidogo, bali ni kwamba Marekani inaona Umoja wa Mataifa na katiba ya umoja huo yenye kanuni za usawa kati ya nchi zenye mamlaka kama ni kikwazo chake cha kutaka kuitawala dunia nzima.
Japokuwa mfumo wa uhusiano wa kimataifa umeathirika vibaya kutokana na vita vya Iraq, lakini mwelekeo mkuu wa kuwa na ncha nyingi duniani bado unaendelea na hauwezi kuzuilika. Hivi karibuni, maendeleo ya jumuiya ya ushirikiano wa Shanghai, kuboreshwa kwa uhusiano kati ya China na India, juhudi za Umoja wa Ulaya za kuelekeza utatuzi wa suala la nyuklia la Iran, Russia kuipinga Marekani katika suala nyuklia la Iran, na nchi za Umoja wa Ulaya kutetea kuondoa vikwazo vya silaha dhidi ya China, hayo yote yameakisi maendeleo ya kuwa na ncha nyingi duniani.
Idhaa ya kiswahili 2005-03-18
|