Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-03-21 15:01:25    
Utabiri wa hali ya mkutano wa viongozi wa Umoja wa Ulaya

cri

Mkutano wa viongozi wa Umoja wa Ulaya utafanyika tarehe 22 na 23 mjini Bruselss, mji mkuu wa Ubelgiji. Mkutano huo utajadili mageuzi ya "Mkataba wa Utulivu na Maongezeko" na kupima utekelezaji wa "Mkakati wa Lisbon" ambao umepita nusu yake ya muda kabla ya kufikia lengo lililowekwa na mkakati huo, na kujadili maendeleo endelevu na hali ya siasa duniani. Vyombo vya habari vinaona kuwa mageuzi ya "Mkataba wa Utulivu na Maongezeko" ni mada itakayozungumziwa zaidi katika mkutano huo.

"Mkataba wa Utulivu na Maongezeko" ulitungwa mwaka 1997 kwa lengo la kutuliza thamani ya euro. Mkataba huo unataka nakisi ya bajeti kwa nchi zinazotumia euro isizidi asilimia 3 ya thamani za bidhaa zilizozalishwa za nchi hiyo, ama sivyo, nchi hiyo itatozwa faini kubwa. Lakini uchumi wa nchi zinazotumia euro unafufuka pole pole, hadi mwaka 2004 nchi za Ujerumani na Ufaransa zilikuwa na nakisi zaidi ya asilimia hiyo, na nchi nyingine pia zinakabiliwa na hatari ya kupita kiasi hicho. Kwa hiyo nchi za Ufaransa na Ujerumani zinataka kulegeza utelekezaji wa Mkataba huo na kutaka Umoja wa Ulaya ufikirie "hali isiyo ya kawaida", kwamba uchumi unaendelea pole pole na idadi ya watu wasio na ajira inaongezeka. Lakini nchi ndogo ambazo hazikuzidi kiwango cha nakisi hiyo zinataka Umoja huo utekeleze kabisa mkataba huo, na zinataka nchi kubwa na ndogo lazima ziwe sawa. Mawaziri wa fedha wa nchi zinazotumia euro wamewahi kujadiliana namna ya kufanya mageuzi ya mkataba huo mara nyingi, lakini hawakufikia makubaliano.

Ili kufanikisha mkutano huo, nchi mwenyekiti wa zamu Luxembourg tarehe 20 iliitisha mkutano wa mawaziri wa fedha wa nchi zinazotumia euro kwa makusudi ya kujadili mageuzi ya mkataba huo. Mwenyekiti wa kundi la euro, ambaye ni waziri mkuu wa Luxembourg Bw. Jean-Claude Juncker alitoa pendekezo la kurekebisha mkataba huo baada ya kuzingatia mapendekezo ya pande mbalimbali. Inasemekana kwamba pendekezo lake halikuorodhesha nchi zinazosamehewa kuzidi nakisi ya bajeti kwa sababu ya "hali isiyo ya kawaida" kama nchi kubwa zinavyotaka, lakini limerefusha muda kwa nchi hizo kudhibiti nakisi.

Mada nyingine ya mkutano huo ni kujadili na kupima utekelezaji wa "Mkakati wa Lisbon". Viongozi wa Umoja wa Ulaya waliweka "mkakati wa Lisbon" kwenye mkutano wao mwaka 2000 huko Lisbon, mji mkuu wa Ureno. Huu ni mkakati wa maendeleo ya miaka kumi na hivi sasa muda huo umepita nusu. Lengo lake ni kupita Marekani kabla ya mwaka 2010, na kuwa jumuyia kubwa ya uchumi yenye nguvu kubwa ya ushindani duniani. Lakini kutokana na hali ilivyokuwa katika miaka mitano iliyopita, lengo hilo halitafikiwa katika miaka mitano iliyobaki, kwa hiyo viongozi wa Umoja huo wanataka kupima utekelezaji wa mkakati huo na kuweka lengo la maendeleo la miaka mitano ijayo. Kabla ya hapo, mwezi Februari kamati ya Umoja wa Ulaya imetayarisha mkakati mpya wa maendeleo katika miaka mitano ijayo ili mkutano huo uujadili. Imefahamika kuwa mkakati huo mpya umeweka lengo la kuongezeka kwa thamani za bidhaa zilizozalishwa za kila nchi kwa asilimia 3 na kuongeza nafasi za ajira milioni 6. Kamati ya Umoja wa Ulaya inasema kuwa mkakati huo mpya ni majumlisho ya hali ya utekelezaji wa "Mkakati wa Lisbon" katika miaka mitano iliyopita na pia ni marekebisho ya "Mkakati wa Lisbon".

Licha ya mada hizo mbili mkutano huo pia utajadili bajeti ya Umoja wa Ulaya, na mchakato wa amani ya Mashariki ya Kati. Mawaziri wa mambo ya nje na wa fedha pia watahudhuria mkutano huo. Kutokana na ratiba, mawaziri wa mambo ya nje watajadili suala la pande nyingi duniani na mawaziri wa fedha watajadili suala la uchaguzi wa mkuu wa benki ya dunia.

Idhaa ya kiswahili 2005-03-21