Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-03-21 21:22:15    
Mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Nchi za Kiarabu waunga mkono kuanzisha tena pendekezo la amani

cri

Mkutano wa siku mbili wa mawaziri wa mambo ya nje na wawakilishi wa nchi 22 wanachama wa Umoja wa Nchi za Kiarabu tarehe 20 ulimalizika huko Algiers, mji mkuu wa Algeria, ambapo ulipitisha mswada mmoja kuunga mkono kuanzisha tena pendekezo la amani la waarabu.

Katika mswada huo mawaziri wa mambo ya nje na wajumbe wa nchi mbalimbali waliohudhuria mkutano huo walisisitiza kuwa, nchi za kiarabu zinatumai kuwa kutokana na misingi ya maazimio husika ya Umoja wa Mataifa na kuanzisha nchi huru ya Palestina, nchi za Mashariki ya Kati zinaweza kutimiza amani ya kudumu. Hivyo walikubali kuliwasilisha pendekezo la Jordan kuhusu kuanzisha tena "pendekezo la amani la waarabu", ambalo lilipitishwa kwenye mkutano wa wakuu uliofanyika Beirut mwaka 2002, kwenye mkutano wa wakuu wa nchi za kiarabu utakaofanyika hivi karibuni.

Watu hao pia walieleza kuwa wanaunga mkono Syria kurejesha uwanda wa juu wa Golan unaokaliwa na Israel, na kupinga Marekani kuiwekea Syria vikwazo vyovyote, na kuzitaka Marekani na Syria kutatua mgogoro kupitia mazungumzo ya kiujenzi. Walisisitiza kulinda mamlaka ya Lebanon katika mambo ya siasa, uchumi na usalama, na kupinga nchi za kigeni kuishinikiza Lebanon. Pia walikaribisha mafanikio ya uchaguzi mkuu wa Iraq uliofanyika tarehe 30, mwezi Januari na kusisitiza kuwa wataendelea kuunga mkono juhudi za kulinda mamlaka ya Iraq na ukamilifu wa ardhi yake.

Habari zinasema kuwa, mswada huo utawasilishwa kwenye mkutano wa 17 wa wakuu wa nchi za kiarabu. Kwa mujibu wa ratiba, mkutano huo utafanyika kuanzia tarehe 22 hadi tarehe 23.

Katibu mkuu wa Umoja wa Nchi za Kiarabu Bw. Amr Musa tarehe 20 baada ya mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje kumalizika alisema kuwa, mkutano wa wakuu wa nchi za kiarabu hautapokea pendekezo la Jordan lililotolewa kabla ya hapo kuhusu kurudisha uhusiano wa kawaida kati ya nchi za kiarabu na Israel. Alisema, pendekezo hilo limeacha msimamo wa "ardhi kwa amani", ambao ni msimamo wa jadi wa nchi za kiarabu. Alisema, "kama Israel itatekeleza ahadi zote, basi nchi zote za kiarabu zitarudisha uhusiano wa kawaida na Israel. Hatutasujudu katika suala hilo."

Katika wiki iliyopita, Jordan ilipendekeza mkutano wa wakuu wa nchi za kiarabu kujadili masuala ya kutatua migogoro kati ya nchi za kiarabu na Israel na kurudisha uhusiano wa kawaida, lakini pendekezo hilo halikutaja suala la kuitaka Israel iondoe jeshi lake kutoka sehemu za nchi za kiarabu. Hivyo pendekezo hilo lilipingwa na nchi nyingi za kiarabu. Baadaye Jordan ilirekebisha pendekezo hilo, na kusisitiza kuanzisha tena "pendekezo la amani la kiarabu" lililopitishwa na mkutano wa wakuu wa Beirut mwaka 2002.

Waziri wa mambo ya nje wa Algeria alifahamisha kuwa, mawaziri wa mambo ya nje na wawakilishi wa nchi mbalimbali pia waliafikiana kuhusu suala la kufanya mageuzi ndani ya Umoja wa Nchi za Kiarabu, ambayo ni pamoja na kurekebisha katiba ya Umoja wa Nchi za Kiarabu, kuzifanyia mageuzi idara za umoja huo, kuanzisha bunge na mahakama huru ya kiarabu na kurekebisha utaratibu wa upigaji kura wa umoja huo.

Idhaa ya Kiswahili 2005-03-21