Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-03-22 15:53:52    
China yajitahidi kuendeleza sekta ya hifadhi ya mazingira ya asili

cri

Katika miaka ya karibuni pamoja na maendeleo ya kasi ya uchumi wa China, rasilimali na mazingira ya asili yanakabiliwa na shinikizo kubwa. Hivyo serikali ya China imeimarisha udhibiti wa matumizi ya rasilimali na utoaji wa vitu vyenye uchafuzi huku ikihamasisha maendeleo ya sekta zinazotumia nishati kidogo na kutoa vitu visivyo na uchafuzi vingi zikiwa ni pamoja na ya huduma na ya teknolojia ya kiwango cha juu, ambapo sekta ya hifadhi ya mazingira ya asili inayotoa vitu vya mahitaji kwa shughuli za hifadhi ya mazingira na teknolojia inayohitajika imepata nafasi kubwa ya maendeleo nchini China.

Naibu mkurugenzi wa jumuiya ya sekta ya uzalishaji ya hifadhi ya mazingira ya China bibi Chen Shangqin alimwambia mwandishi wetu wa habari kuwa China ilianza kuendeleza sekta ya hifadhi ya mazingira tokea mwanzoni mwa miaka ya 70 ya karne iliyopita, baada ya kuendelezwa kwa miaka zaidi ya 30, umejengwa mfumo wa uzalishaji bidhaa za aina mbalimbali za hifadhi ya mazingira. Hivi sasa nchini China kuna viwanda na kampuni zaidi ya elfu 20 za kuzalisha bidhaa zinazohifadhi mazingira, ambazo thamani yake imezidi Yuan za Renminbi bilioni 230 kwa mwaka, tena inaongezeka kwa 15% kila mwaka. Bibi Chen Shangqin alipoeleza chanzo cha maendeleo ya kasi ya sekta ya hifadhi ya mazingira alisema,

"Maelekezo, uungaji mkono na uhimizaji wa serikali ni vitu vilivyochangia sana maendeleo ya uzalishaji wa sekta ya hifadhi ya mazingira. Serikali iliweka mpango wa maendeleo ya sekta ya hifadhi ya mazingira, kigezo na kiwango cha teknolojia husika, ambavyo vimeelekeza maendeleo ya sekta ya uzalishaji ya hifadhi ya mazingira pamoja na kuboresha utaratibu wa sekta hiyo. Aidha, pamoja na maendeleo ya jamii, watu wanazingatia sana ubora wa mazingira, hivyo shughuli za sekta ya hifadhi ya mazingira zimeendelezwa kwa mfululizo."

Kampuni ya hifadhi ya mazingira ya Ziguang ya chuo kikuu cha Qinghua ni moja ya kampuni kubwa za hifadhi ya mazingira hapa nchini, ambayo inatoa huduma ya elimu kuhusu udhibiti wa vitu vyenye uchafuzi na hifadhi ya mazingira pamoja na kufanya ushirikiano wa kibiashara katika hifadhi ya mazingira. Hivi sasa thamani ya mali ya kampuni hiyo imezidi Yuan bilioni 1.1 na pato lake limezidi Yuan milioni 100 kwa mwaka. Mkurugenzi mkuu wa kampuni hiyo Bw. Li Xingwen alisema kuwa katika muda wa zaidi ya miaka mitatu tangu kampuni hiyo ianzishwe, imekuwa na ushirikiano katika mambo ya teknolojia na fedha pamoja na taasisi za utafiti wa huduma za miji maarufu ya nchini na ya nchi za nje pamoja na kampuni maarufu duniani kutokana na hali yake bora ya wataalamu na teknolojia. Hadi hivi sasa kampuni hiyo imetoa taarifa ya tathmini juu ya mazingira ya miradi zaidi ya 600 pamoja na udhibiti wa vitu vyenye uchafuzi vilivyotolewa na viwanda zaidi ya 400. Aliongeza kuwa hivi sasa kampuni yao inakusanya rasilimali zake na kujiendeleza katika shughuli mpya za hifadhi ya mazingira. Alisema,

"Tukitaka kujiendeleza na kufikia kiwango cha juu, hatuna budi kuwa na lengo kubwa. Endapo tunatulia katika shughuli za kusafisha maji machafu na uteketezaji wa takataka, basi hatutakuwa na mafanikio makubwa. Hivi sasa sisi tunashughulikia ujenzi wa eneo la upatanishi wa viumbe lenye hekta zaidi ya 330 katika mji wa Qingdao ambao uko katika sehemu ya mashariki ya China. Eneo hilo ni kama uwanja wa maendeleo ya kampuni za hifadhi ya mazingira za nchi mbalimbali, ambapo tutaweza kuwa na ushirikiano na kunufaishana kutokana na nafasi inayoletwa na maendeleo ya sekta ya hifadhi ya mazingira ya asili ya China."

Habari zinasema kuwa hivi sasa nchini China kuna kampuni nyingi za hifadhi ya mazingira kama kampuni ya Ziguang, baadhi ya sehemu zimechukulia kazi za hifadhi ya mazingira kuwa nguvu kuu ya maendeleo ya uchumi wake. Katika miaka ya karibuni, China ilikuwa na ushirikiano na mashirika na wawekezaji husika duniani katika usafishaji na uteketezaji wa maji machafu na takataka za mijini, udhibiti wa hewa chafu zinazotolewa na magari na kutoa habari kuhusu hifadhi ya mazingira, wakati kampuni maarufu zaidi ya mia moja duniani za hifadhi ya mazingira zimeingia katika soko la hifadhi ya mazingira nchini China.

Pamoja na maendeleo ya soko la hifadhi ya mazingira, wanamji pia wamenufaika. Mfano mmoja ni kuhusu mabadiliko ya matumizi ya maji ya kusafishia magari mjini Beijing. Beijing ni mji wenye upungufu mkubwa wa maji, wastani wa maji kwa kila mtu bado haujafikia mita za ujazo 300, kiasi ambacho ni sehemu 1 kwa 30 ya wastani wa maji kwa kila mtu kwa mwaka duniani. Ili kupunguza matumzi ya maji, mwaka jana bei ya kusafisha gari moja mjini Beijing ilipanda mara mbili kuliko zamani. Lakini wakazi wa Beijing wamenufaika na kupunguzwa gharama ya kusafisha magari kutokana na kutumika kwa maji machafu yaliyosafishwa na kampuni ya hifadhi ya mazingira. Meneja wa kituo cha kusafisha magari Bw. Liu alisema,

"Kusafisha magari kwa kutumia maji ya kunywa ni gharama kubwa kuliko kutumia maji yaliyokwishatumika na kusafishwa. Tani moja ya maji yaliyokwishatumika na kusafishwa ni Yuan 10 ikilinganishwa na Yuan 40 kwa maji safi."

Habari zinasema kuwa katika miaka mitano ijayo serikali itatenga Yuan bilioni 900 katika hifadhi ya mazingira, hali ambayo ni nafasi kubwa kwa maendeleo ya sekta ya hifadhi ya mazingira.

Idhaa ya kiswahili 2005-03-22