Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-03-22 20:29:43    
Mageuzi ya Umoja wa Mataifa

cri

Tarehe 21 katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Kofi Annan aliwasilisha ripoti kuhusu mageuzi ya umoja huo iitwayo "Uhuru mkubwa zaidi kwa kuwapatia watu wote maendeleo, usalama na haki za binadamu" kwenye baraza kuu la 59 la Umoja wa Mataifa, na kuzitaka nchi mbalimbali kukubali mapendekezo yaliyotolewa kwenye ripoti hiyo kuhusu maendeleo, usalama, haki za binadamu na mageuzi ya Umoja wa Mataifa. Ripoti hiyo inasisitiza kuwa kufanikiwa au kutofanikiwa kwa mageuzi ya Umoja wa Mataifa kunategemea mageuzi ya Baraza la Usalama, na ripoti hiyo pia inazihimiza nchi mbalimbali kuzingatia mipango miwili kuhusu kupanua baraza hilo iliyotolewa na kikundi cha watu mashuhuri wa ngazi ya juu kinachoshughulikia mageuzi ya Umoja wa Mataifa.

Baada ya vita baridi, suala la mageuzi ya Umoja wa Mataifa liliwekwa kwenye ratiba. Mageuzi ya Baraza la Usalama ni muhimu zaidi katika mageuzi ya umoja huo. Mwaka 1993, baraza kuu la 48 la Umoja wa Mataifa liliamua kuunda kikundi maalum kinachoshughulikia mageuzi ya umoja huo. Bw. Annan alianza kushughulikia mageuzi hayo baada ya kushika cheo cha katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa mwezi Januari mwaka 1997. Mwezi Machi, mwenyekiti wa baraza kuu la 51 la Umoja wa Mataifa Bw. Ismail Razali ambaye pia alikuwa mwenyekiti wa kikundi kinachoshughulikia mageuzi ya Umoja wa Mataifa alitoa mpango wa mageuzi akipendekeza kuongeza nchi wajumbe watano wa kudumu wasio na haki ya kupiga kura ya turufu na nchi wajumbe wanne wasio wa kudumu kwenye Baraza la Usalama. Mwezi Julai mwaka huu, Bw. Annan alitoa mpango kamili wa mageuzi kwenye baraza kuu la 51 la Umoja wa Mataifa. Mpango huo ni pamoja na kupunguza mashirika, kuinua uwezo wa kufanya kazi, kupunguza matumizi ya fedha na kutumia fedha zilizopunguzwa kuzisaidia nchi zinazoendelea kukuza uchumi.

Mabaraza ya Umoja wa Mataifa yalikuwa yakijadili suala hilo katika miaka mingi iliyopita, lakini kwa sababu masuala ya kupanua baraza la Usalama, kuongeza nchi wajumbe wa kudumu na haki ya kupiga kura ya turufu yanahusiana na maslahi ya pande nyingi, nchi wajumbe zilikuwa na maoni tofauti kuhusu mpango wa mageuzi, na hazikuweza kuafikiana.

Mwezi Novemba mwaka 2003, Bw. Kofi Annan alikitaka kikundi cha watu mashuhuri wa ngazi ya juu kufanya utafiti kuhusu masuala makubwa yakiwemo changamoto zinazoikabili amani na usalama wa dunia, na mageuzi ya Umoja wa Mataifa. Mwezi Desemba mwaka 2004, kikundi hicho kilitoa mipango miwili kuhusu kupanua Baraza la Usalama. Mpango wa kwanza ni kuongeza nchi wajumbe 6 wa kudumu wasio na haki ya kupiga kura ya turufu ambazo mbili ni nchi za Afrika, mbili ni nchi za Asia, na nyingine mbili ni nchi za Ulaya na Amerika, na kuongeza nchi wajumbe watatu wasio wa kudumu,. Pili ni kuongeza nchi wajumbe 8 wa nusu kudumu ambazo Afrika, Asia, Ulaya na Amerika kila moja itapata nafasi mbili, na kuongeza nchi mjumbe mmoja asiye wa kudumu.

India, Brazil, Ujerumani na Japan zimeanza kugombea uananchama wa kudumu kwenye Baraza la Usalama. Mwaka jana zilitoa taarifa ya pamoja zikitangaza kuwa, zitaungana mkono kugombea nafasi hiyo. Aidha, Nigeria, Afrika ya Kusini na Misri pia zinataka kuwa nchi wananchama wa baraza hilo zikiziwakilisha nchi za Afrika. Mwezi Februari mwaka huu, mawaziri wa mambo ya nje wa nchi 15 za Afrika zilipofanya mkutano zilikubali kuwa, katika mageuzi ya Umoja wa Mataifa, nchi za Afrika zina haki ya kupata nafasi mbili za ujumbe wa kudumu kwenye Baraza la Usalama. Indonesia pia inagombea nafasi hiyo.

Idhaa ya Kiswahili 2005-03-22