|
Tokea bunge la wilaya ya Shimane ya Japan kupitisha azimio la tarehe ya kuadhimisha kurudishwa kwa mamlaka ya kisiwa cha Dokdo, serikali na wananchi wa Korea Kusini walichukua hatua mbalimbali kujibu azimio hilo. Je, "dhoruba ya kisiwa cha Dokdo" itasababisha uhusiano wa nchi hizo mbili kuwa mbaya?
Wachambuzi wanaona kuwa ingawa msukosuko umetokea katika uhusiano wa nchi hizo mbili, lakini msukosuko huo hautaathiri sana uhusiano wa nchi hizo.
Kwanza, ingawa msimamo wa serikali ya Korea Kusini kuhusu mamlaka ya Dokdo ni mkali, lakini msimamo huo unadhibitiwa kwa kiasi cha kufaa. Tokea bunge la wilaya ya Shmane ya Japan kupitisha "siku ya maadhimisho ya Dokdo" serikali ya Korea Kusini imetoa kanuni nyingi mpya kuhusu uhusiano na Japan ambazo zimeshutumu vikali jinsi Japan inavyoshughulikia suala la kisiwa cha Dokdo na vitabu vya kufundishia vinavyopotosha historia, lakini huku ikiwataka wananchi wajizuie hasira na wasichukue hatua za kudhalilisha heshima na adabu kupita kiasi. Waziri wa mambo ya nje na biashara ya Korea Kusini Bw. Ban ki-moon hivi karibuni amesema kuwa Korea Kusini haitavunja "mkataba wa uvuvi wa Korea Kusini na Japan" kutokana na suala la kisiwa cha Dokdo. Ili kupunguza athari ya suala la Dokdo na suala la historia, rais wa Korea Kusini Roh moo-hyun siku za karibuni amesema, serikali ya Korea Kusini inapaswa kuanzisha idara maalumu ili kushughulikia uhusiano na Japan.
Pili, tokea rais Roh moo-hyun kushika madaraka, anajitahidi kuendeleza uhusiano na Japan. Mwanzoni baada ya kushika madaraka, alikuwa akitetea kupunguza uzito wa suala la kupotosha historia, kwa sababu Korea Kusini ilikuwa ikidhibiti kisiwa cha Dokdo, alitetea kukwepa "vita vya maneno" na Japan. Katika nusu ya pili ya mwaka uliopita, viongozi wa nchi mbili walikutana nchini Korea Kusini, mawazo ya namna moja yaliyopatikana katika mazungumzo yao yameonesha dhamira ya Korea Kusini kutaka kuendeleza uhusiano na Japan. Huu ni mwaka wa 40 tokea Korea Kusini na Japan ziwekeane uhusiano wa kibalozi, na pia ni maadhimisho ya miaka 60 tokea penisula ya Korea iondoe utawala wa kikoloni wa Japan. Katika mwaka kama huo, wananchi wa Korea Kusini wanazingatia sana jinsi serikali inavyoshughulikia uhusiano na Japan.
Tatu, uhusiano mzuri kati ya Korea Kusini na Japan unanufaisha Korea Kusini. Korea Kusini na Japan ni nchi zinazopakana, uhusiano ukishughulikiwa kwa busara unasaidia Korea Kusini kuimarisha mazingira bora na nchi nyingine. Hivi sasa suala la silaha ya nyuklia la penisula ya Korea limekwama, kuhusu suala hilo Korea Kusini inahitaji kuimarisha ushirikiano na Japan. Zaidi ya hayo uhusiano wa kibiashara kati ya nchi hizo mbili ni wa karibu sana, Japan ni mwenzi mkubwa wa kibiashara wa Korea Kusini, lakini kutokana na tofauti ya maendeleo ya kiuchumi, Korea Kusini ni dhaifu, inataka kuimarisha uchumi wake kwa kutegemea uhusiano mzuri na Japan.
Licha ya yote yaliyotajwa hapa juu, serikali ya sasa ya Korea Kusini inataka kupiga hatua katika mambo ya diplomasia, Bw. Roh moo-hyun anasifu sana mchango wa Ufaransa katika Umoja wa Ulaya, akitamani nchi yake pia iwe kama Ufaransa katika Asia ya Kaskazini Mashariki na kutoa mchango wake katika ustawi wa kiuchumi na amani katika Asia ya Kaskazini Mashariki. Korea Kusini haitakuwa nchi yenye msimamo mkali kama Marekani na Japani katika kanda zao, bali inatumai kutoa mchango wake katika Asia ya Kaskazini Mashariki. Kutokana na mazingira hayo, uhusiano kati ya Korea Kusini na Japan utaendelea kwa makini.
Idhaa ya kiswahili 2005-03-23
|