Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-03-23 15:04:52    
Nchi mbalimbali zaunga mkono ripoti ya Annan kuhusu mageuzi ya Umoja wa Mataifa

cri
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Kofi Annan tarehe 21 alilikabidhi baraza kuu la 59 la Umoja wa Mataifa ripoti ya mageuzi ya kufufua Umoja wa Mataifa. Ripoti hiyo imeleta maoni tofauti katika jumuiya ya kimataifa, nchi nyingi zinaeleza kuunga mkono mpango wa mageuzi wa Bw. Annan, lakini nchi kadhaa bado zina maoni tofauti kuhusu masuala makubwa kadhaa yaliyomo kwenye ripoti hiyo.

Nchi nyingi zinaona kuwa, mazingira ya kimataifa ya Umoja wa Mataifa yana tofauti kubwa na yale ya miaka 60 iliyopita, hivyo kuna haja ya kufanya mageuzi. Hasa katika miaka ya hivi karibuni, sifa na heshima ya Umoja wa Mataifa imeathirika kutokana na vita vya Iraq na kesi ya ufisadi katika "mpango wa chakula kwa mafuta" na mambo mengine, hivyo mageuzi ni muhimu katika kurudisha heshima ya Umoja wa mataifa.

Jumuiya ya kimataifa kwa kimsingi inaunga mkono ripoti hiyo. Marekani, Uingereza, Canada, Russia, Ufaransa na Ujerumani zote zinapongeza ripoti hiyo, na zinaeleza kuunga mkono mpango huo wa mageuzi. Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya China Bwana Liu Jianchao alisema kuwa, China inamsifu Bw. Annan kwa juhudi zake alizofanya katika kuhimiza uhusiano wa pande nyingi na demokrasia katika uhusiano wa kimataifa, China inafanya uchunguzi kuhusu ripoti ya Annan na kufanya maingiliano na mashauriano na pande mbalimbali, ili kusukuma mbele kwa pamoja mchakato wa mageuzi ya Umoja wa Mataifa.

Lakini bado kuna maoni tofauti katika masuala kadhaa nyeti kama vile upanuaji wa baraza la usalama, suala la kutumia nguvu, kuunda baraza la haki za binadamu na jinsi ya kuwa na tafsiri sahihi kuhusu ugaidi.

Kuhusu suala la upanuaji wa baraza la usalama, mgongano kati ya "umoja wa nchi nne wa kuomba kuteuliwa kuwa ujumbe wa kudumu wa baraza la usalama" ulioundwa na Brazil, Ujerumani, India na Japan na "klabu ya kahawa" inayozipinga nchi hizo nne bado upo, lakini nchi hizo nne zimebadili msimamo wao wa kushikilia kuwa na haki ya kupiga kura za veto kama zilivyoshikilia. Tarehe 22 nchi hizo nne zilitoa taarifa kuunga mkono ripoti ya Annan. Hali hiyo imeonesha kuwa, miswada miwili iliyotolewa na Annan kuhusu kupanuliwa kwa baraza la usalama yote imekubalika, jambo litakalofanywa ni kuchagua mswada upi.

Kuhusu suala la kutumia nguvu, ripoti ya Annan inasisitiza kuwa, baraza la usalama ni kiini cha kutoa uamuzi, nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa zinapaswa kufuata kwa makini hatua zilizowekwa katika suala hilo, haziwezi kutumia nguvu bila ya kupewa idhini na baraza la usalama. Lakini pendekezo hilo linapingwa na Marekani inayodai mkakati wa "kuchukua hatua kabla ya kushambuliwa".

Kuhusu pendekezo la kuondoa kamati ya haki za binadamu ya sasa na kuunda baraza la haki za binadamu lenye kiwango kidogo zaidi lakini lenye utaalamu zaidi. Bw. Annan anaona kuwa, nchi za baraza hilo zinahitaji kuungwa mkono na theluthi ya nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa. Lakini nchi zilizopinga pendekezo hilo zinaona kuwa, kuunda baraza la haki za binadamu ni matokeo ya shinikizo la Marekani, pia zina wasiwasi kuwa, baraza hilo huenda litakuwa chombo cha nchi za magharibi kuingilia kati mambo ya ndani ya nchi zinazoendelea kwa kisingizio cha haki za binadamu.

Kuhusu kubaini tafsiri sahihi kuhusu ugaidi pia kuna maoni tofauti. Katika kipindi kirefu kilichopita, hakuna mkataba wa kimataifa unaohusu vifo na majeruhi kwa raia. Katika miaka ya hivi karibuni, kutokana na ukweli wa mambo, watu wengi zaidi wasiokuwa na hatia wameathirika na vitendo vya uhasama, hivyo Umoja wa Mataifa unatetea kubaini haraka iwezekanavyo tafsiri ya ugaidi, ili kusaini mkataba husika wa kimataifa. Lakini baadhi ya nchi zinasisitiza kuwa, wale waliothibitshwa kuwa "magaidi" na upande mmoja huenda ni "wapigania uhuru" kwa upande mwingine. Ili kukwepa migongano, Bw. Annan katika ripoti yake alithibitisha "ugaidi" kuwa "kitendo chochote kinachofanywa na mtendaji kwa ajili ya kuonesha malalamiko yake kwa njia ya kuhatarisha kwa makusudi maisha ya raia". Lakini baadhi ya nchi bado haziridhiki na tafsiri hiyo.

Hivi sasa lengo na ratiba ya mageuzi ya Umoja wa Mataifa zimethibitishwa, lakini kama nchi wanachama zinaweza kuondoa tofauti na kuafikiana kuhusu masuala hayo au la itahusiana na kama ripoti hiyo itaweza kupitishwa au la katika mkutano wa wakuu wa Umoja wa Mataifa unaotarajia kufanyika mwezi Septemba mwaka huu, na vilevile itahusiana na kufaulu kwa mageuzi yenyewe au la.

Idhaa ya kiswahili 2005-03-23