|
Mkutano wa 17 wa wakuu wa nchi wanachama wa Umoja wa nchi za Kiarabu uliofanyika kwa siku mbili jana umefungwa huko Algiers, mji mkuu wa Algeria. Ingawa wakuu wa nchi 13 tu kati ya nchi 22 wanachama wa Umoja huo walihudhuria mkutano huo, lakini mkutano huo pia ulipata maendeleo kadhaa katika suala la amani ya Mashariki ya Kati na mageuzi ya miundo ya jumuiya hiyo.
Mkutano huo ulizingatia sana suala la amani ya Mashariki ya Kati, hasa amani ya Israel na Palestina. Rais Muammar Al-Kadhafi wa Libya aliainisha kuwa, hali isiyo ya haki ni chanzo cha kuenea kwa ugaidi wa kimataifa, na inapaswa kutatua suala la Palestina kwanza ili kuondoa ugaidi wa kimataifa.
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Kofi Annan aliyealikwa kuhudhuria mkutano huo alitaka mgogoro kati ya Israel na Palestina utatuliwe kwa amani. Alisisitiza kuwa, mazugumzo ya amani ni njia mwafaka ya kutatua suala hilo, na kutumia nguvu katika kutatua suala hilo, kunaweza tu kuongeza mateso kwa watu wa nchi hizo mbili.
Azimio la Algiers lililopitishwa siku hiyo limesisitiza kuwa, amani bado ni chaguo cha kimkakati kwa nchi za kiarabu. Ili kusukuma mbele mchakato wa amani ya Mashariki ya Kati na kutatua mapema mgogoro kati ya Israel na nchi za kiarabu, wakuu hao walisisitiza tena kuunga mkono "Pendekezo la Amani ya Kiarabu", na kuona kuwa, pendekezo hilo linalingana na kauni za kimataifa, maazimio husika ya Umoja wa Mataifa na kanuni ya "ardhi kwa amani", na kusisitiza kuwa mgogoro huo unaweza tu kutatuliwa kwa njia hiyo.
"Pendekezo la amani ya Kiarabu" liliwasilishwa na Saudi Arabia na kupitishwa kwenye mkutano wa Beruit mwaka 2000. pendekezo hilo linaItaka Israel iondoke kwenye ardhi yote ya waarabu iliyokaliwa na nchi hiyo tangu mwaka 1967; kutambua uhuru wa nchi ya Palestina yenye mamlaka kwenye ardhi ya ukando wa magharibi ya mto Jordan na kanda ya Gaza, na mji wake mkuu ni Jerusalem ya Mashariki; na kutatua kwa haki suala la wakimbizi wa Palestina kwa kufuata azimio No. 194 la Umoja wa Mataifa na kanuni husika za kimataifa. Kwenye msingi huo tu, nchi za kiarabu zitatambua mgogoro kati ya Israel na nchi za kiarabu kumalizika na kukuza uhusiano wa kawaida na Israel ndani ya mfumo wa amani kamili.
Kutokana na hali hiyo, wakuu wa nchi za kiarabu waliohudhuria mkutano huo walitaka jumuiya ya kimataifa iunge mkono juhudi za nchi za kiarabu ili kutimiza lengo la amani, na kuunga mkono "Pendekezo la Amani ya Kiarabu". na Umoja huo pia utafanya majadiliano na Umoja wa Mataifa, Umoja wa Ulaya, Marekani na Russia kuhusu kutekeleza pendekezo hilo.
Aidha, azimio la Algiers pia linakaribisha uamuzi wa Syria kuondoa jeshi lake nchini Lebanon, kuunga mkono makubaliano ya amani kati ya serikali ya Sudan na makundi ya kijeshi ya nchi hiyo na juhudi za serikali ya nchi hiyo kuhusu suala la Darfur, na kutaka kuwasaidia watu wa Iraq waharakishe mchakato wa ukarabati wa nchi na kurejesha usalama na utulivu nchini humo.
Kuhusu mageuzi ya umoja wa nchi za kiarabu, azimio hilo linaona kuwa, mageuzi kamili na mwafaka ya umoja huo yatasukuma mbele mchakato wa mambo ya kisasa ya nchi za kiarabu, kulingana na maslahi ya waarabu wote, na kusaidia umoja huo kufanya kazi kubwa zaidi katika mambo ya kikanda na kimataifa. Mkutano huo ulisifu maendeleo yaliyopatikana katika mageuzi ya umoja huo, na kupitisha mswada wa mageuzi ya umoja huo uliowasilishwa na mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa umoja huo.
Wachambuzi wanaona kuwa, mkutano huo haukupata maendeleo mapya kuhusu mbinu za kutatua suala la Mashariki ya Kati; mageuzi ya umoja wa nchi za kiarabu yako kwenye maandishi tu, na hayajachukua hatua yoyote halisi.
Idhaa ya Kiswahili 2005-03-24
|